Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Eng. Kundo Andrea Mathew

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa hii nami niweze kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili katika nafasi mbalimbali niweze kutoa ufafanuzi katika maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge wameweza kuyagusa katika Wizara yetu ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Mheshimiwa Spika, nimepitia hoja ya Mheshimiwa Mhata Mbunge wa Nanyumbu kuhusiana na masuala ya ujenzi wa mkongo wa Taifa ambapo matarajio yake ni kwamba mkongo huu unapokamilika basi alitarajia mabadiliko ya bei yatokee katika Jimbo lake la Nanyumbu.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Serikali ilianza kuwekeza katika ujenzi wa mkongo wa Taifa mwaka 2009 ambapo kufikia mwaka 2021 tayari kilometa 8,319 zilikuwa zimejengwa nchi nzima kwenye Mikoa 25 vilevile Wilaya 43.

Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu lilipitisha bajeti mwaka jana ya ujenzi wa mkongo wa Taifa takribani Bilioni 170 ambazo ni uwekezaji ambao unaenda kukamilika katika mwaka huu wa fedha ambapo takribani kilometa 4,442 zitaweza kukamilika, maana yake itakuwa tumefikia asilimia 85 ya lengo la kufikia kilometa 15,000 ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Spika, implication yake nini ni kwamba tunaweza tukaangalia bei ya mawasiliano kuanzia mwaka 2009 na mpaka sasa mwaka 2022 ili kuona nini Mkongo wa Taifa umesaidia. Mwaka 2009 Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote watakumbuka kupiga simu ilikuwa ni Shilingi 147 kutoka mtandao mmoja kwenda mtandao mwingine hiyo ni kwa wastani, lakini kulikuwa na makampuni mengine ambayo ilikuwa zaidi ya hapo. Vile vile kupiga simu kutoka mtandao mmoja wa Vodacom labda kwenda TiGO gharama ilikuwa inaongezeka.

Mheshimiwa Spika, leo hii kutokana na uwekezaji huu wa Serikali kilichofanyika ni mpaka sasa ukipiga simu bila kujiunga na kifurushi chochote kile utaweza kutumia Shilingi 30 peke yake bila kujali unapiga kutoka mtandao wa Vodacom kwenda TiGO, unapiga TiGO kwenda Halotel kwa wastani ni Shilingi 30. Hayo ni mapinduzi makubwa ambayo yametokana na Serikali kuwekeza katika ujenzi wa mkongo wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kwa upande wa Mangaka kwenda Mtambaswala ambapo Serikali imejenga takribani kilometa 72. Lengo kuu la ujenzi wa mkongo ule ni kuhakikisha kwamba tunaenda kutoa huduma katika nchi jirani ya Msumbiji ili tuhakikishe Serikali inajipatia mapato yanayotokana na fedha za kigeni ambapo tukiwa tunatoa huduma ya mkongo wa Taifa, ndiyo maana pale tumeweka POP pale Mtambaswala mpakani.

Mheshimiwa Spika, kuna mambo mengine ambayo yamejitokeza ambayo yamejadiliwa na Waheshimiwa Wabunge, ambayo sana sana ni upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo yao. Hili ni takwa la Ilani ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 61 (J) ambapo inahitaji Serikali kuhakikisha kwamba inafikisha mawasiliano kwa wananchi wote vijijini.

Mheshimiwa Spika, kwa Serikali kwa kuona hilo kupitia Sheria Namba 11 ya Mwaka 2006 ambapo mfuko wa mawasiliano kwa wote ulianzishwa mahsusi ili kuondoa pengo lilokuwepo la mawasiliano kati ya Vijijini na Mijini.

Mheshimiwa Spika, Serikali sasa imeshaanza kuwekeza katika maeneo ambayo yameonekana na changamoto ninapenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali kupitia mradi wa Tanzania kidigitali, ifikapo mwezi wa Tano inaenda kutangaza zabuni ya maeneo 778 ambapo maeneo haya yote yataenda kufikishiwa huduma ya mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maeneo haya ni pamoja na maeneo ambayo Mheshimiwa Shangai Mbunge wa Ngorongoro ambaye alihitaji kutajiwa maeneo ambayo kuna Kata ambazo hazijafikiwa na mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie uwekezaji ndani ya Wilaya ya Ngorongoro na Kata ambazo Mheshimiwa Mbunge anazihitaji tuko Tayari kumpatia ili ajiridhishe maeneo yake yanaenda kufikishiwa huduma ya mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru.