Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii katika dakika hizi za Aziz Ki. Nami moja kwa moja nitafanya lile lengo la kuweka goli katika uchangiaji wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja katika ugharamiaji wa mpango. Katika hili mara nyingi sana huwa zinatajwa fedha ambazo zitakuwepo katika ugharamiaji wa mpango, na wakati mwingine hutaja vyanzo vya ugharamiaji wa mpango, lakini mara nyingi ule ugharamiaji siyo unaokwenda kutumia fedha zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitaeleza, Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake wakati akitaja bajeti ya 2021/2022 alisema kwamba makusanyo yalikuwa ni asilimia 97 ya mapato, lakini fedha za maendeleo, ukitazama taarifa ya Wizara ya Fedha inaonesha kwamba ni zaidi ya asilimia 85. Sasa ukitazama Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022: Je, ulifikiwa kwa asilimia 85? Huwezi kukuta kwamba ulifikiwa kwa asilimia hizo. Sababu zinazopelekea hivyo ni kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi miradi inapopelekewa fedha ambazo tumepitisha kwenye mpango na bajeti, fedha zile zinakwenda kwanza kulipa madeni, claims, interest na variations za miradi. Ukitaka kujua hayo, tutazame percentage ya miradi ambayo labda tunaisema kwenye mpango: Je, kweli tunapokuja kwenye utekelezaji na tunapotoa tathmini inakuwa imefikiwa vile? Inakuwa haikufikiwa hivyo. Sababu ya kutofikiwa ni hizi, kwamba hizi fedha zinaenda kulipwa huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa mfano mmoja. Tulijadili sana hapa kuhusiana na barabara katika bajeti ya 2021/2022, tukaja kugundua kwamba fedha nyingi zilizotengwa kwa ajili ya barabara zilikwenda kulipia madeni kuliko kutengeneza zile barabara zilizotajwa. Kwa kuwa yanatokea hayo, japo kuna msemo kwamba “mpango siyo matumizi,” lakini kwa kuwa Mpango huu tunapanga hapa kwenye Bunge hili, nitoe rai moja. Kwanza, Waziri anapoleta gharama za mpango, anapotaja ile source ya fedha labda kwa mradi fulani fedha hii, basi kile kianzio kiwe ringfenced, na kikiwa ringfenced ina maana hakitaweza kuingiliwa kama zilivyo fedha za REA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, Waziri atakapokuwa anawasilisha labda mradi wa maendeleo, mfano Standard Gauge Railway route ya kutoka Dar es Salaam – Morogoro, anataka kufanya percent ngapi? Ataje baseline na malengo yake ili tukija kutathmini mpango, tukute kwamba fedha zilizotengwa kugharamia huu mpango ziwe zimekwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika dhima ya mpango tutasema ni kujenga uchumi shindani. Mimi nasema ushindani katika usafirishaji. Tuna bandari na tunajenga Standard Gauge Railway. Bandari tunajenga, lakini kuna nchi tunazoshindana nazo; kuna Angola, South Africa, Msumbiji na Kenya. Sisi tuna faida ya kijiografia (geographically advantage), kwamba tunaweza tukapeleka kokote, lakini wenzetu wanatumia mbinu nyingine mbadala katika financing ya mradi wa Standard Gauge Railway. Wenzetu wana-finance mradi wote. Tukitazama nchi nyingine Jirani, wamejenga Standard Gauge Railway, baada ya kuona haitoshi, wanatengeneza mikataba na zile nchi ambazo ni masoko. Wanatengeneza mikataba na Kongo, Zambia, ili kuondoa ile geographical advantage ambayo tunayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasi kama tunataka kujenga uchumi shindani, ni lazima na haya tuyaangalie. Mpango huu utoe jawabu kwamba tunataka kufanya ushindani katika usafirishaji na hawa wenzetu. Kwa mfano, kuna nchi moja ina bandari lakini imeenda kuweka bandari kavu katika nchi nyingine, ambapo nasi katika nchi ile ni soko letu, watu wataenda kuchukulia bidhaa pale. Kwa hiyo, tunataka mpango huu katika usafirishaji hasa kupitia bandari na reli itoe jawabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nije kwenye umeme wa REA. Kuna takwimu ambazo bado sijazielewa. Tulisema tunafanya vijiji 12,000. Tukatoa ripoti 2021/2022 kwamba vijiji 10,000 tayari vimeshafanyiwa. Ila kwenye mpango vimeelezwa vijiji 8,000 ndivyo vilivyofanyiwa, siyo 10,000 tena. Maelezo ya Waziri yanasema vijiji 9,000. Je, tushike kauli ipi hapa? Kwa maana hiyo kama vilifanyika vijiji 10,000, leo tumerudi vijiji 8,000, ina maana bado vijiji 4,000, na Waziri amesema vijiji 9,000. Ina maana bado vijiji 3,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonesha kitu gani? Kitu kinachooneshwa katika tofauti ndani ya Serikali, ina maana kwamba inawezekana vijiji vile tayari vimeshafanyiwa kazi, lakini pengine kwa sisi tunaofikiria kwamba ile gharama yake watu wanataka kuja kuirudisha ipate kutumika visivyo; au kule mwanzo tulipotajiwa vijiji 10,000, ina maana zile fedha hazikutumika kweli kwenye vijiji 10,000 na fedha zile labda badala yake zilifanyiwa vitu ambavyo siyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali itupe takwimu sahihi katika miradi ya REA. Kuna takwimu tatu tofauti; kuna 10,000, 9,000 na 8,000, ni ipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)