Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Awali ya yote napenda kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuongeza bajeti katika miradi ya maendeleo na maeneo mbalimbali hii inadhihirisha kuwa kweli uchungu wa mwana aujuae mzazi na hasa mama.

Mheshimiwa Spika, nipende kutoa shukrani kwa Serikali kwa kuongeza bajeti ya maendeleo inayogusa moja kwa moja kwa wananchi hasa bajeti ya Mradi wa TASAF, ujenzi wa barabara za vijijini, upimaji wa ardhi na miradi ya maji. Pia niipongeze sana Serikali hasa kwa kuongeza bajeti ya kushughulikia masuala ya maafa, wote ni mashahidi kuwa nchi yetu hivi karibuni ilikumbwa na maafa, hivyo niipongeze sana Serikali kwa hatua hii.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa kutoa ushauri wangu; kwanza mchakato wa kuchagua wanufaika wa Mradi wa TASAF uongezwe umakini ili tuweze kupata wanufaika wanaostahili, tofauti na sasa maana kuna baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu wamekuwa wanaingiza wasiostahili bila sababu za msingi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ardhi, kumekuwa na migogoro mingi japo utatuzi wa migogoro umekuwa wa kusuasua na baadhi ya Mabaraza ya Ardhi yamekuwa chanzo cha migogoro kuongezeka, hivyo nashauri Serikali kuangalia mabaraza haya kwa jicho la kipekee ili yatende haki.

Kuhusu sekta ya afya nazidi kuipongeza Serikali kwa kuendelea kujenga hospitali kwa kila Wilaya, vituo kwa kila kata na zahanati kwa kila Kijiji. Katika mkoa wetu wa Simiyu tunaomba sana kupewa watalaam zaidi wa afya ili waweze kuendana na mitambo mipya na ya kisasa ambayo Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikileta mkoani kwetu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu zao la pamba; hili ni moja ya zao la mkakati ambapo kwa asilimia 50 linazalishwa katika mkoa wa Simiyu, pia niipongeze Serikali hasa Wizara ya Kilimo kupitia Waziri Hussein Bashe na wenzie kwa kugawa vitendea kazi kwa Maafisa Ugani nchi nzima. Nashauri pia motisha iende pia kwa wakulima wa pamba kwa kupandisha bei ya kununulia zao hilo ili kuleta tija kwa wakulima kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeweza kuitekeleza ajenda 10 kwa 30, kilimo ni biashara.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya nashukuru sana na naunga mkono bajeti hii.