Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii. Pia nawashukuru wananchi wa Urambo kwa ushirikiano wanaonipa pamoja na familia yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Waziri Mheshimiwa Bashungwa na Naibu Mawaziri Mheshimiwa Silinde, Mheshimiwa Dugange na Profesa Shemdoe kwa kazi kubwa wanazofanya, Manaibu wake, Ndugu Mweli, Dkt Grace, Ntuli naweza kuwataja wote, nawajua kichwani nawajua kwa sababu wanafanya kazi kubwa sana wakina Dkt Ntuli mambo ya afya hayo, akina Engineer Seif, Komba wa TARURA wanafanya kazi, jamani tuwapigie makofi TARURA wanafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana, wanafanya kazi kubwa, hii Wizara ni kubwa, Mheshimiwa Waziri anajua Wizara yake ni kubwa sana, lakini nawapongeza sana. Pia nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuongoza Serikali ya Awamu ya Sita, ametoa misaada mingi sana siwezi kusahau, jinsi ambavyo ametusaidia Urambo, ametupa vituo vya afya vingi, ametupa madarasa mengi. Tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu, ampe afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi tu kwa niaba ya wananchi wa Urambo ni kwamba kutokana na madarasa mengi tuliyopata tuna upungufu wa Walimu zaidi ya 600 ambapo tutashukuru sana Serikali ikitupa ili kazi nzuri iendelee. Pia kwa upande wa afya tumepata vituo vya afya, zahanati, tunahitaji wafanyakazi zaidi ya 269, kwa hiyo tutashukuru sana kama Serikali ikituwezesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo ambayo nawaunga mkono wenzangu ambao tayari wameshaongea, kwa mfano, kuwaongeza posho Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Vijiji na Madiwani. Hawa wanafanya kazi kubwa sana, naomba kweli suala lao lizingatiwe ili waweze kumudu kazi zao vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo naunga mkono wenzangu wote, kulikuwa na Mheshimiwa Mbunge alizungumzia juu ya chakula cha mchana, naomba sana suala la chakula cha mchana litolewe mwongozo kwa sababu watoto wengine wanatoka mbali, ni vizuri kukawa na chakula cha mchana. Wakati huo huo tumekuwa tukiomba sana suala la taulo za kike kwa ajili ya watoto wa kike. Kwa hiyo tunaomba suala la taulo za kike ziweze kupatikana kutokana na fedha za halmashauri. Suala ni mipango tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimesikia wengi wakizungumzia kuhusu wafanyakazi wanaopelekwa vijijini. Mtu anapelekwa kijijini kwa style ya kizamani, wanawekwa kwenye malori halafu wanashushwa wanaambiwa wewe shuka hapa, mtu hapajui na wengine hata shule yenyewe haijui au kituo cha afya hakijui. Kwa hiyo napendekeza hivi, Ofisi hii ya Rais TAMISEMI watoe mwongozo wa jinsi ya kupokea wafanyakazi, kuwe na mpango maalum wa kupokea wafanyakazi, siyo lazima hela tu, lakini wanaweza kuweka utaratibu wa kuandaa nyumba ambayo wanajua akifika, atakaa, atalipa mwenyewe lakini kuwe na maandalizi ambayo yatamfanya mfanyakazi asijisikie kufanya kazi, kuliko wanavyofanya style ambayo mtu anashushwa tu porini anaambiwa nenda kule utaiona shule au utaona kituo cha afya. Kwa hiyo nafikiri kuwe na maelekezo ya jinsi ya kupokea wafanyakazi wanapokwenda kwenye vituo vyao vipya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikienda kwa upande wa Walimu; Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia juu ya uhaba wa Walimu, wamesema wengi sana na mimi mwenyewe nimesema tunahitaji Walimu zaidi ya 600; Walimu 547 kwa upande wa msingi na Walimu 152 kwa upande wa sekondari. Kwa hiyo zaidi ya Walimu 600, lakini sasa nafikiria jinsi Walimu wanavyozidi kuwa wengi kulikuwa pia na haja ya kurudi kuiangalia Tume iliyoundwa ya Walimu kwa ajili ya kuwashughulikia Walimu ambayo inaitwa TSC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Kamati ya USEMI tuliomba tathmini ifanyike kuhusu Tume inayohudumia Walimu kutokana na wingi wao na maeneo wanayofanyia kazi, lakini naishukuru sana ofisi ya Mheshimiwa Bashungwa kwa sababu wamesema ukweli kwamba kazi ya kuichunguza TSC kuona kama inafanya kazi yake iliyokusudiwa haikufanyika ipasavyo.

Kwa ruhusa yako naomba nisome kitabu; kazi za Tume ya Walimu (TSC) wameeleza vizuri kabisa kwenye Dhima, kuhakikisha Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari wanapata huduma bora kuhusu masuala ya ajira, kupandishwa vyeo na kukuza maadili. Halafu wakaanza kuzichambua zile kazi, siwezi kusoma zote kwa sababu ya muda, nimechagua tatu tu wanasema kuajiri, kupandisha vyeo na kuchukua hatua za nidhamu kwa walimu; Kuhakikisha uwiano sawa katika usambazaji wa Walimu ndani ya Serikali za Mitaa na shule. Hivi ndiyo kazi wanazofanya hawa? Halafu (g) Kusimamia program za mafunzo ya Walimu kazini, hizi ndiyo kazi baadhi ya kazi ambazo zimetajwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nampongeza sana Waziri kwa sababu ile Tume iliyofanya hii kazi wamekuwa wakweli sana, wamefanya tathmini ya TSC na wenyewe wameeleza vizuri kabisa wanasema hivi, wao wenyewe, kwamba, Sekretarieti ya Tume imejitathmini yenyewe na ni vyema utafiti mwingine ukafanywa kwa kutumia watathmini wa nje ili kuangalia kwa jicho la mtu mwingine bila kuwepo na upendeleo namna Tume ilivyofikia kusudi la kuanzishwa kwake. Wao wenyewe kabisa wameomba Tume nyingine iundwe. Kwa hiyo napendekeza Tume nyingine iundwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wao wenyewe wamekubali kwenye kitabu chao, muda wa kufanya utafiti huu ulikuwa mfupi sana na pia kulikuwa na uhaba wa fedha za kufanyia utafiti. Ili uweze kukamilika kwa wakati, ni matumaini yetu kwamba katika tafiti nyingine muda pamoja na uwezeshwaji utolewe wa kutosha.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Magreth Simwanza Sitta.

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sekunde moja nimalizie.

MWENYEKITI: Basi nakuongeza dakika moja, lakini muda wako ulikwisha.

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kwa kazi yao nzuri sana, wanasema hivi; (3) Tafiti kama hizi ziendelee kufanyika ili kuweza kumshauri kikamilifu Waziri kuhusu masuala ya ajira, maadili na maendeleo ya Walimu, kwa sababu mpaka sasa TSC bado kazi zingine hazifanywi vizuri ili kuwahudumia Walimu kutokana na wingi wao waweze kufanya kazi vizuri, walipwe haki zao kwa wakati ili watumikie vizuri kwa sababu elimu ndiyo namba moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, lakini naamini Mheshimiwa Waziri hii kazi atafanya tena. Ahsante sana. (Makofi)