Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kupata fursa ya kuchangia hotuba hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, sekta ya kilimo; hivi mkulima ni nani? Ni vigezo vipi vinafanya umuite mkulima? Je, ile asilimia 76 au 65 ya ajira za wakulima huwa mnaitoa wapi? Je, mnayo orodha ya wakulima wa nchi hii kwa asilimia? Mmewaainisha kila daraja? Tunalenga kuwa na wakulima wangapi?

Mheshimiwa Spika, Serikali ije na majibu hayo, tumeona Mheshimiwa Rais ametoa vifaa kwa Maafisa Ugani, ni jambo jema. Tunaitaka Serikali kupitia maafisa hao watuletee sasa majibu hayo.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu; Serikali ihakikishe wakulima wanapata mafunzo juu ya kilimo bora. Tuwekeze TARI kwenye tafiti ili kupata mbegu mpya na bora, vinginevyo hatutaweza kushindana na wenzetu nchi nyingine. Tuwekeze katika mazao ya kimkakati.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu ukurasa 26 imeeleza hali ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo. Takwimu za Wizara zinaonesha mahitaji ya uzalishaji na usambazaji wa mbolea nchini hadi tarehe 28 Februari, 2022. ni kama ifuatavyo; makadirio ni tani 698,280, jumla ya upatikanaji ni tani 480,848, kilichouzwa ni tani 283,411. Hii inaonesha kuwa pamoja na upatikanaji huo wa mbolea bado wakulima wanashindwa kununua sababu ya gharama hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kupanda bei ya mbolea, Urea mfuko kilo 50 imeongezeka kwa wastani wa shilingi 55,000 hadi 130,000 sawa na ongezeko la asilimia 120; CAN mfuko mmoja shilingi 34,000 hadi 125000 sawa na ongezeko la asilimia 150; DAP sh 60000 had 120000 ongezeko la asilimia 100. Mfumuko huu utasababisha kuingia kwa baa la njaa siku za usoni na uzalishaji utapungua. Nini kifanyike?

Mheshimiwa Spika, Serikali ichukue hatua za haraka ili kunusuru mfumuko huu wa bei, pia Serikali itoe motisha maalum kwa wawekezaji wa viwanda vya mbolea nchini. Aidha, Serikali ipunguze kiwango cha tozo za mrahaba kwenye malighafi za mbolea zinazochimbwa nchini. Serikali itoe ruzuku kwenye mbolea ili kushusha gharama na bei iwe nafuu kwa wakulima na Serikali iweke bei elekezi ya usambazaji hadi mwisho.