Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami nichangie kwenye wasilisho hili la Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Pili naomba niseme Waheshimiwa Wabunge kama Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara tumewasikia, maoni yenu tumepokea na tunakwenda kuyafanyia kazi ili tunapokuja sasa na mpango wa maendeleo kwa mwaka 2023/2024 uwe umebeba maaoni ya wananchi kwa sababu Wabunge ni wawakilishi wa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya hasa kwa kufungua Taifa letu, kwa kutuletea wawekezaji na kutuletea wafanyabiashara wa kutosha pia kuwapeleka wafanya biashara wa Tanzania kulifikia soko la Dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamesemwa mengi kama nilivyosema tumepokea naomba nisemee moja tu nalo ni kuhusu Bagamoyo Special Economic Zone. Tunapoiongelea eneo maalum la kiuchumi la Bagamoyo lina miradi kadhaa ambayo bandari ni sehemu mojawapo ya miradi hiyo iliyopo kwenye eneo hili. Kwa hiyo, ningeomba sana Waheshimiwa Wabunge na nashukuru mmesema mawazo mema na mazuri ambayo kama Serikali tumeendelea kuyafanyia kazi na niwashukuru sana Viongozi wetu wa Taifa hili kuanzia Rais wetu Mstaafu wa awamu ya Tatu aliliona na likawekwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo ambayo imeanza kutekelezwa mwaka 2000 mpaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne akalibeba na kuanza utekelezaji wake, Mheshimiwa Rais wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli naye kwenye Awamu ya Tano alilifanyiakazi na ikafika alipolifikisha. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amelibeba jambo hili na ameliondoa kwenye mkwamo uliokuwepo. Kwa sababu mwanzo ilikuwa inaongelewa bandari peke yake, Mheshimiwa Samia suluhu Hassan amesema tukijenga bandari peke yake bila miundombinu mingine wezeshi hiyo bandari haitofanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijenga bandari peke yake bila kuwa na Mji wa viwanda pale Bagamoyo tutakuwa hatujafika dhamira njema iliyowekwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo. Katika hili ukijenga bandari bila kuwa na logistic hub utakuwa hujafanya lolote. Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo na nikushukuru sana wewe Mheshimiwa Mwenyekiti na Bunge lako Tukufu lilitupitishia bajeti na sasa tunahitimisha kufanya mapitio ya mpango kabambe wa eneo zima la Bagamoyo ambalo tunahitimisha Tarehe 15/11/2022 tukishakuwa na master plan mpya itatueleza sasa ni kipi cha kufanyika kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iliulizwa pia kuhusu eneo hili kuhusu fidia wapi tumefikia. Niseme kwa historia nilioitoa yapo maeneo ambayo tayari yalishalipiwa fidia na yako maeneo ambayo yalikuwa hayajalipiwa fidia. Eneo lote ambalo lilitarajiwa enzi hizo kujengwa bandari lote la hekta 800 lilishalipiwa fidia, lakini eneo lote ambalo lilikuwa lijengwe Chuo cha Teknolojia tayari lilishalipiwa fidia nalo ni eneo la hekta 179.7.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lote pia ambalo lilikuwa lijengwe Chuo cha Uongozi ambalo ni hekta 198 lililipiwa fidia, eneo lililobaki lilikuwa halijalipiwa fidia kwa sababu kulikuwa na changamoto ndani yake na ndiyo maana ya Serikali kuelekeza sasa turejee kwenye mpango kabambe mpya ili eneo hili sasa tuhitimishe na tuwalipe fidia wale waliotakiwa kulipwa, lakini wapo Watanzania wenye maeneo yao kwenye eneo hili ambao wako tayari kuwekeza hatutakiwi kuwalipa fidia kwa sababu wanawekeza kulingana na mpango kabambe. Kwa hiyo, hili tunalibeba tunakwenda nalo niwahakikishie wananchi wa Bagamoyo, niwahakikishie Watanzania tuko tayari kwa ajili ya eneo hili. Ahsante sana. (Makofi)