Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwa ajili ya kuiletea nchi yetu maendeleo. Pia nichukue nafasi hii kuwapongeza Wizara ya TAMISEMI kwa kazi kubwa wanayoifanya katika majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo ningependa kuongelea suala la TARURA. Kwanza nawapongeza sana TARURA kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya, hususan kwenye Jimbo la Segerea. Pamoja na pongezi hizo kwa kazi kubwa wanayoifanya TARURA Jimbo la Segerea au Wilaya ya Ilala, kuna mambo mengi au kuna barabara nyingi ambazo ningependa kwa mwaka huu TARURA waziangalie. Kuna barabara nyingi sana ambazo TARURA wamezijenga na wamebakisha vipande vidogo vidogo sana. Ukichukulia kama barabara ya Kata ya Liwiti, barabara ya Chang’ombe, wamejenga kilomita moja lakini imebaki kipande kidogo sana. Kwa hiyo, naomba kwa mwaka huu wa bajeti TARURA waweze kumaliza hicho kipande. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna kipande kingine ambacho kinapita Kisukulu, kuelekea Bonyokwa, naomba na hicho kipande kiweze kumaliziwa kwa sababu ni vipande vidogo vidogo sana. Haiwezekani kipande kama cha kilomita moja kikakaa kwa muda wa miaka mitatu yaani kuna na barabara kilomita mbili wameitengeneza ya lami, lakini kuna na barabara ndogo sana ambayo wameiacha, kwa hiyo ile barabara ya kilomita mbili ambayo wametengeneza na kuaca kipande kidogo hicho kinaondoa kabisa maana ya ile barabara waliyotengeneza. Kwa hiyo, nawaomba TARURA, hivi vipande vidogo vidogo katika Jimbo la Segerea, waweze kuvimaliza kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine nilitaka kuongelea kuhusiana na Miradi ya DMDP. Tumezungumza hapa mwaka 2021 nikiongelea Bonde la Mto Msimbazi kwamba litaanza kujengwa mwezi wa Tatu mwaka huu, lakini mpaka sasa hivi halijaanza kujengwa. Bonde la Mto Msimbazi lilikuja na barabara zake ambazo tulikuwa tumeahidiwa na wataalamu wetu kwamba litajengwa pamoja na barabara ambazo zimefuatana, nikiongelea barabara ya Segerea - Seminari ipo kwenye mradi wa Bonde la Msimbazi na pia ukichukua barabara ya Kisukulu – Maji Chumvi – Migombani, ipo kwenye Bonde la Mto Msimbazi. Mpaka sasa hivi tunavyoongea, bado hili Bonde la Mto Msimbazi halijaanza kujengwa wala hizi barabara hazijaanza kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na nimemwulizia sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa sababu ndiyo walikuwa wanapitisha huu mradi wa DMDP, mpaka sasa hivi hatujajua. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu, kwa sababu sisi tayari tulishawaahidi wananchi kwamba itakapofika mwezi wa Tatu litaanza kujengwa.

Mheshimiwa Spika, kama unavyojua, Mkoa wa Dar es Salaam mvua kidogo ikinyesha au isiponyesha Dar es Salaam, ikanyesha sehemu nyingine, yale maji yanapita kwenye Bonde la Mto Msimbazi na kwa sababu ya miundombinu chakavu iliyopo katika Jiji la Dar es Salaam, yale maji yanawafuata wananchi. Zamani tulikuwa tunasema kwamba Bonde la Mto Msimbazi watu wamejenga karibu na bonde, lakini hapana, ni kwa sababu lile bonde sasa hivi limekuwa chakavu sana, kwa hiyo, maji yanaenda kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tulikuwa tunaomba sana majibu, tutakapomaliza huu Mkutano wetu wa Bajeti, tunarudi kwa wananchi na watatuuliza, mlituahidi kwamba Bonde la Mto Msimbazi litaanza kujengwa, lakini halijaanza kujengwa mpaka sasa hivi pamoja na hizo barabara nilizozitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna barabara moja ya Banana - Kitunda – Kivule ambayo inapitisha zaidi ya magari 3,500 kwa siku. Nimeona hii barabara ni ambayo ni ya lami, sasa hivi imetengewa shilingi milioni 560 kwa ajili ya kuiwekea changarawe. Sasa utaona kwamba barabara iliyokuwa ya lami inarudishwa kwenye changarawe; na hii barabara mwaka 2021 ilitengewa shilingi milioni 400, ikatengenezwa kwa changarawe; na mwaka huu imetengewa shilingi milioni 560 inatengenezwa kwa changarawe.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri aweze kuangalia barabara zetu ambapo kuna maeneo ambayo wananchi wengi wanaishi. Mfano kama hii barabara ninayoisema, ina kilometa 12.5 na wananchi ambao wanaishi kule ni zaidi ya 300,000. Kwa hiyo, sasa ukisema kwamba unaitengea barabara shilingi milioni 560 ili iwekewe changarawe, bado hujatatua tatizo, kwa sababu baada ya hapo, mvua itakaponyesha, ina maana matatizo yataendelea. Kwa hiyo, tulikuwa tunamwomba Mheshimiwa Waziri, kwa sababu barabara hii ipo katika mradi wa DMDP, tunaomba huo mradi uweze kusainiwa mapema ili hizi barabara ziweze kujengwa. Barabara zetu… (Makofi)

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Bonnah Kamoli, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Mtemvu.

T A A R I F A

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa mzungumzaji juu ya DMDP. Ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam siyo tu eneo hilo analolizungumza la nyimbo la Segerea, lakini hata kwenye Jimbo la Kibamba ahadi ilitokea kilometa 107 mwaka 2020 mbele ya Rais aliyepo sasa akiwa Makamu wa Rais kwamba zitajengwa na DMDP III lakini mpaka sasa bado kuna mtu kakalia kwa miezi minne kusaini mkataba huo. Ni kweli nakuunga mkono ili tupate majibu Mheshimiwa Waziri akija kutoa hoja.

SPIKA: Mheshimiwa Bonnah Kamoli, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hiyo. Nami nataka niongezee tu kwamba, sisi wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam tukija hapa tunaomba barabara na maji. Tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri aangalie ni jinsi gani atatuboreshea barabara zetu ambazo tunaona zinawasaidia wananchi kwa ajili ya kufanya shughuli zao za maendeleo za kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, barabara hizi tulizosema kwamba zimeingia kwenye mradi wa DMDP, ni barabara kubwa. Mfano, hiyo barabara moja ambayo inatoka Kimanga ya kilometa 3.5, obvious huwezi kuiweka kwenye TARURA, itachukua muda mrefu. Tuna barabara nyinginye ya Bonyokwa - Kimara ambayo ina kilometa 4.6, na yenyewe pia imewekwa kwenye mradi DMDP. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba hizi barabara ambapo hatuombi zote zitengenezwe lakini hizi ambazo zitawasaidia wananchi waweze kufanya shughuli zao kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine nilichokuwa nataka kuongelea, kwanza niishukuru wizara kwa kutujengea vituo vya afya Kinyerezi, Segerea pamoja na Kiwalani. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri Jimbo la Segerea ndiyo lenye wananchi wengi Tanzania nzima. Kwa hiyo, kuwa na Kata ambayo haina hata zahanati inakuwa ni changamoto sana. Kwa sababu unakuta Kata moja; mfano, Kata ya Buguruni ina wananchi karibu 300,000, lakini hawana zahanati. Kwa hiyo, tunaomba wapate zahanati. Pia Kimanga pamoja na Kisukulu, hizi Kata zote hazina zahanati. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aje na haya majibu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)