Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Leo naelekeza mchango wangu katika maeneo mawili. Maeneo hayo ni suala la Wizara ya Ujenzi na suala la Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama cha Mapinduzi kilitoa Ilani yake ya Uchaguzi yenye kurasa 303 ambayo mimi ni mwanachama wake na ni Mbunge wa Jimbo la Sengerema kupitia Chama cha Mapinduzi. Ilani hii inanipa nafasi ya kulinda yaliyomo kuhakikisha yanatekelezwa ili Chama changu kiwe salama pamoja na mimi. Ilani hii ya uchaguzi Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni miongoni mwa watu walioiandaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa tisa wa Ilani yetu ya Uchaguzi una maneno mazuri sana, unasema katika aya ya 12, “Mapinduzi ya uchumi kwa maendeleo ya watu.” Maneno mengine pale yako hapo. Mheshimiwa Waziri ataenda kuuangalia. Kwa hiyo, mpango wowote atakaokuwa anauandaa lazima basi akaangalie ukurasa huo wa tisa. Tukitoka katika eneo hilo sisi watu aina ya Tabasamu huwa hatukubali, lakini kwa sababu mambo yaliyoelezwa pale yana upana mkubwa katika Taifa hili, Mheshimiwa Waziri atakwenda akaangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naanza mchango wangu. Wizara muhimu sana katika nchi hii kwenye ukuaji wa uchumi ni Wizara ya Ujenzi. Kwa ukubwa wa miradi iliyopo katika Wizara ya Ujenzi tunazo kilomita za lami ambazo zinaunganisha barabara zetu kuu za Taifa, barabara zetu za Mkoa. Wakati huo huo tuko na shughuli za kupanua Bandari, kutengeneza Bandari mpya, kutengeneza reli pamoja na viwanja vya ndege. Kazi hii kubwa inafanywa kwa maono ya Mheshimiwa Rais ambaye anachukua katika tafsiri ya mpango wa miaka mitano. Sasa tukija katika mpango wetu huu wa bajeti yetu, ni kwamba lazima tukaangalie mpango huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ina kazi nyingi. Mchango wangu leo nataka kutoa ushauri tu kwa mamlaka kwamba sasa imefika wakati ili tukatekeleze miradi hii, tunatakiwa tuwe na kitu kinachoitwa contract management tukahakikishe kwamba lazima tukazigawe Wizara hizi zipate ufanisi. Tuwe tuna Wizara ya Uchukuzi, wakati huo huo tuwe na Wizara ya Ujenzi kwa sababu miradi hii iliyopo ili twende 2025 imetekelezwa. Kwa kuwatumia Manaibu Waziri halafu Waziri mmoja ambaye yuko safari, hawa wanashindwa kutoa maamuzi, hili jambo linaweza kutuchelewesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti kama Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ushauri wangu ni kwamba hili tuliangalie. Siyo vibaya kuwa na Wizara kwa sababu matirioni ya fedha yanaenda huko Wizara ya Uchukuzi. Sasa hivi tuna reli, tuna bandari, tunataka tukuze bandari. Leo mzigo unaopokelewa bandarini unasafirishwa, na kusafirishwa kwa njia ya reli ni asilimia mbili, kwa njia ya barabara asilimia 98. Hili ni jambo la hatari sana. Sasa hili tunaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha akaliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Shirika letu la Reli lipewe exemption ya mafuta likajiendeshe lenyewe. Mnakwenda kuwapa exemption wawekezaji wa nje, mnashindwa kulilinda Shirika lenu la Reli mkawapa exemption ya mafuta nao wakaagiza mafuta yakapita hapa zero zero wakapata faida kwa ajili ya kwenda kutanua uchumi unaoelekea huko pembeni kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la nishati kwa miradi iliyopo ya TANESCO na REA. Pamoja na kuwa na miradi mikubwa kama hiyo ya TANESCO, mabwawa ya Mwalimu Nyerere, miradi tuliyonayo zaidi ya ishirini na kitu ambayo inaandaliwa kwa ajili ya kupata umeme wa maji na gesi; lakini ukiangalia usambazaji wa umeme, kuweza kuwafikia wateja, tunaomba Mamlaka kwamba sasa umefikia wakati tuwe na Wizara ya Mafuta na Gesi na tuwe na Wizara ya Nishati ya Umeme (steamer). (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndiyo maombi yangu leo kwa Watawala. Ahsante sana, nakushukuru kwa muda huu.