Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa dhati kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia mpango huu wa maendeleo wa mwaka mmoja. Awali ya yote nami niseme yapo mambo ambayo Serikali imeyaainisha inataka kufanya katika kipindi hiki cha mwaka mmoja lakini jambo kubwa ambalo tunalo pia ni tatizo ni katika hali ya usimamizi wa mipango yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue maneno aliyoyasema Profesa Kitila, lengo la mipango yetu iwe ni kuondoa umaskini. Jambo hili ukiliangalia, nimeisoma hotuba ya Waziri kwa kuirudia, nimesoma mpango wenyewe, unaona kabisa baadhi ya maeneo tunatoka katika kuondoa umaskini. Umaskini kwa maana ya the object poverty bado hatujau-address vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijikite katika Mkoa wa Dodoma. Kwanza naipongeza sana Serikali kwa uamuzi wake wa kuhamia katika Mkoa wa Dodoma, Dodoma sasa imekuwa Jiji na Mji wa Dodoma unakua. Ukilinganisha maisha yaliyopo katika Jiji la Dodoma na nje ya Dodoma kwa maana ya Wilaya zake na wananchi wake bado kuna umaskini wenyewe ule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili nataka niseme, kuna Mheshimiwa Mbunge alisema bado sera zetu tunachanganya, Sera ya Mkoa wa Njombe ya Kilimo inakuwa sawa sawa na Mkoa wa Dodoma, Sera ya Mkoa wa Mbeya inakuwa sawa sawa na Mkoa wa Dodoma. Sera ya Kilimo ya maeneo ambayo mvua inanyesha sana inakuwa the same treated na Dodoma. Sisi tunasikia habari ya ruzuku ya mbolea, kwetu sisi hapa hakuna. Kwa hiyo, Ukiangalia maeneo ya Kanda ya Kati, hebu naiomba Serikali iunde sera mahususi kwa maeneo kame, iwe ni sera ya kilimo katika maeneo kame. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna umaskini mkubwa kwa sababu mvua hainyeshi. Mvua inanyesha mwezi wa kwanza, mwezi wa pili imekatika. Hata hivyo pamoja na mvua hii kunyesha, maji yanayopatikana Dodoma kipindi cha mvua ni mengi. Sasa Serikali tengeni basi hata shilingi bilioni 200 au 500 mtuchimbie bwawa kubwa la uhakika la umwagiliaji. Ile Farqwa imepigwa danadana mpaka leo. Kwa hiyo, umaskini wetu sisi umekuwa mkubwa kwa sababu hatupati mvua ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili Serikali hamlifanyi, inakuja falsafa ya Waziri wa Kilimo kwamba wanaanzisha block farming, zile ni vitone vidogo lakini kwa maana ya kuondoa umaskini katika Kanda ya Kati bado Serikali haijawekeza. Sisi mbegu hatuna, sasa hivi tunatafuta mbegu, ASA (Wakala wa Mbegu) hana mbegu ya kustahimili hapa Dodoma, hatuna. Kwa hiyo, mnavyoongea habari ya ruzuku ya mbolea sisi hapa hatuna ruzuku ya mbegu na hatuna mbegu yenyewe. Mlituletea alizeti mwaka jana yenyewe inarefuka mara tatu, yaani Dodoma bado inashida na Kanda ya Kati bado ina shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema Mkoa wa Singida unalima alizeti, leteni kiwanda kikubwa cha shilingi bilioni 200 au bilioni 300 tuweze kuweka kiwanda cha maana pale, ili tuweze kuzalisha mafuta ya uhakika. Bado hatuja address mkoa huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naliongea hili na nataka niseme, jana ulisema na si umwagiliaji ule ambao unakuja wa kukinga hivi vibwawa vya umwagiliaji vinavyotengenezwa, tunataka umwagiliaji wa matone. Tunataka tulazimishe kwamba kila mkulima awe na heka mbili za umwagiliaji wa mtama ili tuwe na uhakika wa chakula nyumbani. Maji yanatoka mengi niliwahi kusema kuanzia Kongwa shuka yote Mpwapwa ile, njoo kwetu Bahi tuna swamp, ina maji lakini nani wa kufanya utaratibu wa maji yale tuweze kuyatumia? Kwa hiyo, bado kuna tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni katika ufugaji; nchi hii tumeamua kuchunga na sio kufuga, nchi za wenzetu Kusini mwa Afrika wale wanafuga, maana yake mchungaji anataka afuate ng’ombe zake zinakokwenda naye anaenda huko huko, zinampeleka Kusini, Mbeya anaenda huko huko, mashamba ya watu yeye anachunga humo humo, ndio tatizo ambalo bado tuko nalo nchi hii. Wizara ya Ardhi hii iliyopo ukiiuliza mwaka huu imepima mashamba mangapi kwa ajili ya wafugaji? Hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kongwa nayo mnataka muanze kuilimisha alizeti, yaani ile ranchi tena tuibadilishe iwe kwa ajili ya alizeti. Kwa hiyo, bado hau-address. Watu wameacha kulisha nyasi sasa wanalisha mifugo concentrate na mahindi utaweka humo humo na kila kitu, ng’ombe anapata kilo moja kila siku. Sasa umaskini tutauondoa namna ipi? Hata hivyo tukijinasibu tunasema Tanzania ina ng’ombe 45, ng’ombe wa aina gani? Ng’ombe ambao wamekomaa, wameshupaa misuli, hawezi kula mtu kimataifa. Kwa hiyo tu-address sera zetu, ng’ombe kweli tunao, lakini tunachunga karne hii! Bado kuna tatizo, bado sera zetu...

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kingine ambacho tumeshindwa kuelewa, tumepata Awamu ya Kwanza Mwalimu Nyerere alituwekea base nzuri sana zilikuwepo ranchi alizianzisha, kiwanda kile cha Tanganyika Packers na maeneo mengi, lakini kwa nini tunashindwa ku-copy mambo ambayo yamefanyika nchi hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme Serikali ifanye mambo machache ya kuonekana. Zimbabwe walipata shida sana ya kiuchumi, wameyumbishwa, lakini Zimbabwe mwaka jana wameweza kulima ngano ya kuwatosheleza wao na ziada wamepata, nchi ya Zimbabwe, mfano mdogo kabisa. Zimbabwe sasa upande wa Kusini mwa Afrika ndio wanaozalisha maziwa kwa uhakika, laikini wanafanyaje? Walima nyasi na wanalisha pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niseme bado tuna tatizo, kwanza hatuamini katika kuendelea kupitia kilimo. Tunajinasibu kwenye madini, kwenye nini, lakini kilimo ndio kinabeba watu wetu. Asilimia 65 ya Watanzania wapo kwenye kilimo, sasa nilikuwa naangalia hapa kwenye Mpango kwa mfano, kama nilivyosema Kanda ya Kati anasema kwamba kuangalia maeneo ambayo yana tatizo la mabadiliko ya tabianchi. Vinakuja vile viprogramu vidogo vidogo vile vya kimazingira na mnaitaja Bahi kwamba tutawapelekea viprogramu vya kuhifadhi, kupanda miti, tunahitaji mtuondelee umaskini. Huko mnakotupeleka viprogramu ambavyo niseme havina maana muda wake umepita sana. Tuna umaskini mkubwa tunataka kuondoa umaskini kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa dhati kabisa; reli hii imejengwa lakini unaangalia hivi reli hii ni kwa ajili ya kupeleka mizigo Congo tu au na nchi zingine? Sisi tunabeba nini kutoka hapa kwa ajili ya ku-export? Tatizo kama nilivyosema mipango yetu ni mingi, lakini je, mipango ya kuondoa umasikini iko wapi? Ziko nchi zingine ambazo tulikuwa nao sawa, nachukulia kanchi kama Bangladesh kametoka kwenye uchumi wa kilimo sasa kako kwenye uchumi wa viwanda. Hata hivyo asilimia kubwa sasa ya Wabangladesh wengi wako mjini kwa sababu ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu Mawaziri wetu na viongozi wetu wengine jitahidini kwenda kwenye nchi hizi nyingine mkaone wamefanyaje? What is the success story? Hata hivyo nchi tu kama ya Zimbabwe kama nilivyosema wenzetu wamepiga hatua kubwa kwa maana ya kuendeleza kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nataka nimalizie; wenzangu wameongelea habari ya Presidential Delivery Bureau. Malaysia ndio nchi ambayo imefanikiwa kwa kutumia Presidential Delivery Bureau na kwetu hapa kuna shida ya ufuatiliaji. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaenda nje ya nchi, anaingia mikataba, anarudi, lakini nani wa kufuatilia ile mikataba? Utekelezaji wake unasuasua. Tulikuwa na Presidential Delivery Bureau baadhi ya maeneo ambayo yalifanikiwa ni namna ya kuibana Serikali katika quarterly, kwamba kulikuwa na maelekezo ya Rais haya hapa mmeyafanyanje? Sisi nchi hii tunajuana, jambo likishakuja mnaliweka mezani wale wenzetu tulioingia nao mkataba watatuma email na haijibiwi na jambo hilo tumekuwa wazito wa kujibu ndio linakuwa limetoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninachoomba na niungane na wenzangu, tunataka Presidential Delivery Bureau irudi ili kuwe na chombo cha ufuatiliaji na kukumbusha Wizara zetu kwamba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliingia mkataba China, sasa jambo hili Wizara ya Mifugo mmefikia wapi na hatima yake imefikia wapi? (Makofi)

Kwa hiyo, kinachokosekana ni namna gani masuala ambayo viongozi wakuu wa kitaifa aidha wanaingia mikataba wanavyokuwa nje na wakirudi hapa utekelezaji wake na ufuatiliaji wake ni kidogo. Jambo hili sasa linafanya kwamba tunaingia mikataba na watu, utekelezaji ni jambo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ahsante sana. (Makofi)