Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nami nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, katika mijadala inayoendelea moja ya hoja kubwa ambayo imejadiliwa ni kuhusu mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali hapa nchini na hasa katika kipindi hiki ambapo tupo katika majanga mbalimbali ikiwemo iliyokuwa UVIKO pia na yale yanayoendelea huko katika nchi za Ukraine na Urusi.

Mheshimiwa Spika, changamoto hii ya mfumuko wa bei siyo ya Tanzania tu ni maeneo yote au dunia nzima na Serikali tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali kuona namna gani tunapunguza makali ya maisha ya wananchi katika kuhakikisha bidhaa nyingi zinapatikana kwa bei nafuu.

Mheshimiwa Spika, mwelekeo wa sera ya nchi yetu ni kuona tunaachia nguvu za soko huria katika kuendesha biashara. Hiyo haiachi jukumu la Serikali la kuhakikisha tunalinda ushindani wa haki kwenye soko pia kuhakikisha mlaji nae analindwa.

Mheshimiwa Spika, tutakumbuka sote kwamba bei za bidhaa mbalimbali kuanzia mbolea pia bidhaa muhimu kama sukari lakini pia na vifaa vya ujenzi, mafuta ya kula na kadhalika vilipanda bei sana, ilianza mwaka jana mwezi wa Desemba.

Mheshimiwa Spika, kama Serikali tulianza kuchukua hatua za awali za haraka kuhakikisha tunapunguza makali hayo ambayo yanatokana na bei hizi kuwa juu.

Mheshimiwa Spika, moja ya vitu ambavyo tumefanya kwanza ni kukaa na wazalishaji kuongea nao hasa wale wanaoanzisha bidhaa za ndani. Bidhaa ambazo zilikuwa zimepanda bei sana mwaka jana na hata hivi karibuni zimeendelea nyingine ni pamoja na vifaa vya ujenzi. Mtakumbuka vifaa vya ujenzi vilikuwa vimepanda sana pia vinywaji baridi, tulipokaa na wazalishaji tulikubaliana na kuona maeneo mahsusi ambayo yalikuwa si sahihi na hasa kupitia Tume ya Ushindani ambao wanajukumu la kuhakikisha sheria ya ushindani inatumika kudhibiti vitendo vya kuvuruga mwenendo wa soko au bei ya bidhaa sokoni.

Mheshimiwa Spika, ninyi ni mashahidi Waheshimiwa Wabunge wataona kwamba bei za saruji angalau zimepungua kidogo, ingawaje bado tunaendelea kufanyia kazi lakini pia na bei za vinywaji baridi zilipungua lakini pia tunaendelea na kazi hiyo kwa sababu kazi ya kuhakikisha ushindani wa haki na kulinda mlaji ni endelevu siyo kazi ya siku moja.

Mheshimiwa Spika, hivyo tunaendelea kuhakikisha kwamba bei za bidhaa mbalimbali zikiwemo, sasa tumeona bei za vyakula vya kawaida kwa maana ya mchele, maharage na kadhalika navyo pia vimepanda bei. Moja ya changamoto tuliona katika kukaa na wazalishaji na wasafirishaji ilikuwa kwenye eneo la usafirishaji ambalo kimsingi tunaendelea kulifanyia kazi ili tuone ni namna gani ya kuhakikisha tunadhibiti upandaji holela wa bei za bidhaa katika soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za muda mfupi ni hizo lakini pia hatua za muda wa kati ni pamoja na kuendelea sasa kuhakikisha tunaendelea kuweka vivutio au motisha maalum kwa ajili ya uzalishaji wa ndani, kuhakikisha tunawezesha viwanda vyetu vya ndani vinavyozalisha ili viweze kuendelea kuzalisha kwa tija, hii tumeendelea kuchukua hatua ikiwemo tarehe 25 Machi tuliweza kutia saini mikataba ya utekelezaji kati ya makampuni ambayo yapo kwenye miradi ya kimkakati au mahiri hii ikiwemo Intracom ambao wapo hapa Dodoma watazalisha mbolea, pia Bagamoyo Sugar ambao wataenda kuzalisha sukari pia Taifa gas, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar na wale wenzetu NAFO ambao watazalisha Gypsum Board na Gypsum Powder.

Mheshimiwa Spika, hii mahsusi kuhakikisha uzalishaji wa bidhaa unaoweza kufanyika ndani ufanyike kwa tija ili kuhakikisha tunapunguza utegemezi wa kuagiza bidhaa kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha tunakuwa na uhakika wa kuwa na bidhaa hizi muhimu tunaendelea sasa kuhakikisha tunaweka mazingira wezeshi na bora ili tuweze kupata wawekezaji wengine kutoka nje kuhakikisha kwamba bidhaa nyingi tunakuwa na uwezo wa kuzalisha nchini badala ya kutegemea kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumeona kwamba mfumuko huu wa bei maeneo makubwa mengi yametokana na tunasema imported inflation ambao umetokana na kupungua kwa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali huko nje, hata kwa malighafi ambazo zinatumika katika viwanda vya ndani lakini ambazo zinatoka nje, zile malighafi ambazo zipo ndani tutaona ni namna gani tutahakikisha tunaweka mazingira ili ziweze kuzalisha bidhaa ambazo zitakuwa hazina bei ghali.

SPIKA: Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.