Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Haji Khatib Kai

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Micheweni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia, kwa kuniwezesha siku ya leo kuamka salama na afya tele na kuweza kusimama mahali hapa na mimi kuweza kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ulinzi ni muhimu kwa Taifa lolote duniani, kwani bila ya ulinzi ulio imara, Taifa haliwezi kuwa salama. Nianze ku-declare interest, kwanza mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Kati ya miradi ambayo Kamati yetu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ilikwenda kuyatembelea ni mradi wa ukarabati wa majengo na miundombinu. Mradi huu ulitengewa na Bunge likaidhinisha shilingi bilioni nane kamili, lakini hadi Februari, 2016 hakuna fedha yoyote iliyotolewa kwa ajili ya mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni masikitiko na niaibu kubwa. Ni masikitiko kwa sababu Kamati tulipofika kwenye mradi huu, kwa kweli binafsi sisi Wajumbe wa Kamati tuliogopa hata kuingia hata katika majengo ambayo yalitarajiwa kufanyiwa ukarabati katika pesa ambazo ziliidhinishwa na Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika miundombinu hiyo ambayo kuna mess ambayo wanajeshi hawa wanakuwa wanaitumia, kwa bahati mbaya sana wanajeshi hawa ni waungwana na ni waadilifu sana, lakini bahati mbaya sana mess hii inavuja. Ni aibu!
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi mwingine ambao tuliutembelea katika Kamati yetu ni mradi wa ulipaji wa fidia katika maeneo ambayo yalichukuliwa na Jeshi. Mradi huu ulitengewa na Bunge shilingi 7,390,000,000. Hadi kufikia mwezi Februari, 2016 fedha zilizopelekwa ni shilingi milioni 180, wananchi wa Tanzania walikuwa na imani na vyombo viwili vya nchi hii, moja likiwa ni Bunge na la pili likiwa ni Jeshi wa Wananchi wa Tanzania. Kwa bahati mbaya sana Watanzania kupitia chombo chao cha Bunge, wameshakata matumaini kwa sababu ya kukatishwa kuoneshwa matangazo ambayo waliona kwamba wanasaidiwa na wanatetewa na Bunge lao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa chombo cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuwachonganisha na wananchi kwa kutopeleka fedha ambazo zilitegemewa kulipia fidia kwa maeneo ambayo yalichukuliwa na Jeshi, hii ni aibu, ni tatizo na mnasababisha kuwachonganisha wanajeshi ambao walikuwa na imani na wananchi, lakini leo imani hiyo itakuwa imetoweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie uchaguzi wa marudio Zanzibar. Ni mara kadhaa nimemsikia Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akisema kwamba Jeshi la Wananchi wa Tanzania halijapelekwa Zanzibar. Nasema hili siyo kweli, kwa sababu Mheshimiwa Waziri anasahau kwamba wanajeshi hao wanapokwenda Zanzibar hawapitii mbinguni. Wanajeshi hawa wanapokwenda Zanzibar wanapitia baharini, tunawaona wanavyokwenda, lakini pia tunawaona wanaporudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nadhani Mheshimiwa Waziri atafute maneno mengine ya kutuambia, lakini siyo kwamba Wanajeshi hawajapelekwa Zanzibar kwa madhumuni mamoja tu ya kisiasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri huyo huyo amekuwa akisema kwamba wanajeshi waliopelekwa Zanzibar au waliopo Zanzibar, kazi yao ni kulinda amani na usalama wananchi. Nasikitika kusema kwamba hivi wananchi wanapolindwa kwa usalama au Jeshi linapolinda usalama ni kuwatisha wananchi ambao wametulia? Hii haileti maana kwamba ni kuwasaidia na kuwalinda wananchi walioko Zanzibar. (Makofi)
Nasikitika kusema kwamba Makamu Mwenyekiti wangu wa Kamati namheshimu sana, lakini kwa bahati mbaya au bahati njema alisema kwamba watu wamekuwa wakisimama hapa wakizungumza kwamba Zanzibar kulipelekwa vifaru katika uchaguzi wa marudio.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie tu Mheshimiwa Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Ulinzi na Usalama, sawa hata kama vifaru hatuvijui, kwa sababu hatujaenda jeshini lakini tunaona. Kwa hiyo, suala la kusema kwamba watu hawajui, sawa hatujui, lakini tunaona. Kwa hiyo, tunapoona, tunajua hiki ni kirafu. Tumeona na tumeshuhudia wakati wa uchaguzi wa marudio, wanajeshi wakizunguka na vifaa vya kivita mpaka kwenye vijiji. Sasa tunaposema kwamba jeshi lilikuwa limeingilia shughuli za kisiasa Zanzibar, msituelewe vingine. Tunasema kwa jambo ambalo tumeliona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la malalamiko ambayo yapo kwa wanajeshi wa rank ya chini. Wanajeshi wa rank ya chini na ninaomba Mheshimiwa Waziri hapa atakapokuja atoe ufafanuzi, inawezekana hawafahamu lakini pia inawezekana kwamba hawajajua kwa sababu pengine wameingia juzi juzi au hawajakuwa wazoefu katika Jeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanajeshi hawa wa rank ya chini wanasema kwamba kwa kawaida ration allowance inakuwa ni sawa kwa wanajeshi wote, lakini kwa bahati mbaya wamekuwa wakiona kwamba mwanajeshi wa rank ya chini kabisa amekuwa akilipwa shilingi 180,000, lakini kuanzia Koplo, nyota moja hadi nyota mbili wamekuwa wakilipwa kiwango kikubwa ambacho ni tofauti kabisa na difference inakuwa ni kubwa. Kwa hiyo, nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja alitolee ufafanuzi ili wale ambao pengine hawafahamu, waweze kufahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri tu kwa hili, ni vyema basi, ili kuondoa malalamiko na mambo ambayo yanaweza yakaleta tofauti kwa wanajeshi wetu, basi naomba labda itafutwe njia nyingine ya kuweza kuweka hii tofauti ambayo inaonekana ni kubwa kwa wale askari waliopo rank ya chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nimalizie kusema kwamba siyo jambo la busara na siyo jambo jema kwa Wizara kama ya Ulinzi na Usalama kwamba inapopangiwa bajeti ambayo itasaidia usalama wa nchi hii, vinginevyo leo bajeti inakuwa haipelekwi na inapelekwa ambavyo Bunge halikuidhinisha. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri usimamie hili, kwa sababu na wewe upo Serikalini upo kwenye Baraza la Mawaziri, utie lobbying yako ili uhakikishe kwamba Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kama ilivyopangwa ndivyo inavyopelekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, nasema ahsante kwa kunisikiliza.