Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema, pia nishukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniteua na kuniamini na kunipa dhamana ya kuweza kuwatumikia Watanzania, ninamuahidi yeye pamoja na viongozi wengine Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba nitatekeleza majukumu yangu kwa uaminifu, uadilifu lakini katika kusaidia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nikupongeze na kukushukuru pia wewe kwa kuendesha Bunge lako vizuri pamoja na uongozi wote wa Bunge aidha niwapongeze pia Watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu ambao wametusaidia katika majukumu mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, ninaupongeza muhimili wa Mahakama na viongozi wengine pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kulisimamia Taifa letu kuwa salama.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nijielekeze katika mambo ambayo yamezungumzwa zaidi au yamechangiwa zaidi na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, nikianza na eneo la ajira. Ofisi ya Waziri Mkuu mbali na majukumu mengi yaliyopo inalo jukumu pia la kuweza kuhakikisha kwamba inasimamia na kuratibu Sera pamoja na sheria zote zinazohusika na masuala ya ajira. Katika msingi huo tunamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuwa akituelekeza wakati wote tuweze kuwapokea, kuwasikiliza pia kuwahudumia wale wote ambao wanafika katika ofisi hiyo kwa ajili ya kupata huduma.

Mheshimiwa Spika, katika study ambazo tumejaribu kuzifanya ili kutafuta ulinganifu na suluhu ya changamoto za masuala ya ajira nchini, Ofisi ya Waziri Mkuu na kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Waziri wangu wa nchi Professor Joyce Ndalichako pamoja na watumishi tumejaribu kufanya study na ulinganifu mbalimbali katika kuangalia changamoto za ajira kwa nchi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, tumeweza kufanya utafiti wa kuangalia na kuandaa taarifa ya uchambuzi wa sera, sheria na mikakati ya nchi mbalimbali kuhusu utatuzi wa changamoto za ukosefu wa ajira. Katika maeneo ambayo tumejaribu kuangazia mojawapo ilikuwa ni nchi ya Uganda, Rwanda, Brazil, China Marekani, Tunisia, Uturuki, South Afrika na Kenya.

Mheshimiwa Spika, katika maeneo hayo yote ambayo tumefanyia utafiti wenzetu wamefanana pia maeneo mengi na sisi lakini sisi pia tumeenda hatua ya mbali zaidi. Changamoto kubwa ambazo zinaonekana katika wimbi hili kubwa la ukosefu wa ajira, ambalo sehemu nyingi wanaita kama timing bomb duniani, sababu zinazosababisha ukosefu au changamoto ya ajira nyingine ni chanya na nyingine hasi.

Mheshimiwa Spika, sababu ya kwanza ni ongezeko la taasisi za elimu kwa maana ya uhamasa katika kusoma, kumekuwa na wahitimu wengi katika kada mbalimbali tofauti na uhitaji wa ajira. Sababu ya pili ya kidunia inayoelezwa katika takwimu mbalimbali za International Labour Organization kwa maana ya shirika la kazi duniani, pamoja na taasisi nyingine ni uwepo wa advancement ya teknolojia.

Mheshimiwa Spika, uwepo wa teknolojia umeenda ku-replace human labor, kwa maana ya computer au mashine sasa inaweza ikafanya kazi ya watu zaidi hata ya
100. Sababu nyingine imeelezwa ni masuala ya natural catastrophic na force majeure - acts of God pamoja na masuala kama ya magonjwa kama vile COVID-19 ambayo imesababisha viwanda vingi kufungwa na changamoto nyingine pia makampuni na kadhalika kuweza kufilisika.

Mheshimiwa Spika, sababu nyingine ni masuala ya sasa biashara kiujumla duniani, Serikali zimeacha kufanya shughuli ya biashara na badala yake zinatoa huduma, kwa hiyo biashara imelekezwa katika private sector. Jingine ambalo limeelezwa katika takwimu ni masuala ya viwango vya elimu inayotolewa, mtu apate skill na knowledge competence and performance ya kuweza kufanya kazi. Kwa hiyo, wanapimwa kulingana na ubora na hizo ndio wakati mwingine vimekuwa ni vigezo vya kuweza kusaili watu.

Mheshimiwa Spika, sasa nini kimefanyika kwenye Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu katika eneo hili na katika kutafuta njia mbadala sasa za kukabiliana na changamoto hizo. Kwanza katika kufanya hivyo tulifanya pia utafiti wa kuangalia wingi wa vijana wengi ambao wanaingia katika soko la ajira kila mwaka. Katika tafiti tulizozifanya ukiangalia kwa darasa la saba ukiacha kwa sababu ya muda nisianze mwaka 2012 mpaka mwaka 2021 niende kwenye mwaka 2021 peke yake.

Mheshimiwa Spika, wahitimu wa darasa la saba walikuwa milioni moja na laki moja, kidato cha Nne ni Zaidi ya laki nne na themanini na saba elfu, kidato cha sita ni zaidi ya wahitimu elfu themanini, walioweza kufuzu mafunzo ya VETA ni zaidi ya laki mbili na thelathini na sita na FDC Wahitimu Zaidi ya elfu kumi na moja, lakini pia NACTE ni wahitimu elfu themanini na saba. Kwa ujumla ukienda kwenye vyuo vikuu peke yake kwenye soko wanaingia 47 elfu katika soko la ajira.

Mheshimiwa Spika, sasa nini kwa sababu ukija kuangalia katika ujumla wake tuna watu zaidi ya laki moja wanohitaji ajira katika soko tofauti na hitaji lilivyo.

Mheshimiwa Spika, hatua tulizozichukuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ni:

Moja; kuandaa na kutengeneza uwepo wa vyuo vya VETA kama jinsi China walivyofanya vyuo vikuu zaidi ya laki sita wamevibadilisha na kuwa vyuo vya kati kuweza kutoa mafunzo na skills za kazi.

Pili; tumeendelea kutoa fedha za mikopo za kuweza kuwasaidia katika ngazi za Halmashauri na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili waweze kupata mitaji ya kuweza kufanya shughuli mbalimbali.

Tatu; kumekuwa na mkakati wa kutengeneza mfumo wa ukuzaji wa ujuzi wa vijana ambao wamekuwa wakitoka vyuo vikuu na wale ambao hawajarasilimishiwa ujuzi, tumekuwa tukitoa fedha kwa ajili ya kurasimisha ujuzi na Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa mwaka wa jana alitoa zaidi ya bilioni tisa ilinufaisha vijana zaidi ya 14,440 katika mafunzo.

Mheshimiwa Spika, pia kuna mafunzo ya...

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)