Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza nianze kumshukuru Mungu kwa kupata nafasi hii, lakini pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kupanga hii timu ya TAMISEMI ambayo inaanza na namba moja ile inayochezwa na Mheshimiwa Bashungwa; namba mbili anacheza Silinde; anafuata huyo anayeitwa Dugange; anafuata huyo anayeitwa Shemdoe; anafuata huyo anayeitwa Seif kwa TARURA. Nimpongeze tu Mheshimiwa Rais kwa kupanga hii timu. Sasa baada ya hii timu kupangwa inafanya vizuri, kwanza ni wanyenyekevu sana kwenye Wizara hii, ukipeleka matatizo ya wananchi wanasikiliza na wanafanya hii kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niwaombe leo kupitia hotuba hii wajinyenyekeze zaidi katika kusikiliza, lakini muwe wakali kwa watendaji hasa kwenye maeneo yetu ya kazi ili nchi iende vizuri. Hizi pongezi nataka niziweke vizuri kabisa ili waelewe na kwa kweli wanafanya kazi kubwa na kutokana na fedha ambazo zimekuja katika Majimbo yetu hasa Mbulu Vijijini nishukuru kwa ajili ya hilo. Niliomba fedha za kumalizia hospitali ya halmashauri, wamepelekea juzi na imeingia, nawashukuru kwa hilo. Biblia inasema; moyo usioshukuru ukarudisha mema mengi, nawashukuru kwa niaba ya wananchi wa Mbulu Vijijini kwa haya waliyotutendea sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa TARURA, nimeshukuru wameongeza fedha, ila kuna ombi ambalo tumeleta maalum Mbulu Vijijini, liko Daraja la Hudaya ambalo linaunganisha kata nne Kata ya Masieda na Kata ya Endagichani na kwa upande wa Mji wa Mbulu, lakini sasa shida iliyoko pale daraja lile likijaa wanafunzi hawaendi kabisa shule na nimeleta picha nimeleta video kwa ajili hiyo tu, niwaombe sana muone kama kuna namna ya special (maalum) watenge fedha kwa ajili ya pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa daraja lile lisipojengwa wanafunzi hawawezi kwenda shule, wametupa milioni 600 ya kujenga shule ya sekondari kwenye Kata ya Endagichan. Vifaa haviwezi kwenda kwa sababu ya mvua daraja lile halipitiki. Naamini kutokana na usikivu na unyenyekevu wa ndugu hawa ambao wameteuliwa na Mheshimiwa Rais watafanya haya ninayoyasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi niende kwenye suala la afya. Tuna kituo ambacho kimejengwa na wananchi Kituo cha Maretab, naomba sasa waone namna ya kuwasaidia wananchi wale kwa kuwapelekea fedha. Pia Kituo cha Afya cha Masieda wananchi wameshajenga, kule kwetu tunajichangisha wenyewe kwa kujenga hivi vituo vya afya. Basi waone namna gani ya kuendeleza mchango huu wa wananchi kwa kuwapelekea fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni hili la Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji. Kama unavyojua Mwenyekiti wa Vitongoji kesi ya kwanza ya ndoa kabla ya kukufikia wewe Mbunge inafika kwake, wanafanya kazi nzuri. Naomba basi Wizara ione namna gani ya kufanya, hata namna ya kuona tu, najua hali ya bajeti ni tata kidogo, lakini wawawekee fedha kidogo ku-appreciate utendaji wao wa kazi ili angalau Mwenyekiti wa Kitongoji aone kwamba alaa! Nimetambuliwa na Serikali na naamini kwa mama Samia Suluhu Hassan watatekeleza hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mwenyekiti wa Kijiji, anafanya kazi Januari to Desemba, anatoka tupu, niombe hili kama Wabunge tumelisemea na naomba tuendelee na TAMISEMI walione hili, wawatengee kidogo, lakini pia Madiwani posho zao zimeonekana posho tu, mshahara ni haki ya mtumishi yeyote, wanapokwenda kwenye halmashauri unakuta mtumishi ana fedha za mshahara wa kwake, lakini Diwani ana posho tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la msingi sana nimeshaongea na Waziri na naomba niliseme hapa, Madiwani wanalipwa sitting haina shida hiyo iko kwa mujibu wa sheria, lakini posho zina tofauti diwani wa angle nyingine analipwa Sh.100,000, mwingine analipwa Sh.40,000, mwingine analipwa Sh.30,000, kwa nini hizi hela zisiwekwe kwa uwiano wa nchi nzima kila Diwani awe wa Temeke, Manyara au Bukoba walipwe sawasawa kama watumishi wengine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe TAMISEMI wajipange waweke flat rate ili Diwani ajulikane huyu Diwani siyo mwingine anaonekana Diwani maalum, mwingine special, hata wao wameanza kuchanganyana kule, mwingine anaonekana yuko maalum sana kwa sababu anatoka mbali, mwingine anaonekana yuko namna Fulani, kwa hiyo tuunde utaratibu, waweke kwenye kanuni, wazilete hapa tuone namna ya kufanya, wawe kwenye level moja tu ili kila mtu ajue huyu ni Diwani ana stahili hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine najua tunakwenda kuajiri, naomba ajira hizi zinapotoka zitoke kwa uwiano waone mikoa yetu ambayo imesahaulika kule watupelekee hizi ajira na wakati wanazigawa ajira hizi Walimu wa sayansi ndugu yangu Mheshimiwa Bashungwa, kule kwetu hali ni mbaya, ziko sekondari ambazo hakuna kabisa Walimu wa sayansi, nikisema sayansi nafikiri Waziri ananielewa. Tuna upungufu wa Walimu 900 kwenye Jimbo zima, lakini tuna Walimu 37 tu wa sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu fikiria kwenye Jimbo hilo la Mbulu Vijijini, kama kuna upungufu wa namna hiyo, ni hatari sana. Kwa hiyo ufaulu wetu unategemea nini? Hautegemei moja kwa moja Walimu, ile 25% inayosemwa kitaaluma tunaikosa. Kwa hiyo niombe ndugu yangu Mheshimiwa Waziri aliangalie eneo hilo na atusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ahadi ya viongozi ambayo imeahidiwa katika wakati mzuri kabisa wa Mheshimiwa marehemu John Joseph Pombe Magufuli, kilomita tano za lami katika Mji wa Hydom, tunashukuru zimejengwa 1.8, lakini vizuri sasa basi ahadi za viongozi zikapewa kipaumbele ili zitimizwe na hii itasaidia sana kuonekana kuwa, viongozi wetu wanavyoahidi huwa inatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi, niombe pia yapo maeneo muhimu ambayo tunapaswa kuyaona vizuriā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Najua muda umekwisha, ahsante sana. Nitapeleka mchango wangu kwa maandishi. (Makofi)