Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie nafasi nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Pili, niseme tu kwamba Waheshimiwa Wabunge tumeyasikia maoni yao na ushauri wao na ndoto zao na sisi kama Wizara na upande wa Serikali tutaendelea kuyafanyia kazi kadri ambavyo Mwenyezi Mungu anatujalia na upatikanaji wa rasilimali (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nichangie mambo machache tu. Kwanza ni ukweli kihatarishi namba moja ambacho kinatukabili kama Taifa ni mabadiliko ya Tabianchi. Kama Serikali ukiangalia kwamba ukuaji wa population unakua kwa wastani wa 3.2% na Sensa iliyopita imetuonesha kwamba umri wastani wa Mtanzania ni kati ya miaka 16 na 18 maana yake society ambayo ina watu wenye umri mdogo sana lakini sekta iliyoajiri watu wengi ndiyo ambayo ina mchango mdogo na ukuaji wake ni mdogo ni jambo la ukweli ambalo halipingiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imechukua hatua za maksudi, nalishukuru Bunge, ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa niaba ya wakulima, Serikali imeongeza fedha katika mwaka uliopita na tumeanza kuchukua hatua, tunazo ekeri jumla ya Milioni 29 zinazofaa kwa umwagiliaji, huko nyuma kwa muda mrefu tumekuwa tukijenga miundombinu ya umwagiliaji ambayo imekuwa inasubiri na yenyewe kudra ya Mungu mvua inyeshe ndiyo watu waweze kuitumia hiyo miundombinu. Kwa mwaka huu wa fedha tunajenga Mabwawa 13, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge na Kamati ya Bajeti, hatua ya Serikali kujenga mabwawa katika maeneo ya Kati siyo hatua ya kutilia mashaka. Ni hatua ambayo umefanyika utafiti wa kisayansi na kujiridhisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajenga bwawa kubwa la Msagali liloko Mpwapwa lenye uwezo wa kuhifadhi Milioni 95m3 ambalo litamwagilia eneo kubwa la umwagiliaji. Tunajenga Mabwawa Dodoma, Simiyu, Mwanza, Singida, Tabora, Kigoma na Manyara. Haya ni kwa mwaka huu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili ambayo tumechukua mtaona mwaka ujao wa fedha mlitupitishia fedha hapa ya kwenda kufanya feasibility study na design kwenye Mabonde 22 ya nchi yetu, yakiwemo Mabonde ya Lake Victoria, Mabonde yaliyoko Ziwa Nyasa, Mabonde yaliyoko Mto Ruvuma. Mabonde yote haya sasa hivi tumesha-commission na watu wanafanya feasibility study ambayo tutaanza kuyajenga katika mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inayokabili sekta ya kilimo ni tija na tija ina-equation; Kwanza ni utafiti, Pili ni uzalishaji wa mbegu, Tatu ni extension services, Nne ni kuwa na miundombinu ya uhifadhi na miundombinu ya umwagiliaji. Serikali ya Awamu ya Sita imeanza kuchukua hatua hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uzalishaji wa mbegu mmetupitishia fedha hapa, kutoka Bilioni 15 kwa ujumla wake mpaka Bilioni 83. Tunafanya nini? Tumeanza kujenga miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya kuzalisha mbegu, ambayo toka tunapata uhuru hayakuwepo haya mashamba yakiwa na miundombinu ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanza kujenga mwaka huu tunajenga hekta 95,000 kuongeza mtandao wetu wa umwagiliaji. Miundombinu ya DADPs na mingine yote ambayo ilikuwa inasubiri mvua za Mungu na yenyewe tunaijengea mabwawa. Kwa hiyo, nilitaka niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba hii ni hatua ambayo tunaichukua na niseme hapa kwamba kilimo ni process, hatuwezi kutegemea matokeoya kwenye kilimo kesho, ni lazima tu-invest kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ninataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge msiwe na hofu na mashamba ya block farm, kwa nini? Vijana wengi wanaomaliza Vyuo Vikuu hawaendi kwenye kilimo kwa sababu kubwa tano: Moja, hawana ardhi, Mbili, hawakopesheki, Tatu, Teknolojia zimepitwa na wakati, Nne, suala la masoko ya uhakika. Miradi hii ya jumla ya ekari 188,000 ambayo phase one tunaanza na Dodoma na Chunya itatengeneza ajira za vijana 40,000 watakaoenda kulima shambani. Serikali inatumia Bilioni 200 gharama ya ajira moja ni Shilingi Milioni Tano. Kwa hiyo nilitaka tu niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge maoni yao tumeyapokea, tunayachukua lakini hii ni process ya muda mrefu ambayo tutaenda kufanya kazi pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu Mheshimiwa Sanga ameongelea miradi ya zaidi ya Bilioni Hamsini tuliyoisaini Mbarali miradi ile haijafa. Tunaenda kujenga zile skimu zote ambazo zilisainiwa mbele ya Mheshimiwa Rais. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Haya ahsante sana. Tusaidie tu jambo moja, hayo mabwawa makubwa yanayojengwa yanajazwa na maji kutoka wapi? (Makofi)

WAZIRI WA KILIMO: Ahsante. Mheshimiwa Mwenyekiti kuna njia mbili ambazo tutajaza maji kwenye mabwawa na nitaliomba Bunge lako, Kamati ya Kilimo imeshaenda kutembelea imeona na tutafanya tour ili waone. Kuna njia mbili za kujaza maji na niseme specifically Dodoma najua hofu iko Dodoma.

MWENYEKITI: Wewe nenda hapo kwa sababu muda wetu umeenda Mawaziri wanasubiri nimeuliza swali dogo tu.

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna njia mbili tu. Moja tunatega maji ambayo kipindi cha mvua yanasafiri yanayopotea. Nasi wote tunajua hapa katikati ya Dodoma, Morogoro huwa tunakaa masaa mamilioni ya lita ya maji yanapita, hiyo ni njia ya kwanza. Njia ya pili Mkoa wa Dodoma una-water reserve nyingi mno underground. Tunalo Bwawa hapo Chinangali ambalo linajaza lita milioni 32 kwa visima vitatu ambapo shamba la hekta 1000 litahudumiwa kwa mwezi mzima bila kutafuta maji sehemu nyingine. (Makofi)