Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kassim Majaliwa Majaliwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza kabisa nami niungane na wenzangu waliotangulia kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa rehema na kutujalia siha njema na kutuwezesha kukutana hapa kwenye Kikao hiki cha Sita, Mkutano wa Saba wa Bunge la 12, kwa ajili ya kuhitimisha mjadala huu kuhusu hoja ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kwa kumshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, kwa Miongozo yake mizuri iliyowezeshwa ofisi ya Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yake na kulifanya Taifa letu kufanya maendeleo hadi leo hii. Pia niendelee kumshukuru Mheshimiwa Daktari Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia anamsaidia kazi Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan naye kwa kutoa Miongozo kwa ofisi ya Waziri Mkuu na kuwezesha ofisi ya Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yake vilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nikushukuru sana wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kuongoza vyema mjadala kuhusu hoja ya Bajeti, ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023. Pia niendelee kutoa shukrani zangu za dhati kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Kamati ya Kudumu yaBunge ya Bajeti na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kwa kazi kubwa waliyoifanya ikiwemo kutoa michango yao yenye tija kwenye hoja ya Waziri Mkuu, nawashukuru sana Wajumbe wa Kamati zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia tena kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri wa ofisi ya Waziri Mkuu, Mawaziri wa Sekta waliyochangia hoja za Bajeti ya Waziri Mkuu, Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Idara, Mashirika, Wakala wa Taasisi za Serikali kwa ushirikiano mkubwa katika kufanikisha hoja ya Bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, vilevile kipekee ninawashukuru sana watumishi wote wa ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri waliyoifanya na ushirikiano walioendelea kunipatia katika kipindi chote, hususan wakati wa maandalizi hadi kipindi tunapoelekea kuhitimisha mjadala wa Bajeti wa ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, nitumie vilevile nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa michango yenu muhimu, hakika mnaendelea kutekeleza kwa ufanisi majukumu yenu ya msingi ya kuisimamia na kuishauri Serikali, kwa kutoa michango mizuri yenye lengo la kuisaidia Serikali katika kutekeleza kikamilifu vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Serikali napenda kuwapongeza na kuwashukuru sana tena Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa hoja na michango yenye kujenga utendaji wetu Serikalini. Niwahakikishie kwamba Serikali itazingatia maoni yenu na ushauri wenu mlioutoa katika kutekeleza majukumu yatu ndani ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge 115 walichangia hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa mjadala huu. Kati yao, Waheshimiwa Wabunge 104 walichangia kwa kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge 11 walichangia kwa maandishi. Ninatoa shukrani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja ya Waziri Mkuu. Aidha, kutokana na ufinyu wa muda, ninaomba uridhie nisiwataje mmoja mmoja kwa majina na badala yake majina yao yaingizwe kwenye Hansard moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na mjadala wa hoja ya Waziri Mkuu, Serikali imetoa majibu ya hoja nyingi zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge, kupitia Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri. Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa muda Serikali itatoa majibu yenye ufafanuzi zaidi kuhusu hoja zilizosalia kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Spika, vilevile, wakati Waheshimiwa Mawaziri wakiwasilisha hoja za bajeti za sekta zao wataendelea kutoa ufafanuzi wa kutosha na kwa undani zaidi wa baadhi ya hoja ambazo zimeibuliwa kwenye mjadala huu chini ya ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, naomba niueleze mwaka mmoja wa Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, itakumbukwa kwamba tuna mwaka mmoja pekee tangu Mama yetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ashike hatamu za kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, katika kipindi hicho kifupi Tanzania imepata mafanikio lukuki ambayo yametufanya kuendelea kutembea kifua mbele na kujiamini.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mafanikio hayo ni kuendelea kuimarika kwa uchumi, shughuli za kijamii, ongezeko la mapato ya kodi, kurejea kwenye diplomasia na medani za kimataifa, kuongezeka kwa uwazi katika usimamizi mzuri wa sera za soko huria, sera za kiuchumi na kifedha sambamba na kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, makusanyo ya kodi, usimamizi mzuri wa sera za kiuchumi na fedha sanjari na kujenga mahusiano mazuri kati ya walipa kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kumechangia ka kiasi kikubwa kuimarika kwa mapato ya kodi. Kwa mfano, mwezi Desemba 2021, TRA ilikusanya Shilingi Trilioni 2.51 sawa na ufanisi wa asilimia 109 wa lengo la kukusanya Shilingi Trilioni 2.29 katika kipindi hicho cha Desemba. Kuvunjwa kwa rekodi hiyo ya makusanyo ya kodi ni kielelezo tosha cha kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Rais pamoja na Taasisi zote za ndani ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie Mpango wa Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19. Afrika inamtazama Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kuwa miongoni mwa viongozi waliochangia kuliweka Bara hili katika ramani nzuri ya dunia kutokana namna alivyofanikiwa kushughulikia suala la UVIKO-19.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango huu wa UVIKO-19 kwa Ustawi wa Taifa na Maendeleo dhidi ya UVIKO- 19 unaakisi dhamira ya Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha inaboresha sekta za jamii. Kwa mfano, sekta ya elimu, afya, maji, maliasili na utalii, pia ujasiriamali na hifadhi ya jamii kwa pande zote mbili za Muungano.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie mfano wa mkopo nafuu wa Shilingi Trilioni 1.3 usiokuwa na riba yoyote kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuonesha namna Mheshimiwa Samia, Rais wetu alivyofanya kazi kubwa katika kuboresha huduma za jamii pamoja na miundombinu ya usafiri na usafirishaji.

Mheshimiwa Spika, huduma za afya. Kupitia Mpango wa Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, Serikali ya Awamu ya Sita imetoa Shilingi Bilioni 204.4 kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali za afya. Afua hizo, zinajumuisha kuimarisha huduma za dharura, huduma za wagonjwa mahututi, wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu na huduma za maabara. Kwa upande wa vifaa na vifaa tiba, Serikali imenunua mashine za CT Scan 29, MRI Nne, magari 253 ya kubebea wagonjwa kwa lugha nyingine ambulance, magari 250 kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za afya ngazi ya Wizara, Mikoa na Halmashauri zote nchini, magari manane ya damu salama na magari 30 ya kusambaza chanjo.

Mheshimiwa Spika, huduma za Elimu. Nyote mtakubaliana nami kwamba katika mwaka 2022, tumeshuhudia wanafunzi wote 907,803 waliokidhi vigezo vya kujiunga na Kidato cha Kwanza wakichaguliwa kwa mkupuo mmoja tofauti na miaka ya nyuma ilipotulazimu kuwa na machaguo mawili na wakati mwingine hadi machaguo matatu.

Mheshimiwa Spika, hali hiyo imewezekana ndani ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya Serikali kutumia Shilingi Bilioni 240 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 12,000. Katika hatua nyingine ya kuboresha miundombinu ya elimu na kuhakikisha watoto wa kitanzania hawabaguliwi katika kupata elimu, Serikali imetumia Shilingi Bilioni 60 kujenga vyumba vya madarasa 3,000 kwenye vituo shikizi vya Shule za Msingi na hivyo kuondoa changamoto kwa wanafunzi wanaoshindwa kufika kwenye shule mama.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imepeleka Shilingi Bilioni 100.58 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za sekondari 214. Taratibu za kuanza ujenzi huo, zinaendelea kwenye Kata za Majimbo yote nchini. Aidha, Shilingi Bilioni 30 zimepelekwa kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari mpya za wasichana kwenye Mikoa 10, ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kujenga shule moja ya sekondari ya wasichana kila Mkoa wa Tanzania Bara.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la ufundi stadi, Serikali imeanza ujenzi wa chuo kikubwa cha ufundi Mkoani Dodoma ambapo Shilingi Bilioni 3.44 zimetumika. Ujenzi huo unakwenda sambamba na kuanza ujenzi wa vyuo vingine vinne vya ufundi stadi katika Mikoa ya Geita, Njombe, Rukwa na Simiyu ambayo haikuwahi kuwa na Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA).

Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali hapa ni kuhakikisha kwamba vijana wanapatiwa stadi za kazi na ujuzi ili waweze kuendesha shughuli zao za kiuchumi kwa kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana ndani ya nchi hii na hivyo kuondokana na changamoto ya upatikanaji wa ajira.

Mheshimiwa Spika, huduma za maji. Katika kutekeleza mpango wa kumtua ndoo mama kichwani, kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19, Serikali ilitoa Shilingi Bilioni 104 kwa ajili ya kutekeleza jumla ya miradi ya maji 218 nchini. Kati ya hiyo, miradi 172 inatekelezwa mijini na miradi 46 inatekelezwa vijijini. Miradi hiyo itaongeza idadi ya wananchi wanaonufaika na huduma ya maji safi na salama na yenye kutosheleza vilevile.

Mheshimiwa Spika, kiasi cha Shilingi Bilioni 17.5 zimetumika kununua seti 25 za mitambo ya kuchimbia maji, kwa maana ya kuchimba visima kwa Mikoa 25 ya Tanzania Bara. Aidha, Shilingi Bilioni 17.6 zitatumika kununua seti Tano za mitambo ya ujenzi wa mabwawa na vifaa vya utafiti wa maji chini ya ardhi ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo ambayo hakuna vyanzo vya uhakika vya maji.

Mheshimiwa Spika, miundombinu ya usafiri na usafirishaji. Katika eneo la usafiri na usafirishaji, Mheshimiwa Rais ameibuka mshindi wa tuzo ya uwekezaji kwenye miundombinu ya usafirishaji na usafiri kwa mwaka 2020, tuzo iliyotolewa na taasisi ya Media for Infrastructure and Finance in Africa (MIFA). Maelezo yaliyotolewa na wadhamini wa tuzo hiyo ambao ni Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) yameonesha kutambua mchango mkubwa wa Rais wetu katika ujenzi wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uwekezaji mkubwa kwenye barabara za mzunguko kwenye Makao Makuu ya nchi Jijini Dodoma, ununuzi wa mabehewa mapya ya treni 1,430 pamoja na usimamizi mzuri wa Serikali unaoongozwa na uwazi wa hali ya juu imekuwa chachu ya mafanikio hayo.

Mheshimiwa Spika, hatua hizo zinazochukuliwa na Mheshimiwa Rais ni muhimu katika kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ujenzi wa uchumi unaoongozwa na viwanda. Ikumbukwe kwamba miongoni mwa mahitaji muhimu katika ujenzi wa viwanda na uwekezaji ni uwepo wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji, upatikanaji wa maji ya kutosha, huduma nzuri za afya na wafanyakazi wenye ujuzi.

Mheshimiwa Spika, diplomasia ya uchumi. Utekelezaji wa diplomasia ya uchumi umepiga hatua kubwa katika kipindi cha mwaka mmoja cha Mheshimiwa Rais wetu mpendwa. Mheshimiwa Rais ametumia vema ziara zake za kikazi nje ya nchi kuhamasisha uwekezaji, kujenga mahusiano mazuri ya kibiashara sambamba na kujenga taswira ya nje ya nchi kwa nchi yetu. Ripoti ya uwekezaji iliyotoka mwezi Juni mwaka 2021, inaonesha kuwa licha ya janga la UVIKO- 19, Tanzania katika mwaka 2020 ilipokea uwekezaji kutoka nje wa takribani Dola za Marekani Bilioni Moja.

Mheshimiwa Spika, aidha, takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa katika kipindi cha Machi, 2021 hadi Februari, 2022, Serikali imeweza kuvutia na kusajili jumla ya miradi ya uwekezaji 294. Miradi hiyo inatarajiwa kuwekeza mtaji wa thamani ya dola za Marekani Bilioni 8.13 na kutoa ajira kwa watu wasiopungua 62,000.

Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine Mheshimiwa Rais amefanikiwa kuimarisha mahusiano yetu na nchi jirani.

Kwa mfano, kufuatia ziara yake ya Kitaifa Jamhuri ya Kenya, jumla ya vikwazo 30 visivyo vya kibiashara vilijadiliwa. Kati ya hivyo vikwazo 10 vilipatiwa ufumbuzi na kuondolewa, vikwazo vitano vilifutwa kwa sababu ya kukosa taarifa za kutosha kuweza kujadiliwa na vikwazo 15 vimewekewa ukomo wa kuvitatua ifikapo tarehe 30 Juni mwaka huu 2022.

Mheshimiwa Spika, kupatiwa ufumbuzi kwa vikwazo hivyo kumeimarisha shughuli za kiuchumi za kijasiriamali kwenye maeneo ya mipakani, kuinua vipato kwa wananchi wetu na kuimarisha mtangamano kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo tarehe 29 mwezi wa Tatu mwaka huu 2022 ilipokea mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa hiyo Congo sasa ni nchi ambayo pia ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwahakikishi na kuwahamasisha Watanzania kuchangamkia fursa zilizotokana na kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara pamoja na ujio wa mwanachama mpya huyu wa Congo unaozidi kuimarisha soko la Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki kibiashara na kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, suala la ushirika. Ushirika umeendelea kuwa sehemu ya kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha unakuwa na tija kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na Taifa kwa ujumla. Hatua zinazochukuliwa katika kuimarisha utendaji wa vyama vya ushirika zimeanza kuonesha mafanikio makubwa kama ifuatavyo: -

Moja; vyama vya ushirika kuanzisha na kufufua viwanda vidogo na vikubwa 452. Viwanda hivyo ni pamoja na viwanda vya kahawa, alizeti na pamba ikiwemo viwanda vya kuchambua pamba vilivyopo Kahama na Chato.

Mbili; kusimamia urejeshaji wa mali za vyama vya ushirika zikiwemo mashamba, viwanja, majengo, maghala na viwanda, pia nyinginezo zenye thamani ya takriban Shilingi Bilioni 68.

Tatu; kujenga imani ya wakulima katika ushirika ikilinganishwa na hapo awali. Kutokana na imani iliyojengeka, idadi ya vyama vya ushirika vyenye usajili vimeongezeka na kufikia 9,741 kufikia mwaka 2022 ikilinganishwa na vyama 9,185 mwaka 2020, sawa na ongezeko la vyama 556. Kadhalika, kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanachama 914,948 wa VVyama vya ushirika kutoka mwaka 2021 hadi mwaka 2022.

Nne; kuimarika kwa uuzaji wa mazao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani. Hatua hii imewezesha kuimarika kwa bei ya baadhi ya mazao. Mathalan, hivi karibuni tumeona bei ya cocoa inayolimwa kule Mkoani Mbeya, Wilaya ya Kyela ikiongezeka mara dufu kutoka Shilingi 2,500 hadi Shilingi 5,000 kwa kilo baada ya kutumia mfumo wa ushirika na stakabadhi ghalani.

Mheshimiwa Spika, aidha, kupitia uhamasishaji wa masoko na uwekezaji katika vyama vya ushirika, mazao ya aina 10 yenye uzani wa tani 575,296 zenye thamani ya Shilingi Trilioni 1.52 yaliuzwa kupitia ushirika kwa kipindi cha Julai 2021 hadi 2022.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kusimamia ushirika, bado kuna changamoto ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi ili ushirika uendelee kuimarika. Changamoto hizo ni pamoja na usimamizi usioridhisha wa mali za ushirika, wizi na ubadhirifu unaofanywa na baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika, kukosekana kwa elimu ya ushirika kwa wadau muhimu, upatikanaji wa masoko na utitiri wa tozo unaofanya bei anayolipwa mkulima kuwa ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto ya bei ndogo ya mazao, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutafuta masoko ndani na nje ya nchi, kuimarisha viwanda vya ndani vya kuchakata mazao pamoja na kuondoa tozo zisizo za msingi zinazosababisha bei anayolipwa mkulima kuwa ndogo.

Mheshimiwa Spika, mara zote Mheshimiwa Rais amesisitiza kufanya mapitio ya tozo kwa kuzirekebisha au kuzifuta ili kuleta unafuu kwa mkulima. Kwa kuzingatia maelezo hayo ya Mheshimiwa Rais, Tarehe 29 Machi mwaka huu 2022 nikiwa Mjini Karagwe, nilikutana na viongozi na wadau wa ushirika kwa ajili ya kutoa maelekezo na mwelekeo wa usimamizi na uendeshaji wa zao la kahawa Wilayani Karagwe, Wilaya ya Kyerwa na wilaya za jirani kama vile Bukoba Vijijini na pia Muleba na Ngara.

Mheshimiwa Spika, kupitia kikao hicho, nilitangaza uamuzi wa Serikali wa kufuta tozo 42 kati ya 47 zilizokuwa zinatozwa na vyama vya ushirika kwa zao la kahawa. Awali, mkulima alilazimika kulipa Shilingi 805 kwa kila kilo ya kahawa aliyoiuza kutokana na uwepo wa tozo hizo 47. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninatoa maelekezo kwa Wizara ya Kilimo kukutana na wadau wote muhimu ili kuhakikisha mpangokazi wa zao la kahawa kwa ajili ya msimu ujao wa ununuzi unaanza mara moja. Serikali kwa upande wake itaendelea kuchukua hatua za makusudi kunusuru hali ya wakulima nchini ili kuhakikisha kuwa kilimo kinakuwa chachu katika kutengeneza ajira, upatikanaji wa malighafi za viwanda na kuwapatia tija kwa wakulima wenyewe. Vilevile, Serikali inafanya mapitio ya tozo zilizopo katika mazao mbalimbali ili kuufanya ushirika uwe na tija na mkulima aweze kunufaika zaidi.

Mheshimiwa Spika, suala la amani, umoja na mshikamano wa Kitaifa. Itakumbukwa kuwa Tarehe 7 Aprili, 2022, ilikuwa ni kumbukizi ya kifo cha Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza na muasisi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Tukio hilo lilifuatiwa na mdahalo wa kumbikizi ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa muasisi mwingine wa Taifa hili Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mheshimiwa Spika, uhuru tunaoushuhudia leo, amani na umoja tunaoushuhudia leo, mshikamano wa Kitaifa tunaoushuhudia leo na kustahimiliana kuliko tufikisha hapa tulipo leo, ni miongoni mwa misingi ya uongozi uliotukuka na wenye kujali utu tulioachiwa na waasisi wetu ambao Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania ameyaamua kuuishi.

Mheshimiwa Spika, 19 Machi, 2021 baada ya kuapa kuliongoza Taifa hili, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitamka maneno yafuatayo, naomba kunukuu “… Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama Taifa, ni wakati wa kufarijiana, kuoneshana upendo, undugu wetu, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu na Utanzania wetu. Huu si wakati wa kutazama mbele kwa mashaka, bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini…” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tangu atamke maneno hayo, Mheshimiwa Rais ameendelea kuyaishi kwa vitendo huku akiwa kinara wa kuhubiri amani na mshikamano hapa nchini, nia yake ya dhati ya kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa Kitaifa inajionesha wazi katika kuundwa kwa kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia, kufuatia maoni yaliyotolewa katika mkutano wa wadau wa demokrasia nchini uliofanyika tarehe 15 na 16 Disemba, 2021 hapa Jijini Dodoma.

Mheshimiwa Spika, katika kuonesha nia yake ya kuleta maridhiano na amani, Mheshimiwa Rais aliwataka wajumbe wa kikosi kazi hicho kwenda kutafakari zaidi na hatimae kuwasilisha taarifa itakayoainisha njia bora za kutatua changamoto ambazo nyingine ametaka zitafutiwe ufumbuzi wa haraka hata kabla ya kufanyika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.

Mheshimiwa Spika, vilevile Mheshimiwa Rais alitaka kikosi kazi hicho kuchambua masuala yote ambayo hayaleti siasa za tija, kukwaza demokrasia na kufanya siasa kuwa chuki. Aidha, katika kudumisha amani na maridhiano ya dhati, Mheshimiwa Rais alitoa rai kwa vyombo vya habari kuwa na mahusiano chanya kati ya Serikali na vyama vya siasa bila kuwa na upendeleo.

Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza dhamira yake ya ushirikishwaji na usawa, Mheshimiwa Rais alitoa wito kwa vyama vya siasa kuzingatia usawa wa kijinsia, kwa kutoa nafasi kwa wanawake ili waweze kushiriki katika siasa ndani ya vyama vyao. Aidha, aliwataka wanawake kutambua wajibu wao katika vyama vyao na jamii kwa ujumla na kuhakikisha wanaelewa ipasavyo ajenda zinazowawezesha na kuwasemea wanawake wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa katika kuhakikisha tunakuwa wamoja, sambamba na kuimarisha demokrasia nchini huku akitambua kuwa umoja wetu ndiyo uhai wetu. Kwa msingi huo, jitihada tunazozifanya za kujenga uchumi imara, shindani na endelevu zimebebwa na misingi ya amani, maelewano na mshikamano.

Mheshimiwa Spika, nami nitoe wito kwa Watanzania wenzangu kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais kusisitiza kuhusu umuhimu wa kudumisha amani na kwamba, kwa hakika nchi yetu itajengwa na watu wenye itikadi zote za siasa. Aidha, nitoe rai kwa vyama vyote vya siasa kuendeleza siasa za maridhiano na amani sambamba na kutumia vema haki ya demokrasia kwa maslahi mapana ya Watanzania. Katika kila sera na mipango ndani ya vyama vyetu, hatunabudi kuwatanguliza Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha kumbukizi ya kifo cha Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kumbukizi ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tunapaswa kujiuliza tunairithisha nini, tunairithisha vipi misingi muhimu hususan uongozi iliyojengwa na waasisi hao kwa vizazi vya sasa na vinavyofuata? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa lugha nyingine, tunayo kila sababu ya kufanya tafakari kuhusu namna bora ya kuhakikisha urithi wa maisha ya waasisi wetu ambao walikuwa tayari kuacha kila kitu kwa ajili ya Taifa hili umeenziwa, unatambulika, unahifadhiwa, unasherehekewa na unajulikana kwa Watanzania wengi hususan vijana wa leo. Urithi huo ni tunu na nguzo kubwa ya Taifa letu hususan katika masuala yanayohusu maadili ya uongozi, kuimarisha muungano, kuondoa tofauti za kidini, kikabila pamoja na kuchagiza mapambano dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini.

Mheshimiwa Spika, sensa ya Watu na Makazi. Tarehe 08 Aprili, 2022, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizindua rasmi Tarehe na Nembo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Tukio hilo ni sehemu ya hatua muhimu kuelekea kukamilisha Sensa ya Watu na Makazi siku ya tarehe 23 Agosti 2022.

Mheshimiwa Spika, binafsi ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo amelibeba suala la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Mheshimiwa Rais amekuwa akishiriki kwa karibu katika hatua zote muhimu zenye lengo la kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. Kwa mfano, tarehe 14 Septemba, 2021 katika viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma, Mheshimiwa Rais alizindua Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ikiwa ni mwongozo wa kuhamasisha wananchi wote kushiriki zoezi la kuhesabiwa ifikapo Agosti, 2022. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile, tarehe 08 Februari, 2022, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Jakaya Kikwete (JKCC) uliopo Jijini Dodoma. Zoezi la utambuzi na kujenga mfumo wa anwani za makazi na postikodi nchi nzima ni sehemu muhimu kuelekea kwenye Sensa ya Watu na Makazi vilevile.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa mradi huo unaotarajiwa kutumia shilingi bilioni 28, utachangia masuala yafuatayo: -

Moja, kuifungua Tanzania kuelekea kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda (uchumi wa kidijitali) sambamba na kuimarisha biashara ya Kimataifa.

Mbili; kuimarisha Tanzania kuwa nchi ya kwanza kwa ukanda wa Afrika Mashariki kufikika kwa haraka, uhakika na wepesi zaidi na hivyo, kufungua milango ya biashara Kimataifa na shughuli nyinginezo za kiuchumi.

Tatu; Kusaidia utambuzi wa maeneo ya uwekezaji wa viwanda, ufugaji na kilimo na hivyo kuondoa migogoro ya matumizi ya ardhi hususan baada ya kukamilika kwa uandaaji wa ramani za kidijitali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, Kuimarisha huduma za ulinzi wa usalama sambamba na kurahisisha shughuli nyingine za kijamii kwa kuwa mfumo huo unatambulisha mahali halisi ambapo mtu anaishi, mahali ilipo, biashara yake au ofisi anayofanyia kazi kwa kufuata jina la barabara na mitaa, namba ya nyumba au jengo pamoja na Postikodi.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwakumbusha viongozi na watendaji wote hususan Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kusimamia ipasavyo maelekezo ya Mheshimiwa Rais, kwamba kazi ya kuweka mfumo wa anwani za makazi na postikodi itekelezwe kwa haraka na kuhakikisha inakamilika ifikapo mwezi 30 Mei, 2022.

Mheshimiwa Spika, ninalishukuru Bunge lako Tukufu kwa kuidhinisha kiasi cha Shilingi Bilioni 215.6 katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya Sensa ya Watu na Makazi. Aidha, nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuhamasisha wananchi wote katika Majimbo yetu ili washiriki ipasavyo katika zoezi la kuhesabiwa kwa kutoa taarifa sahihi za kijamii, kiuchumi na mazingira wanayoishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwaomba viongozi wetu wa dini na kimila ambao wamekuwa bega kwa bega na Serikali tangu kuanza kwa zoezi hili, waendelee kutusaidia kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ili kuwawezesha makundi yote ya jamii kushiriki zoezi hilo. Aidha, nitoe wito kwa viongozi na watendaji wa umma na sekta binafsi kutumia Nembo ya Sensa kwenye shughuli zote za umma na shughuli binafsi pia hadi pale zoezi la sensa ya watu na Makazi litakapokamilika mwezi Agosti, 2022.

Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana na mimi kwamba idadi yetu ndiyo mtaji wetu. Hivyo, kufanikiwa kwa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 ambalo hivi sasa limefikia asilimia 79 kutaiweka nchi yetu kwenye ramani nzuri kimataifa na kuiwezesha kuungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa kwenye nyanja za kiuchumi na maendeleo.

Mheshimiwa Spika, ndugu zangu Watanzania, ninawasihi tukahesabiwe na tutoe ushirikiano wa kutosha kwa Makarani na Wasimamizi wa sensa siku ya Tarehe 23 Agosti, 2022 watakapotutembelea katika kaya zetu. Zoezi hili ni muhimu kwani linakuwa ndiyo msingi wa taarifa ambazo zitatumika kwenye mipango na mikakati mbalimbali ya maendeleo kwa kipindi cha miaka 10 ijayo.

Mheshimiwa Spika, majibu ya hoja ambazo zimeletwa mbele yetu. Kwa mujibu wa Kanuni ya 118 (13) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Juni, 2020, naomba nitumie nafasi hii kujibu na kufafanua baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge zilizoibuliwa wakati wa mjadala huu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hoja ya kwanza ilikuwa ni Serikali iweke utaratibu mzuri wa kutembelea miradi ya maendeleo ili kuepuka kutembelea miradi mingi kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Spika, usimamizi wa miradi ya maendeleo umeendelea kuwa kipaumbele cha Serikali, katika kuhakikisha miradi inayotekelezwa inaakisi thamani ya fedha za umma. Sambamba na hilo, Serikali itaendelea kutumia ziara za viongozi kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa miradi na kuchukua hatua stahiki dhidi ya ubadhirifu wa aina yoyote utakaojitokeza. Kwa upande mwingine, Serikali itaandaa utaratibu mzuri ikiwemo kutenga muda wa kutosha wakati wa ziara za viongozi ili kuhakikisha kwamba miradi na shughuli muhimu za kijamii zinafikiwa.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali imeandaa Mwongozo wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi na programu za maendeleo unaoainisha majukumu na wajibu wa kila mdau katika usimamizi wa miradi. Pamoja na mambo mengine, mwongozo huo unazielekeza taasisi zote za umma kuandaa mpango wa mwaka wa ufuatiliaji na tathmini wa miradi (Monitoring and Evaluation Plan).

Mheshimiwa Spika, tayari mwongozo huo umeshasambazwa katika Wizara, Halmashauri na Taasisi zote za Serikali na utaanza kutumika katika mwaka wa fedha 2022/ 2023. Nitumie fursa hii kusisitiza taasisi zote za umma kuhakikisha zinaandaa mipango ya ufuatiliaji na tathmini ya mwaka ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mwongozo huo.

Mheshimiwa Spika, ili mwongozo huo ulete matokeo tarajiwa, ninaelekeza viongozi na watendaji walio katika Mikoa, Wilaya na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha kwamba, wanatembelea mara kwa mara na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi katika maeneo yao. Aidha, wawatembelee wananchi katika maeneo yao, kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi badala ya kusubiri ziara za viongozi wa Kitaifa. Serikali ihakikishe wananchi wanashirikishwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ilikuwa ni Serikali ihakikishe wananchi wanashirikishwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, hapa jibu ni kwamba Mwongozo wa Taifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya miradi umeainisha umuhimu wa kushirikisha wananchi katika hatua zote za utekelezaji wa miradi. Lengo la Serikali kupitia mwongozo huo ni kuongeza uelewa, umiliki, uwajibikaji na thamani ya miradi inayotekelezwa kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukua hatua zote hizo ili kuhakikisha kwamba wananchi wanaibua changamoto halisia za maendeleo katika maeneo yao, kwa kufanya hivyo, wanaingia moja kwa moja katika mnyororo mzima wa utekelezaji wa miradi inayotoa fursa za maendeleo, kuimarisha huduma za jamii, ajira na kujiongezea kipato.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, Serikali itaendelea kuzingatia ushiriki wa jamii ikiwa ni kigezo muhimu katika kuidhinisha miradi na hivyo kuibua uhalisia wa malengo ya utekelezaji wa miradi hiyo katika kutatua kero na changamoto za wananchi.

Mheshimiwa Spika, kampuni za ndani zitambuliwe, ziwezeshwe na kupewa fursa za kushindana na Makampuni ya nje katika zabuni zitakazotangazwa kupitia Miradi ya Ujenzi wa Bomba la Mafuta la Hoima (Uganda) – Tanga (Tanzania), hatua hii itasaidia kuongeza ajira kwa wazawa. Hii ilikuwa ni hoja nyingine ya kwamba kampuni za ndani zitambuliwe, ziwezeshwe na kupewa fursa za kushindana na makampuni ya nje katika zabuni zitakazotangazwa kupitia mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la Hoima (Uganda) – Tanga (Tanzania). Hatua hii itasaidia kuongeza ajira hususani kwa wazawa.

Mheshimiwa Spika, maelezo ya Serikali ni kwamba, Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba wazawa kupitia kampuni zao wanapata fursa ya kushiriki katika miradi ya kimkakati na uwekezaji. Aidha, katika kuhakikisha tunawafikia kwa urahisi, tarehe 04 Oktoba, 2021 Serikali ilizindua kanzidata ya watoa huduma, wawekezaji na wasambazaji bidhaa wazawa. Kanzidata hizo, zinawawezesha watoa huduma na wasambazaji bidhaa wazawa, kupata taarifa ya zabuni zinazotangazwa na wawekezaji mbalimbali ndani na nje ya nchi. Hatua hizo zinawezesha watoa huduma na wasambazaji bidhaa ambao ni wazawa kutambua na kuunganishwa na fursa zinazotolewa na wawekezaji wakubwa.

Mheshimiwa Spika, katika kukuza Ushirika wa Watanzania kwenye mradi wa East African Crude Oil Pipeline (EACOP), Serikali imekutana na kampuni za wazawa na wajasiriamali kwa nyakati tofauti, katika Mikoa nane ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lengo la kukutana na wadau hao katika Mikoa ambayo bomba la mafuta linapita ni kuwafahamisha tu kwamba fursa zilizopo katika ujenzi wa bomba hilo ni za kwao ili waweze kuzitumia kikamilifu. Mikutano hiyo, pia ilishirikisha Taasisi za fedha ambazo zilipata nafasi ya kueleza fursa za mitaji zitolewazo na taasisi zao.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia kongamano la EACOP lililofanyika tarehe 23 Septemba, 2021 imeendelea kuwajengea uwezo watoa huduma na wasambazaji bidhaa wazawa. Kongamano hilo lililenga kuongeza uelewa wa kampuni za wazawa kwa wajasiriamali juu ya hali ya mradi wa EACOP, pamoja na fursa zinazopatikana katika awamu ya ujenzi wa kwanza wa bomba hilo, ikiwemo fursa ya ajira na zabuni za manunuzi.

Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa wito kwa kampuni, watoa huduma na wasambazaji bidhaa wazawa kujisajili, katika kanzidata ya watoa huduma na wasambazaji bidhaa wazawa katika sekta ya mafuta na gesi ili kupata fursa zitakazotokana na mradi wa EACOP.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa ni Serikali iangalie ni jinsi gani inaweza kushusha bei za mafuta, ikiwezekana kwa kutoa ruzuku, kutenga bajeti maalum ya kufidia bei ya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na swali hili ambalo limechukua maeneo mengi juu ya upandaji wa bidhaa mbalimbali, kati ya mwaka 2019/2020 hadi mwaka 2021/2022 bei za bidhaa nyingi zimekuwa zikipanda kutokana na matukio mbalimbali yanayoikumba nchi yetu na dunia kwa ujumla. Baadhi ya matukio makubwa yaliyoikumba dunia katika kipindi hicho ni pamoja na janga la UVIKO-19, mabadiliko ya hali ya hewa kama vile ukame, uzalishaji mdogo wa bidhaa kwenye viwanda vyetu na maeneo mbalimbali na mashambani na ukosefu wa malighafi. Lakini pia, uwepo wa tukio ambalo linaendelea kwa sasa nchini Ukraine na Urusi la vita.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mwingiliano wa kibiashara, kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania na Mataifa mengine, matukio hayo vilevile yamekuwa na athari za moja kwa moja na wakati mwingine zisizokuwa za moja kwa moja katika uchumi wa maisha ya watu wetu.

Mheshimiwa Spika, janga la UVIKO-19 lilisababisha shughuli nyingi za kiuchumi kusimama duniani. Hali hiyo ilipelekea baadhi ya bidhaa muhimu ikiwemo mbolea, sukari na mafuta ya kula kupanda bei.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa nchi yetu, hatua madhubuti zilichukuliwa na Serikali ikiwemo kuruhusu wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji kiuchumi kuliufanya pia uchumi wa nchi yetu kuendelea kuwa na shughuli za uzalishaji zikituhakikishia usalama wa chakula ikilinganishwa na maeneo mengine ambako hawakuchukua hatua kama ambazo sisi tulichukua.

Mheshimiwa Spika, wakati nchi ikiendelea kuponya majeraha ya kiuchumi yaliyosababishwa na UVIKO-19, mwezi Februari 2022 kulizuka mgogoro mwingine duniani ulioingiza nchi ya Urusi kwenye vita dhidi ya Ukraine. Kama ambavyo mnafahamu, Urusi ni mzalishaji mkubwa wa bidhaa za mafuta akiwa ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa watatu duniani. Kadhalika, nchi ya Urusi na Ukraine ni wazalishaji wakubwa wa bidhaa za ngano duniani. Kwa upande wa Tanzania, takriban asilimia 57 ya ngano inayotumika hapa kwetu nchini imekuwa ikitoka kwenye ukanda wa Ukraine na Urusi.

Mheshimiwa Spika, kufuatia vita hiyo, nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani ziliamua kuiwekea vikwazo Urusi ikiwa ni pamoja na kutafuta vyanzo mbadala vya mafuta na gesi ili kuachana na ununuzi wa bidhaa hizo kutoka Urusi.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba vikwazo dhidi ya Urusi vimechangia kupungua kwa kiwango cha uzalishaji wa mafuta duniani, bidhaa za ngano vilevile zimepungua pamoja na mbolea na hivyo kusababisha ongezeko la bei ya bidhaa hizo.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kueleza, Tanzania ikiwa ni sehemu ya dunia nasi tumekuwa sehemu ya waathirika kiuchumi kufuatia kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa za mafuta na ngano kutoka kwenye nchi hizo za Urusi na Ukraine. Kwa mfano, tumeshuhudia kupanda kwa bei ya mafuta japo bado nchi yetu ina unafuu mkubwa ikilinganishwa na baadhi ya maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, Tanzania kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine duniani, Serikali yetu naendelea kuwahakikishia Watanzania kwamba bidhaa hizo zinazopatikana katika masoko yote nchini, sambamba na kuchukua hatua madhubuti zenye kuleta unafuu kwa wananchi zitaendelea kuangaliwa kwa ukaribu na ufuatiliaji wake kwa ukaribu zaidi.

Mheshimiwa Spika, tarehe 11 Aprili, 2022 Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, Mbunge, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, pamoja na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango, walifanya mkutano na wadau mbalimbali wazalishaji. Kupitia mkutano huo, Waheshimiwa Mawaziri walieleza hali halisi kuhusu mwenendo wa bei na hatua ambazo Serikali inachukua katika kukabiliana na hali hiyo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na maelezo yaliyotolewa na Waheshimiwa Mawaziri, ambao pia waliungwa mkono na wazalishaji, napenda kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kufanya yafuatayo: -

Moja; kuhakikisha kwamba, bei ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi zinakuwa himilivu na kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi Serikali kupitia Kamati za bei za Mikoa na Wilaya itaendelea kufanya tathmini ya kuona namna ya kuleta unafuu katika masoko kila Mkoa na kila Makao Makuu ya Wilaya kupitia Kamati hizo za bei. Kamati hizi zinazoongozwa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ndizo zenye wajibu wa kupita kwenye masoko yetu kuona bidhaa zilizopo, zile zinazozalishwa ndani ambazo hazina sababu ya kupandishwa bei zitakuwa zinadhibitiwa na kamati ya bei ya ngazi ya Wilaya na Mkoa.

Mbili; kuendelea kushirikiana na sekta binafsi hususan wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa hizi, ili kupanga viwango vipya vya kodi vitakavyoleta unafuu kwa mlaji, kama vile kupunguza kodi ya baadhi ya bidhaa, pia kuhakikisha kwamba bidhaa hizo nazo zinapatikana kwenye maeneo hayo.

Tatu; kupunguza gharama za vifaa vya usafiri na usafirishaji ambazo zimekuwa na athari ya moja kwa moja kwenye kupanda bei ya bidhaa. Kupungua kwa gharama hizo kunategemewa kushusha gharama na bei ya bidhaa nyingine ndani ya masoko yetu.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba, inaimarisha uzalishaji wa bidhaa za viwandani, hasa bidhaa za chakula zinazoingizwa kwa wingi kutoka nje ikiwemo ngano, mafuta ya kula na sukari kwa kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji hapa ndani, kwa kutoa vivutio stahiki kwa wawekezaji wetu. Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwa uwekezaji wa ndani kwenye uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali ili kukabiliana na aina hii ya mtikisiko wa kiuchumi. Pia, Serikali itaendelea kufanya mapitio ya kisera za kibiashara ili kuona maeneo yanayoweza kuleta unafuu kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, ninaielekeza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa bei za bidhaa mbalimbali kwenye soko na kuchukua hatua stahiki kwa wakati, sambamba na kusimamia vema mfumo wa kupokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu mwenendo usioridhisha wa bei za bidhaa sokoni. Kamati za bei na biashara za Mikoa na Wilaya zihakikishe zinafuatilia kwenye masoko na kujiridhisha na uhalisia wa kupanda kwa bei za bidhaa kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, vilevile, ninazielekeza Mamlaka na Serikali za Mitaa, Taasisi za Serikali zilizopewa dhamana ya kusimamia mienendo ya masoko ya bidhaa kutekeleza wajibu wao kikamilifu na kwa umakini mkubwa sambamba na kudhibiti vitendo vya upandishaji bei holela wa bidhaa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii pia, kukemea vitendo vya baadhi ya wazalishaji na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kupanga bei, kufanya mgomo, kukubaliana katika manunuzi na kuuza kwa bei ya juu, mbinu ambazo wakati mwingine zimekuwa chanzo cha kupanda kwa bei za bidhaa. Wale wote watakaobainika kufanya michezo hiyo, hatutosita kuwachukulia hatua za kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa Watanzania kwanza kuendelea kuwa wamoja na tuendelee kufanya kazi kwa bidii ili kuufanya uchumi wa nchi yetu kuwa shindani na wa viwanda kwa maendeleo ya watu. Serikali kwa upande wake itaendelea kuhakikisha kuwa hakuna uhaba wa bidhaa nchini wakati ikiliangalia vizuri suala la bei na kuona namna ya kutoa unafuu kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuwahakikishia Watanzania kuwa Serikali imejipanga vizuri kupitia Kamati za Bei, kama nilivyoeleza awali na kutoa agizo kwa wakuu wa mikoa kuziimarisha kamati hizo na kuzifanya kamati hizo ziwe zinafanya kazi mpaka kwenye ngazi ya Wilaya zikiongozwa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya na kupita kwenye masoko kukagua bidhaa zote na kuona gharama zake kama ni halisia au la, lakini pia kukaa na wafanyabiashara wa maeneo haya ya biashara kufanya mapitio ya gharama za bidhaa hizo ili kuona uhalisia wa bei na hatimae tuhakikishe kwamba, wananchi wanaopata huduma kwenye maeneo hayo wanapata unafuu mkubwa.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ya tano; wanasema fedha nyingi zinatumika kwa ajili ya shughuli za mbio za mwenge wa uhuru. Je, Serikali haiwezi kuja na mbinu mbadala ya kuenzi mwenge wa uhuru badala ya kuukimbiza kila mwaka?

Mheshimiwa Spika, jibu la swali hili ni kwamba, tangu kuasisiwa kwa Taifa letu, uhuru na umoja umeendelea kuwa nguzo ya amani na mshikamano wetu. Ukweli huo unajidhihirisha katika itikadi na falsafa za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, zilizojikita katika kuhakikisha kunakuwepo na usawa na utu wa ubinadamu kwa binadamu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, falsafa hizo zimeendelea kuitambulisha Tanzania katika medani za Kimataifa kuwa ni nchi yenye kupinga ukandamizaji, unyonyaji, unyanyasaji na mifumo ya kitabaka yenye kudhalilisha utu wa binadamu. Hali hiyo inajionesha waziwazi katika kauli aliyoitoa Baba wa Taifa kabla nchi yetu haijapata uhuru, mwaka 1958 aliposema, naomba kunukuu, “Sisi Watu wa Tanganyika tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tangu kipindi cha uhuru, Mwenge umeendelea kuwa miongoni mwa alama tano za nchi hii, ikiwa ni pamoja na Bendera, Twiga, Wimbo wa Taifa na Ngao ya Taifa pamoja na Mwenge wenyewe. Hivyo, tumeendelea kuutumia Mwenge wa Uhuru kuhamasisha ujenzi wa Taifa lenye watu wenye amani, upendo, matumaini na kuheshimiana kwa misingi ya utu na usawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa vijana Mbio za Mwenge wa Uhuru zimeendelea kuwa kielelezo cha ukakamavu na uzalendo walionao katika ulinzi na ujenzi wa Taifa hili. Pia, Mwenge wa Uhuru umekuwa sehemu ya kuhamasisha wananchi kubuni na kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo katika nyanja za kilimo, ufugaji, uvuvi, uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya, elimu, maji, umeme na huduma za jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2010- 2021, jumla ya miradi 15,212 yenye thamani ya Shilingi Trilioni 9.19 iliyotokana na michango ya wananchi, Serikali Kuu, Halmashauri na wahisani ilikaguliwa na mingine kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi. Mbio za Mwenge wa Uhuru pia zimekuwa zikitumika kuelimisha wananchi kuhusu masuala ya lishe bora, jinsi ya kupambana na rushwa, dawa za kulevya, maradhi yanayotishia ustawi wa jamii ya watu wetu kama vile UKIMWI, Malaria, UVIKO -19 na magonjwa yasiyoambukiza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, kuna umuhimu wa kuendelea na Mbio za Mwenge wa Uhuru kila mwaka kwani lengo lake kuu ni kuwakumbusha Watanzania wote na vizazi vijavyo juu ya jukumu lao la kulinda uhuru, umoja na amani ambavyo vimekuwepo ili viweze kuendelea na kudumu wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapoelekea kuhitimisha maelezo yangu, nirudie tena kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa michango yenu yenye kuonesha ni jinsi gani tupo pamoja katika kuwatumikia Watanzania sambamba na kusimamia mwelekeo wa sera za Chama cha Mapinduzi zenye lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi imara, unaojitegemea na shindani, lakini Wabunge wenzangu naomba basi na ninyi mfikirie namna ya kupitisha bajeti hii, ili tuendelee kufanya kazi kwa pamoja kupitia Majimbo yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie pia fursa hii kuwasihi viongozi na watendaji wote hususan katika sekta za umma, kuiishi ndoto ya Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuona Watanzania wanafikiwa kwenye maeneo yao, na wanapofika kwenye ofisi za umma wanapokelewa, wanasikilizwa na kuhudumiwa kikamilifu. Eneo hili ni muhimu katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma muhimu na maendeleo ya haraka.

Mheshimiwa Spika, niwatake viongozi wenzangu kuendelea kufuatilia kwa karibu na umakini mkubwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yetu ili kuhakikisha inalingana na thamani ya fedha inayowekezwa kwenye maeneo yetu. Kadhalika, niendelee kuwasihi ndugu zangu Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ili kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa ninawasihi Watanzania kutumia vyema kipindi hiki cha toba cha Kwaresma na mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuiombea nchi yetu iendelee kuwa tulivu, yenye amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Kuwaombea viongozi wetu ili waweze kutekeleza wajibu wao na majukumu yao kwa jamii yetu hasa katika kuinua uchumi na mafanikio makubwa. Aidha, nichukue nafasi hii kuwatakia heri ya sikukuu ya Pasaka kwa ndugu zetu wote wakristu na mfungo mwema waislamu n ahata huko mwisho kutakapokuwa na Iddi yote haya tunawatakia kila la heri kwa sherehe hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya, sasa, naomba Bunge lako Tukufu, narudia tena. Naomba Bunge lako Tukufu liridhie na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake ikiwemo na Mfuko wa Bunge kama nilivyowasilisha katika hoja yangu ya tarehe 06 mwezi huu wa Nne, 2022. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naafiki.