Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ummy Hamisi Nderiananga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ninamshukuru kipekee Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na kuweza kukutana katika Bunge hili. Nitumie fursa hii kuwatakia heri ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani Waislam wote katika Taifa letu na dunia nzima na niwatakie heri ya kwaresma Wakristo wote.

Mheshimiwa Spika, vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassani kwa kutimiza mwaka mmoja wa kuchapa kazi kwa weledi na bidi, hongera sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa uniruhusu niende katika hoja za Kamati zetu zote mbili zimeshauri vizuri, na ninawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge kwa michango mizuri ambayo mmetupatia ili kuboresha eneo letu la bajeti Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba fedha za maendeleo zilizotengwa Shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya mwitiko wa masuala ya UKIMWI Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Rais Samia tutazitoa fedha zote hizo ndani ya mwezi huu wa Aprili katika robo ya nne hii. Kwa hiyo niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kazi inaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la fedha za ndani kwa ajili ya mapambano dhidi ya virus vya UKIMWI, niwaambie tu kwamba Serikali imeongeza fedha kutoka kiasi cha Shilingi Bilioni Moja mwaka 2021/2022 na katika bajeti hii ya leo ambayo mtatupitishia Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Rais Samia tumeongeza fedha kwa asilimia 88 na sasa zitakuwa ni Shilingi Bilioni Moja Milioni Mia Nane na Themanini katika mapambano dhidi ya virus vya UKIMWI na kazi inaendelea.

Mheshimiwa Spika, lipo suala liliongelewa kuhusu mfuko wa mapambano dhidi ya virus vya UKIMWI, tumepokea maoni na ushauri wa Kamati yetu ya masuala ya UKIMWI na kwa uharaka sana mwezi wa pili mwaka huu tumesaini mkataba na taasisi ya sekta binafsi ili kuona namna ambavyo tunaweza tukatafuta fund ndani yetu tuka-mobilize resource. Kwa hiyo, niwaambie Watanzania kwamba kazi hiyo inaendelea na niwashukuru sana taasisi ya sekta binafsi Tanzania kwa kutukubalia ombi letu la kuingia nao makubaliano hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni chanzo cha mapato ya mfuko wa ATF, tumefanya marekebisho ya sheria katika kifungu cha 16 cha Sheria ya Kodi ya Mapato Sura Na. 332 ya mwaka 2020 ambayo hii inaleta nafuu kwa watu watakaochangia mfuko wa ATF.

Mheshimiwa Spika, kwa hili niwakaribishe sana Ofisi ya Waziri Mkuu, muungane na Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia kuchangia kwa sababu unapochangia unapata nafuu ya kodi. Niwapongeze pia kampuni kama ya Barrick ambayo wameweza kutupatia fedha kwa kupitia kipengele hiki na wao wamepata nafuu ya kodi kwa hiyo niyakaribishe makampuni mengine yote kuja kuiunga mkono Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho ni suala la udhibiti wa dawa za kulevya. Serikali ya CCM chini ya Mheshimiwa Rais Samia tunaendelea na mapambano dhidi ya madawa ya kulevya. Mamlaka za kudhibiti dawa za kulevya iko imara sana na kazi inaendelea.

Mheshimiwa Spika, kuanzia Julai, 2021 hadi Februari, 2022 tumefanya operation mbalimbali kupitia mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya na tumekamata watuhumiwa takribani 11, 716 wa dawa za kulevya za kilogram 35,226 wa dawa ya kulevya.

Mheshimiwa Spika, vilevile tumeteketeza ekari 185 za mashamba ya bangi na ekari 10 za mashamba ya mirungi kuanzia kipindi hiko niwahakikishie Watanzania kwamba kazi ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya inaendelea na Serikali iko imara.

Mheshimiwa Spika, lipo jambo Waheshimiwa Wabunge walitushauri kwamba tufundishe elimu hii ya athari za dawa za kulevya, niwaambie tumeingia makubaliano ya Wizara ya Elimu na taasisi zingine tayari tumeshaanda mwongozo wa namna ya kufundisha.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo niwashukuru sana, naomba kuunga mkono hoja ahsante. (Makofi)