Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi nichangie katika Mpango huu. Nianze kwa kuupongeza mpango pia niseme tu tunapokea maoni na ushauri wa Wabunge ambao wameutoa japokuwa hapo baadae nitatoa ufafanuzi kwa kufafanua baadhi ya mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwamba Wizara ya Ardhi ni Wizara wezeshi, na Mpango wa Maendeleo unaozungumzwa katika suala zima la uwekezaji hususani kwenye miundombinu Wizara ya Ardhi inayo mchango mkubwa kuhakikisha kwamba inaweka mazingira mazuri ili kuweza kuona mpango huo unakwenda vizuri.

Mheshimwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha huu ambao tunaendelea na tutakaokwenda kuendelea nao mwaka ujao, tunao ule mradi wa kuimarisha miondombinu kwa ajili ya upimaji. Tunatambua nchi imepimwa kwa asilimia isiyozidi 30 ni kama asilimia 25. Kwa hiyo kwa sasa tunazo pesa zile ambazo ni Dola za Kimarekani milioni 65 ambazo zitatumika kuimarisha miundombinu ya upimaji na tutakwenda kupima nchi walau katika sehemu kubwa. Lakini pia kuna ile ya uboreshaji milki, ambazo ni Dola za Kimarekani milioni 150. Kwa hiyo ukikamilisha maeneo hayo maana yake tutakuwa na zile base map ambazo zitakuwa zinatupa picha ya kuweza kupanga matumizi ya maeneo katika nchi nzima ikiwemo na hiyo miradi ya kimkakati ambayo tunayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uchangiaji jana Mheshimiwa Mbunge wakati anachangia ilionesha kwamba pengine maamuzi ya Serikali ya eneo la Mbarali yangeweza kufifisa matarajio ya Watanzania pengine katika suala zima la kuichumi. Naomba kwanza niwatoe wasiwasi wananchi kwamba, mpango ule ambao umewekwa na Serikali ikiwemo hiyo ya mabwawa kama alivyosema Waziri wa Kilimo uko pale pale na mabwawa yale yapo mbali na eneo ambalo wananchi wameondolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile maeneo yale ambayo wananchi wameondolewa ni vijiji vitano na si vijijini 48 kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge alisema. Vijiji hivyo vitano vinavyoondolewa tayari elimu imeanza kutolewa ambapo maendeleo yanaenda vizuri na wanaweka alama kuhusiana na wapi wanaishia. Lengo letu ni kuhifadhi lile eneo ili maji yaendelee kutiririka katika Mto Ruaha ambayo yanapeleka kwenye Bwawa la Mwalimu la Nyerere. Kwa hiyo tukiharibu miundombinu ya pale maana yake ni kwamba tutajikuta tumeharibu mkakati mzima wa kuwa na umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo suala la kusema kwamba pengine labda tuanaondoa uchumi wa wananchi, tunaimarisha uchumi wa wananchi kwa kuwa na miundombinu ya uhakika itakayotuma umeme wa uhakika na uzalishaji utakuwa ni mzuri…

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri kuna taarifa, Mheshimiwa Sanga.

T A A R I F A

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafuatilia majibu ya Mheshimiwa Waziri. Katika miradi 54 ambayo yamesaini kuna maeneo mawili ambayo wananchi wanaondolewa na miradi inaenda kujengwa. Moja ya eneo hilo linaitwa Mwendamtitu wanaenda kujenga mradi wa umwagiliaji na wananchi wanaondolea. Eneo la pili linaitwa Madibila Phase II wanaenda kujenga mradi wa umwagiliaji na wananchi wanaondolewa. Katika maeneo hayo wanayowaondowa Serikali imeshapeleka combined harvest machine 15 kwa ajili ya wananchi hao ili waweze kuendelea kulima, lakini kwa ripoti ya Mheshimiwa Waziri nampa taarifa kwamba hata dakika hii ninavyozungumza wananchi wanaweka beacon kwenye maeneo hayo ili wananchi waondoke na hawana taarifa na hawajashirikishwa.

MWENYEKITI: Kwa sababu Waziri ametaja idadi ya vijiji, kasema ni vijiji vitano na si 48 hivi vijiji unavyovitaja wewe viwili, vipo katika vitano ambavyo Waziri hajavitaja, vinavyoondolewa.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa sababu hajataja majina ya hivyo vijiji, kwa hiyo sijajua ni vijiji gani anavyovitaja lakini ninavyotaja mimi, ni hivi vijiji vya…

MWENYEKITI: Labda hivyo vipo kwenye yale mengine. Mheshimiwa Waziri vijiji vitano vinanavyoondolewa haya mawili sijajua kama unayo ile orodha ya hivyo vijiji vitano ama hauna tunaweza kupata taarifa baadae.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo taarifa yote ya vijiji vinavyobaki ambavyo ni kumi na tano, vijiji vinavyoondolewa ni vitano. Halafu…

MWENYEKITI: Sawa sasa hebu tusaidie hivyo vijiji vitano, hivi viwili anavyovitaja Mheshimiwa Mbunge hapa vimo katika hivyo vitanno au havimo.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vinavyoondolewa ni kijiji cha Luhanga, Madundasi, Msanga, Iyala na Kilambo. Mabwawa yanayokwenda kujengwa katika eneo lile katika Wilaya ya Mbarali, mabwawa yaliyotajwa yanajengwa na umbali wa bwawa ambapo yapo hayako kwenye yale maeneo ambayo wananchi wanaondolewa. Tunalo bwawa mmoja Scheme ya Msesule liko kilometa tano kutoka pale ambapo wananchi wanatolewa, tunayo scheme ya Utoro na Scheme ya umwagiliaji ya Isenyela ziko kilometa 11 kutoka pale mwananchi wanapotolewa. Tunayo Scheme ya Chozi na Scheme ya umwagiliaji ya Heman iko kilometa 30 kutoka pale wananchi wanapotolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokisema hapa, lengo la Serikali inachofanya ni kutaka kuweka mazingira mazuri kwa miradi ya kimkakati ambayo ndiyo inakwenda kukuza uchumi, moja wapo ikiwa ni hilo bwawa la Mwalimu Nyerere.

MWENYEKITI: Mimi nimekuelewa Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Mbunge ulikuwa unatoa taarifa, hivyo vijiji vilivyotajwa kuondoka, Mheshimiwa Waziri amevitaja, hizo scheme mbili ulizotaja zipo katika vile vijiji vitano au ni nje kwa kuwa ulikuwa hujamsikia bado Waziri.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo kwenye hivyo vijiji vitano kwenye Mwendamtitu na Madibila phase II.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Kilimo hizo scheme zipo upande gani? Hizo scheme mbili alizozitaja.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Scheme ya Madibila Phase II, Phase I imekamilika, Phase II kuna kipande ambacho kinaingia kwenye GN 28 siyo Phase II 100 percent. Kuna kipande kinachoingia ndani ya GN 28. Tunachokifanya ni kwamba wakati technical team inaendelea kule ground na sisi ndani ya Serikali tunaendelea kufanya consultation. Kwa hiyo nimwambie…

MWENYEKITI: Haya hiyo ni nini? Mbarali nini, Madiba Phase two, hiyo scheme nyingine Mheshimiwa Waziri.

MHE. FESTO R. SANGA: Hiyo scheme nyingine ipo Mwendamtitu.

MWENYEKITI: Haya Mwendamtitu? Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, imo au haimo?

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika scheme ambayo inayoathirika ni Madibila phase II tu.

MWENYEKITI: Pekee yake?

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, yes.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Ardhi.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kwa kutoa ufafanuzi pia. Zoezi ambalo linaendelea sasa hivi ni kuonesha mipaka kwa sababu kilio cha wananchi wa Mbarali alichokuwa anakisema walikuwa wanalamamikia GN Namba 28. GN namba 28 iliwekwa 2008 kwa Muswada ambao ulipitishwa hapa na baadaye ukaridhiwa na Mheshimiwa Rais kwa ajili ya ku - protect yale maeneo ya hifadhi ambayo yanapeleka Maji Mto Ruaha na unaokwenda mpaka Mtera pamoja na Kidatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kile kinachofanyika pale sasa hivi ni kuhakikisha kwamba, mpaka unaainishwa ili maeneo yale ambayo yanatunza vyanzo vya maji na mapokeo, ile catchemet area yote ya maji, iweze kubaki wazi na kurudisha ecolojia ya pale ili miradi tunayokwenda nayo isije kuwa imevuruga yote. Kwa sababu tunatambua pia uhifadhi hauruhusu shughuli za kibinadamu; tukiruhusu maana yake tunakwenda kuharibu pia ile hifadhi ya Mto Ruaha.

MHE. BONIPHANCE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. BONIPHANCE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi nataka kuiona hii dhana ya kusema sawa tunatunza vyanzo vya maji kwenye eneo. Hivi tatizo la Mto Ruaha kuisha maji, ni kwamba maji hayaendi mtoni au ni kwamba ule mto umekuwa tambarare maji yote yakienda yanapita yote. Lazima hili nalo tulione, Kwa sababu maji yanaweza kuingia masaa yote ya mvua lakini yakaondoka yote yakaenda ziwani. Tutafute alternative nyingine ya kuweza kuzuia maji kwenye Mto Ruaha. (Kicheko)

MWENYEKITI: Nadhani alikuwa anachangia zaidi kuliko kukupa taarifa, Mheshimiwa Waziri, malizia mchango wako.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza pamoja na mchango wake lakini majibu anayo pia. Kwa sababu unapofanya shughuli za kibinadamu karibu na eneo la hifadhi ya mto maana yake yale maporoko zile siltation inayofanyika inakwenda kuondoa kina cha maji. Matokeo yake…

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki anachokizungumza, kwamba maji ya Mto Ruaha yamekauka kutokana na shughuli za wale wananchi wanaolima pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa taarifa, wananchi wanaolima lile eneo linaloondolewa ambalo ni hekta 53,000, wanalima kati ya mwezi wa kumi na mbili, wa kwanza hadi wa nne na watano. Yale maji hayachepushwi kuingia mashambani kwa wakulima, lakini ni estate mbili ambazo ni za mwekezaji na sisi tunaungana nao wale wawekezaji, ndio wanaotumia maji yanayotoka kwenye Mto Ruaha kwenda estate zao. Kwa hiyo, si wale wakulima wanaotumia wao maji. Wanatakiwa mlifahamu hilo.

MWENYEKITI: Sawa, umeeleweka. Mheshimiwa Waziri hajasema wale ndio wanaokausha maji. Sijamsikia akisema maneno hayo, kwamba shughuli zile ndizo zinakausha maji ila alikuwa anaendelea na sentensi kwamba ukifanya shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya vyanzo. Sasa alikuwa anaendelea kwa sababu alikuwa anamjibu Mheshimiwa Getere. Kwa hiyo alikuwa hajamaliza hoja yake ni nini kwenye hili. Kwa hiyo nampa nafasi Mheshimiwa Waziri, endelea.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kutoa ufafanuzi ni wazi ni kweli nilkuwa naendelea moja wapo nimesema ni kufanya shughuli za kibinadamu. Pia ule uharibifu mkubwa wa mazingira uliopo katika maeneo yale ndicho chanzo pia kwanza cha kukosekana mvua ya uhakika ambayo inaweza ikapeleka maji katika yale maeneo. Kwa hiyo kile kitu kinachofanyika pale kinafanya pia hata mtiririko mzima wa maji, vile vijito vinavyopeleka maji kwenye Mto Ruaha navyo vinakauka. Maana yake ni kwamba hatima yake kutakuwa na ukame ambao hautaweza kurejesha tena ekolojia ya pale jinsi ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe mwenyewe unafahamu, historia ya eneo lile namna ambavyo Tume na Kamati mbalimbali …

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume na Kamati mbalimbali zikiwemo hata na Kamati za Bunge, zimekwenda na majibu yao yalikuwa ni yale mapendekezo ya kutaka kuhakikisha kwamba shughuli za kibinadamu pale zinasimama ili kulinda mazingira yale na kulinda hifadhi ambayo tulikuwa nayo kama uchumi wa Taifa letu unavyotegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kusema hayo. Lakini katika eneo hilo pia si wote wanaondolewa kuna vijiji 15 kama nilivyosema vinabaki na vingine 14 ni baadhi ya vitongoji. Unaweza ukakuta kwenye kijiji kitongoji kimoja na nilitaja vyote na orodha ninayo hapa, wakihitaji tunaweza kuwapa. (Kicheko)