Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia, lakini niseme tu kwamba hoja, michango na maoni ya Waheshimiwa Wabunge kwenye mpango huu sisi Wizara ya Madini tunayapokea yote na kuahidi kwamba tutakwenda kuyafanyia kazi kwa nguvu zetu zote. Hili linatokana na ukweli kwamba sekta yetu ya madini Waheshimiwa Wabunge hawa wamekuwa walezi wakubwa wa kushauri mahali ambako tunaona hatuendi sawa, wamekuwa wepesi haraka kutufikia na kutuambia turekebishe wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa spirit hiyo hiyo nataka nikuhakikishie na bila kupoteza muda wa Bunge lako, kwamba maoni yote waliyoyatoa Waheshimiwa Wabunge kwenye mpango huu tunaamini mtoa hoja ameyapokea na sisi Wizara ya Kisekta tumeyapokea na tutayafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda mmoja tu, la kutoa comfort kwa Waheshimiwa Wabunge, ni kwamba wamesema wengi kwamba GST ipewe mamlaka ya kufanya utafiti wa kina juu ya upatikanaji wa madini hapa nchini. Jambo hili ni la kweli, na hivi karibuni Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi tumefanya marekebisho makubwa kwenye sheria ya madini ambayo sasa imewapa mamlaka GST kufanya utafiti wa kina. Kwa sheria iliyokuwepo huko nyuma ni kwamba GST alikua anakomea kwenye kuchora ramani na kutoa taarifa za awali za madini, lakini uchambuzi na utafiti wa kina GST hakuwa na mamlaka hayo. Marekebisho tulioyafanya juzi hapa sasa yamempa mamlaka GST kufanya utafiti wa kina na kutupa taarifa za kina za madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hilo mtaona tofauti baada ya kuwa sheria imeanza kufanya kazi na Serikali imejipanga. Mheshimiwa Rais, ameshakubali kabisa kwamba ni lazima tufanye utafiti wa kina kwa nchi yetu. Hali tuliyonayo sasa hivi, utafiti tulionao wa ki-jiofizikia wa high resolution ni asilimia 16 tu ya nchi yetu. Sasa ni lazima tufanye zaidi angalau tufike asilimia 50-60 ili tujipatie uhakika zaidi wa rasilimali hii kutambua ziko wapi; na hata kama tunapata wawekezaji wanaokuja kwetu basi tuwe na uhakika bila shaka yeyote kuwaambia kwamba tuna hiki na kiko mahali gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni madini mkakati, Waheshimiwa Wabunge wengi wameelezea habari ya madini mkakati. Nataka niwahakikishieni Waheshimiwa Wabunge kwamba tumeweka utaratibu mzuri sasa, kwa sababu madini mkakati ndio yanayohitajika dunia kwa ajili ya mabadiliko ya kiteknolojia. Watu wanahama kutoka kwenye matumizi ya mafuta na kwenda kwenye matumizi ya betri. Ni lazima kama Taifa tusibaki nyuma na sisi tuchangamkie hiyo fursa. Mataifa makubwa yanakuja kwetu kutafuta madini hayo, kwa sababu tumerekebisha sheria hii, tutakacho kwenda kufanya sasa ni kuangalia mapping ya kujua madini mkakati haya yako wapi. Yametajwa ya aina nyingi na; ndiyo maana mtaona miradi mingi mikubwa ambayo inachimba madini mkakati kama nickel. Sasa hivi imeanza kuchimba kule Kabanga lakini na mahali pengine. Madini kama rare earth elemets tunakamilsha majadiliano na PRG ili madini yale yaanze kuchimbwa. Kule Niobium kwenye eneo la Panda Hill na kwenyewe tunakamilsha majadiliano ili madini yaanze kuchimbwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilitaka niseme hayo machache ili Waheshimiwa Wabunge wapate comfort kwamba mawazo yao na maoni yao yote kwa pamoja tumeyapokea na nikushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)