Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii. Nianze kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mawaziri wake wote wanaomsaidia, Manaibu Mawaziri, Katibu Mkuu wa Wizara hii na Manaibu pia kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa kuwahudumia wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuchangia kwa kuanza na TAMISEMI. TAMISEMI ambayo ndiyo Wizara tunayoichangia na kwenda kuanza na TARURA. TARURA inafanya kazi nzuri sana katika kipindi hiki ambacho imepewa fedha baada ya sisi Wabunge kusema sana katika Bunge hili. Kumekuwa na changamoto, tumepewa fedha shilingi bilioni 1.5 iliyotolewa na Mheshimiwa Rais na tulitangaziwa kwenye Bunge hili. Hata hivyo, naweza kusema wakandarasi ambao wamepewa kazi katika kipindi hiki hasa kwenye jimbo langu kuna changamoto kubwa.

Mheshimiwa Spika, nalisema hili kwa sababu imekuwa ikileta matatizo makubwa kwa wananchi kwa sababu tangu mwaka jana fedha zipo kwenye akaunti wakandarasi wamepewa kazi, wakandarasi ni dhaifu, hawafanyi kazi, matokeo yake wananchi wanalalamika usiku na mchana. Hapa ninapozungumza wananchi wa Kata ya Kihutu wameandamana ambao tumewaambia kwenye mikutano kwamba barabara inatengenezwa toka mwaka jana, wanasema, Mheshimiwa Rais utusaidie Mkandarasi hayupo kazi, wanaona sisi ni waongo, hatufanyi kazi, tunawadanganya kwenye mikutano ya hadhara, wakati Serikali imeshatoa fedha, lakini udhaifu wa wakandarasi. Naomba TARURA waliangalie jambo hili kwa sababu wanatudhalilisha. Fedha za UVIKO zimekuja juzi tu miradi ilishatekelezwa kwa kiwango kikubwa kwa sababu ya usimamizi mzuri. TARURA wanafanya kazi nzuri lakini wakandarasi wanawaangusha, hawafanyi kazi na sisi wanatudhalilisha.

Mheshimiwa Spika, naomba pia katika mgao wa fedha za TARURA kwa majimbo tuangalie kwa sababu kuna majimbo ambayo ni magumu sana kama Jimbo langu la Arumeru Magharibi. Jimbo langu la Arumeru Magharibi lina makorongo, barabara zake zote ni mbovu, kwa hiyo naomba katika mgao watuangalie kwa jicho la huruma kwa sababu wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi na majimbo mengine makubwa, kwa kweli wanahitaji fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba barabara zinatengenezwa. Barabara katika Jimbo langu ni kilometa 685 za changarawe. Sasa kwa fedha ambazo tunazipata ni kidogo sana kwa hiyo naomba mtuangalie.

Mheshimiwa Spika, niende kwenye ahadi za Rais ambazo Mheshimiwa Rais amezitoa katika Jimbo la Arumeru Magharibi na katika majimbo mengine yote. Naomba ahadi hizi ambazo zinatolewa na Mheshimiwa Rais ziangaliwe sana kwa makini na Waheshimiwa Mawaziri katika kuingiiza kwenye mipango yao. Kwa sababu mwisho wa siku Taasisi ya Rais inaonekana kwamba haiheshimiwi na wananchi pale inapotoa tamko kwamba itatekeleza jambo fulani, kwa mfano, Mheshimiwa Rais kwenye Jimbo langu ameahidi ukarabati na marekebisho makubwa kwenye Hospitali ya Wilaya ambayo yeye ameizindua, kwamba itaongezewa majengo, itawekwa na kila kitu lakini tangu Serikali ianze kugawa fedha za Hospitali za Wilaya, Hospitali hiyo ya Wilaya ya Oturumeti Arusha DC haijawahi kupata hata shilingi moja kutoka Serikali Kuu.

Mheshimiwa Spika, naomba Waziri atakapokuja kufanya majumuisho aniambie ni lini atapeleka fedha kwa ajili ya kuboresha hospitali hiyo. Vinginevyo nitashika mshahara wake kwa sababu wale wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi nao wana haki katika mgao wa fedha za hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kujenga barabara kilomita tatu katika hospitali hiyohiyo, Rais ametoa ahadi hiyo hadi leo hakuna namna ambayo kuna namna ambayo wanatekeleza ahadi hiyo ya Rais. Siyo kwangu tu na kwa majimbo mengine yote, lazima sasa wafike mahali Mawaziri wote ahadi za viongozi wetu ambao wanazitoa kwa kuwajengea heshima na hasa Taasisi ya Rais ambaye ndiye msemaji wa mwisho katika Taifa hili na ndiyo tumaini la wananchi anaposema jambo lazima zitekelezwe. Kwa hiyo naomba ahadi za Rais ziwekwe kwenye kitabu maalum kitakachoonyeshwa kila Bunge kwamba zinatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna zahanati ambazo hazijakamilika mmetuma milioni 50, lakini bado tunaomba TAMISEMI warudie tena kutoa fedha kwa ajili ya zahanati hizo na vifaa tiba pia.

Mheshimiwa Spika, posho za Madiwani na Wenyeviti wa Vitongoji; hawa watu wanafanya kazi kubwa sana kwenye majimbo yetu na kwenye halmashauri zetu. Wao ndiyo wanasimamia miradi yote, wao ndiyo wanasimamia Ilani ya Chama cha Mapinduzi lakini kwa mshangao mkubwa tunasema tunawapa posho. Ifike mahali sasa Madiwani hawa wapewe mshahara kama watu wengine, wanafanya kazi kubwa. Kuna zile shilingi 350,000 ambazo wamesema wametoa shilingi 100,000 kwa ajili ya kuwapa watendaji, hizi fedha nazo waziweke kwa ajili ya Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji waweze kupata posho. Serikali sasa iangalie Madiwani kwa sababu wanateseka, hawana uwezo wa kuwasimamia watu wanaolipwa shilingi 700,000 au shilingi 800,000 na wao wanapata mshahara lakini wao wanafanya kazi kama wanafanya bure, halafu tunawatumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakwenda kuingia kwenye eneo la chakula mashuleni. Tunasema watoto wafaulu, ni mtoto yupi anaweza kukaa kuanzia asubuhi hajala chochote lakini unategemea afanye vizuri au amsikilize Mwalimu? Naomba eneo hili TAMISEMI waliangalie na watoe waraka maalum na unaoelekeza namna ya watoto kupata chakula shuleni kwa lazima, kwa sababu ndiyo tunatengeneza Taifa la watoto ambao wanakuwa na kwashiorkor, kwa sababu haiwezekani mtoto kukaa kuanzia asubuhi bila kula chakula alafu tunaona ni jambo la kawaida.

Mheshimiwa Spika, suala la mfumuko wa bei. Kule vijijini kwa sasa hizi hali ya vyakula, vitunguu, nyanya, chumvi, mafuta ya kula, hali ni tete. Kwa hiyo naomba waende waangalie Serikali watoe namna kwamba kuna wafanyabiashara baadhi ambao wanapandisha bei eti tu kwa sababu wamesikia mafuta yamepanda. Naomba Serikali ifanye uchunguzi ili iwape wananchi maelezo na matumaini ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, suala la bajeti hii kutekelezwa. Lazima bajeti hii itekelezwe bila kuwepo na wizi, rushwa, ufisadi na ujanja ujanja. Bajeti ikitekelezwa bila rushwa tutatekeleza vizuri.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kila mmoja achukie rushwa, wizi na ufisadi ili mwisho wa siku Taifa hili lipone. Ahsante sana. (Makofi)