Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye mapendekezo ya Mpango wa Bajeti. Nina mambo machache ambayo nataka nichangie. Kwanza ni kwenye kilimo, kwanza nimshukuru sana Waziri kwa mikakati yake ambayo ameanza kuifanya kuhakikisha kwamba kilimo kinakuwa na nafasi katika nchi hii, lakini kuna mambo ambayo tunahitaji kufanya vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2012 nilipata nafasi ya kualikwa Ubalozi wa Marekani alikuwa amekuja, aliyekuwa US Administrator wa USAID alikuwa anaitwa Rajiv Shah na yeye alikuwa na mpango wa kutaka Tanzania iweze kulima zaidi kwa kupitia taasisi moja ambayo tuliianzisha wanaita ile korido ya Kusini. Alitaka tuwe na benki ya ardhi ambapo yeye anaweza akaleta wawekezaji kutoka Marekani waje walime katika eneo kubwa. Akaonesha masikitiko yake, kwamba tangu aanze ku-support mambo ya kilimo, haoni hatua ambayo imeendelea, kwa hiyo alikuwa na mpango wa kujiondoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu ni nini? kwa kuwa tunasema kwamba Tanzania ina asilimia zaidi 60 ya ardhi ambayo inaweza kulimika, tunaweza tukafanya mapinduzi makubwa sana kwenye ardhi, kwa kufanya nini? Lazima Serikali iwe na benki kubwa ya ardhi ambayo imeisajili na iko mikononi mwake. Mwekezaji mkubwa anapokuja hapa anataka kuwekeza tumwonyeshe kwamba tuna benki ya ardhi iko Morogoro tuna hekta 500,000, tuna hekta 100,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua wawekezaji wakubwa kutoka katika mataifa makubwa hawawezi kuja kuchukua heka 1,000 heka 2,000. Tuone katika mipango yetu ya baadaye, tutakuja kufanya nini katika hilo eneo. Maana vinginevyo tutakuwa na ardhi kubwa, lakini hatuwezi kufaidika nayo. Tuwe na mipango ya muda mrefu ya kuwa na Benki ya Ardhi ambayo tutaweza kuvutia wawekezaji kirahisi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwenye kilimo, kwamba tunafahamu mabadiliko yanayoendelea ya hali ya hewa, mvua zimepungua sana. Naomba Serikali isichelewe, tuwe na mpango endelevu wa muda mrefu. Sehemu nyingi za nchi hii zina mabonde mengi mazuri. Tunaweza tukatengeneza haya mabanio kwa bei ndogo sana. Huhitaji kufikiria mradi wa bilioni 10, 20 au 30, unaweza kutengeneza banio kwa bilioni moja na nusu, unafunga upande huu, upande huu, kwenye mkondo wa maji unatengeneza mabwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwa na mabanio mengi katika nchi hii, tutaokoa majanga mengi ambayo yanatokana na wananchi kukosa mahali pa kulima na sasa hivi wananchi wengi wanakimbilia kwenye vyanzo vya maji kwa sababu hawana maji, sasa utafanya nini? Ni lazima wakimbilie tu huko, lakini kama tutatengeneza mabanio mengi, kwa mfano Mkoa wa Iringa of course na mikoa mingine yako maeneo mengi ya namna hiyo. Serikali isichelewe kwenye huo mkakati, vinginevyo itafika mahali tutaanza kulia wakati tutakuwa tumeshachelewa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nione liwe kwenye mpango wa muda mrefu ni namna gani tutaendelea kuboresha mawasiliano vijijini? Unajua biashara nyingi na mifumo mingi sasa hivi ya kibiashara huwezi kuitenganisha na mawasiliano. Mwaka 2012 wakati nasimamia idara ya M-pesa nilipata nafasi ya kuanzisha kitengo cha M-commerce. Sasa kwenye M- commerce kwa maana ya mtandao biashara tuliingiza afya, kilimo na kwenye afya tulitaka kwamba tusajili vituo vyote vya afya, tusajili zahanati zote ambapo kwa kutumia M-commerce, biashara mtandao tulikuwa na uwezo wa kutoa taarifa kutoka katika vituo mbalimbali kusema hapa unaweza kupata dawa hii, dawa hii na mambo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye M-commerce tulikuwa na uwezo kwenye kilimo wa kujua hali ya hewa ya kuweza kujua ni aina gani ya mbegu, wapi upande nini, ardhi inapatikana wapi, msimu wa kulima na mambo kama hayo. Yote hayo yanafanyika kwa njia mtandao, ndio maana ni muhimu sana kuwa na mipango ya baadaye ya kuboresha mitandao ya simu vijijini kwa sababu ni njia ya uchumi na ya kukusanya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyoona sasa hivi ni njia rahisi sana kukusanya mapato kwa kutumia mitandao ya simu. Sasa kama hatujaweza kupeleka mawasiliano huko tutafanyeje? Kwani eneo lingine muhimu sana la kukuza biashara na uchumi wa nchi yetu. Hilo nalo katika mipango yetu ya baadaye hilo tuliweke na tuone tutafanya nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye mazingira sio jambo la kuchezea. Tumekuwa tukisema mara nyingi hapa tulinde mazingira, lakini ukipita katika milima mikubwa hata kama Kitonga pale unakuta moshi unafuka katikati ya mlima. Sasa unajiuliza ni hatua gani kama Serikali tunachukua? Sasa kama moshi unafuka pale maana yake kuna watu wanachoma mikaa, sasa hili ni jambo la hatari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi mikaa mingi sana inatoka katika nchi hii inaenda kuuzwa Burundi, Kenya na misitu yetu inazidi kuharibika. Sasa kwenye hili eneo la utunzaji wa mazingira kwa kweli kuna hao watu wa hizi kampuni ambazo zinajihusisha na kutunza mazingira wanasema miradi ya kuhifadhi mazingira pamoja na bioanuwai. Kwa hiyo kwamba ziko fedha nyingi sana ambazo tunaweza tukazivutia kwa kuziingiza halmashauri zetu, zikatengeneza maandiko mengi, tukahifadhi mazingira, tukapata fedha, tukafanya maendeleo kwenye vijiji vyetu, lakini bado tumetunza mazingira at the same time tumepata pesa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona muda wangu umekwisha, naunga mkono hoja, mambo ni mengi lakini nitachangia kwa njia nyingine, ahsante sana. (Makofi)