Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, nami nashukuru kwa kupata fursa hii ya kuweza kuchangia hoja ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyoitoa hapa Bungeni wiki iliyopita.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia tumepokea hoja, mapendekezo na ushauri karibu katika maeneo makubwa manane. Tunaomba tu niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa hoja zile na kama Wizara kama Serikali, tumezipokea na tutakwenda kuzifanyia kazi ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, naomba tu nitoe ufafanuzi kwenye baadhi ya maeneo machache ambayo tungependa kutoa ufafanuzi mbele ya Bunge lako Tukufu. Eneo la kwanza ni kwenye mapitio ya mitaala yetu ni sera pamoja na sheria, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba mchakato huu wa kufanya maboresho kwenye mitaala pamoja na sheria yetu unaendelea vizuri, tunataraji mpaka kufika mwaka 2023 mwishoni nadhani tutakuwa tumekamilisha ili kuweza kupata mtaala ambao ninyi Waheshimiwa Wabunge mnadhani ndiyo ambao unaweza kusaidia Taifa letu.

Kwa hiyo mchakato huo unaendelea vizuri na niwaondoe wasiwasi, kwa namna moja au nyingine tutaendelea kushirikiana nanyi kuhakikisha mawazo pamoja na ushauri wenu unaweza kuzingatiwa katika mitaala hii mipya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa niombe kuchukua hoja ya Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei ambae alizungumzia suala la upungufu wa wafanyakazi au wa walimu katika vyuo vyetu vya ufundi. Naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Kimei Waziri wa Utumishi jana ametangaza nafasi mbalimbali za ajira na miongoni mwa nafasi hizo zaidi ya nafasi 2,035 tumepewa sisi Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuhakikishie tu Mheshimiwa Kimei na Bunge lako Tukufu kwamba katika maeneo ambayo tutakwenda kuyafanyia kazi ni kuhakikisha kwamba tunakwenda kupunguza upungufu wa Walimu katika vyuo vyetu vya ufundi lakini Wahadhiri katika vyuo vyetu vikuu pamoja na Walimu katika vyuo vyetu vya FDC na maeneo mengine. Kwa hiyo, Mheshimiwa Kimei jambo hili tunakwenda kulizingatia kwa ukaribu kabisa kuhakikisha kwamba upungufu huu tunakwenda kuupunguza kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili; Mheshimiwa Shigongo amezungumzia habari ya uanzishwaji wa Mfuko wa Ubunifu (National Innovation Fund), napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Shigongo kwamba mwaka 1995 Serikali kupitia COSTECH ilianzisha mfuko huu wawabunifu ambao ulikuwa unaitwa MTUSATE. Kwa hiyo, jambo hili tayari Serikali imeshalifanyia kazi na kila mwaka Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kuwaendeleza wabunifu mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 zaidi ya Shilingi Bilioni 3.5 zilitengwa kwa ajili ya mfuko huu lakini kwa mwaka 2022/2023 tumekwenda kutenga zaidi ya Bilioni Tisa kwa ajili ya kuuboresha na kuusimamia mfuko huu ili bunifu zetu zilete tija na kutoa majawabu katika changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho alizungumza Mheshimiwa Kishimba suala la kuwahusisha Askari katika usimamizi wa mitihani. Naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu katika taratibu zetu za mitihani hasa ile mitihani ya Shule za Msingi pamoja na Sekondari tuna Kamati zetu za Mitihani za Taifa, Kamati za Mitihani za Mikoa pamoja na Kamati za Mitihani zile za Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili la Halmashauri huwa tunawahusisha Askari katika ulinzi wa mitihani hii la siyo usimamizi wa mitihani kule darasani.

Mheshimiwa Spika, ifahamike tu mtihani wa Darasa la Saba kwa ujumla wake unagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 38.6 sasa tukisema tu kwamba tuuache ule mtihani uende ukafanyike katika mazingira ambayo siyo ya usalama, patakapotokea uvujaji wowote wa mtihani tafsiri yake ni kwamba Taifa linakwenda kuingia hasara ya zaidi ya Shilingi Bilioni 38.6. Kwa hiyo, Askari hawa tumekuwa tukiwahusisha kwenye usafirishaji wa mitihani kutoka katika Mikoa kwenda Halmashauri lakini kutoka Halmashauri kwenda katika center ambazo mitihani inafanyika lakini siyo kwamba Askari anaingia katika chumba cha mtihani na kujihusisha moja kwa moja katika usimamizi wa mtihani. Kwa hiyo, Askari wale wapo katika muktadha wa kuhakikisha kwamba usalama wa mitihani wakati inahifadhiwa lakini usalama wa mitihani wakati inafanyika unaenda sawa sawa ili kutoliingiza Taifa kwenye hasara hii kubwa.

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho amezungumza mzungumzaji wa mwisho hapa, amezungumza suala la uwekezaji katika elimu na sisi Serikali yetu imewekeza katika eneo hili la elimu, pia amezungumza suala la scholarship na vitu vingine hili tutakwenda kuliona katika bajeti yetu ya mwaka 2022/2023 kwamba tumetoa kipaumbele kwa kiasi kikubwa kuhakikisha kwamba tunapata scholarship kwa ajili ya vijana wetu kwenda kupata umahiri na utalaam nje ya Taifa letu.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa ufupi tu nilikuwa naomba kutoa ufafanuzi katika maeneo hayo, naomba kuwasilisha na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)