Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii ya uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ya TAMISEMI ndio ina jukumu kubwa sana katika ustawi wa maisha ya wananchi kwa kwa sababu ndio inagusa moja kwa moja kila kitu ambacho kinafanyika kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la fedha kutengwa na fedha kwenda na zikishakwenda kule kwenye halmashauri zetu, zile fedha zinatumika sawasawa? Hiyo ndiyo hoja ya msingi. Kodi ya wananchi ambayo inakwenda kule tunataraji iendee ikatekeleze miradi ya maendeleo yenye tija kwa wananchi swali la kujiuliza je, zile fedha zikifika kule, zinafanya lile ambalo limekusudiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukisoma ripoti ya CAG hii aliyoiwasilisha juzi kwenye miradi ya maendeleo ukurasa wa 137 CAG anasema kumefanyika uwekezaji wa bilioni 533.68 ambao hauna tija. Uwekezaji huu umefanyika kwenye mambo gani? Uwekezaji huu umefanyika kwenye ujenzi wa masoko, kwenye ujenzi wa vituo vya mabasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakutolea mfano mdogo kule kwetu Mtwara, kuna soko limejengwa linaitwa Soko la Chuno, limejengwa kwa kodi ya Watanzania bilioni 5.5. Kwanza katika hali ya kawaida, unaweza kujiuliza huyo mtu ambaye alikuwa amependekeza lile soko lijengwe kule alikuwa anawaza kitu gani? Ni tofauti na uelekeo wa watu wanakoelekea, watu wanaokaa kule ni wachache, kwa sababu sisi Watanzania tumezoea, unatamani sokoni unatoka kwenye shughuli zako you just go there una-pick unaondoka. Sasa kama amekujengea tofauti na uelekeo wa watu wengi wanaokaa unategemea hilo soko wateja wake wanatokea wapi? Maana yake nini bilioni 5.5, zimelala pale, hazina tija. (Makofi)

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Tunza Malapo kuna taarifa kwa Mheshimiwa Kunti Majala.

T A A R I F A

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru napenda kumpa taarifa mzungumzaji, kwamba changamoto iliyoko Mtwara haina tofauti na changamoto ya Jiji la Dodoma. Soko limejengwa Nzuguni, lakini ukiangalia kata nyingi zilizoko zipo upande huu wa magharibi, kwa hiyo, uwekezaji unaofanywa na Serikali na wataalam wetu wanao- design miradi hii wamekuwa wakipoteza kodi kubwa za Watanzania pasipokuwa na tija. Nakushukuru ilikuwa atambue tu hilo Mheshimiwa mchangiaji anayeendelea.

SPIKA: Mheshimiwa Tunza Malapo, unapokea taarifa hiyo?

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa mikono miwili. Serikali inachotakiwa kufanya ni kujitathmini kwa sababu hizi ni kodi za wananchi, tunataraji ziende zikawekeze kwenye miradi ambayo ina tija. Kabla Serikali haijapeleka fedha nyingi kiasi hicho, ifanye tathmini hapa tunapokwenda kuwekeza uwekezaji huu utaleta tija. Hilo ni suala la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili, tukienda kusoma ripoti ya CAG hii mpya siyo kwamba kila mwaka hakuna ubadhirifu, lakini hii nayo imesheheni kwa ubadhirifu. Kila ukienda kwenye halmashauri shida ni watu wanapiga fedha, maana yake ni nini? Wizara inatakiwa ijitathimini ina Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, waende wakafuatilie fedha zinazopelekwa. Nikupe mfano mwingine mdogo, nili-take time nikasoma, kule kwetu Mtwara kulikuwa na mradi wa kufunga taa za barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye mkataba, nakupa mfano mdogo, kwenye ripoti ya maendeleo ukurasa wa 54, ripoti ya CAG, malipo ya ziada ya taa za barabarani Mtwara hiyo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani; taa moja ilitakiwa ilipwe milioni 7.5, taa moja imeendwa kulipwa milioni 18,142,000, hata kama ni tofauti kwamba bei imeongezeka, bei imepanda kutoka milioni saba mpaka milioni 18.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo fedha zimepotea shilingi milioni 588, si zinajenga kituo cha afya kabisa hizi, kwa sababu kituo cha afya kilikuwa kinajengwa kwa shilingi milioni 450 mpaka 500, hizi mtu kalipwa tu kwa matakwa ya watu wachache. Ndio maana nimesema pamoja na hizo fedha kidogo ambazo zinakwenda, wao kama Wizara wana kazi kubwa sana ya kufuatilia kuhakikisha fedha zinazokwenda kule zinaleta tija kwa wananchi. Naambiwa Mawaziri vijana, maana yake vijana tunatambua mchakachaka, wanapaswa wakimbie. Kama walikuwa wanakimbia kwa speed mia moja, inatakiwa waende mia moja ishirini, mia moja hamsini. Hali huko, chini sio shwari sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee issue ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu; kwa mwaka huu wa fedha hii bajeti tunayokwenda kuipitisha, sina uhakika kama itapita, hii bajeti ambayo tunaijadili sasa hivi kwa makusanyo ya ndani asilimia 10 ikitengwa kwenye halmashauri ni bilioni 75.98 zinatakiwa ziende kule kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, hoja ni kwamba, Wizara inatakiwa ifanye tathmini, je, hizi fedha nyingi zinazokwenda kule, kweli zinabadilisha maisha ya wananchi hawa? Tusiseme tu zinatengwa, zinaenda na zingine, hazirudi, zinakwamia wapi? Wakati tuko kwenye Kamati kwa sababu ni mjumbe wa Kamati hiyo wakati tupo kwenye Kamati tumemweleza mengi, waende wakafanye utaratibu wa kuhakikisha fedha hizi zinakwenda kuleta tija, zile ambazo hazieleweki, ziliko zirudi kwa sababu zote walipewa watu hazikupotea angani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nina suala moja, vitu huko mtaani vimepanda bei. Naomba Serikali ifanye tathmini, sasa hivi ndio wa wale wachumi wetu, wale maprofesa wa uchumi waliopo Tanzania watuambie hivi mafuta, kwa mfano, mafuta ya petrol yameongezeka labda kwa shilingi 500 mpaka 800 ndio inahalalisha mafuta ya kula leo ndoo ya lita kumi iliyokuwa inauzwa 28,000 iuzwe 70,000? Hivi vitu haviendani mafuta ya gari yamepanda sawa, lakini kwa hicho kiwango ambacho yamepanda yanahalalisha leo, kitu kilichokuwa kinauzwa 10,000 kiuzwe 30,000? Ndio hoja yangu ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nafikiri watuambie tu kuna remedy gani ambazo zinaweza zikafanyika. Mimi Mtanzania wa kawaida ungeniuliza nikiona maisha yangu magumu, naacha kujenga, naangalia watoto wangu wale na watibiwe. Kwa hiyo watu wa uchumi washauri nchi, sasa hivi mtu akipata 10,000 anajiuliza 10,000 hii nitafanya nini ili aweze kula na watoto kwa namna vitu vilivyopanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, muda ni mchache na mambo ni mengi. Ahsante sana. (Makofi)