Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango duniani ni mpango kama ilivyo mipango yote na ina sifa zake. Tumeletewa mpango na tumeusoma na taarifa yake na jinsi ulivyo. Mpango huu una chanzo chake ambacho ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi; na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ni mkataba kati ya Watanzania na Serikali wanayoenda kuiunda na mambo ambayo wanategemea kwamba Serikali itakwenda kuwafanyia. Serikali ni Mkandarasi ambaye amepewa tenda na CCM kutekeleza yale ambayo iliahidi kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mipango iweze kutekelezwa lazima kuwe na malengo. Malengo tumejiwekea na tunayaona yapo kwenye mpango, lakini Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inatambua kabisa kwamba, Mpango huu ndio unakwenda kutekelezwa katika ule Mpango wa Miaka Mitano ambayo tumeupitisha, ambao ndio unakwenda kutimiza dira ya maendeleo ya Taifa ambao tumeanza kutekeleza tangu mwaka 2000 mpaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi, ninachoona shida kwenye Mpango wetu ile kutokuwa unasomana na ule Mpango Mkuu wa Miaka Mitano kwa sababu malengo yake kama tunasema kwamba, mpango wote unatakiwa kuwa na malengo yanayopimika, yanayokuwa na muda maalum, yanayoweza kufikika, maana yake kuna sifa za malengo. Mpango huu kuna mambo ambayo ukiangalia katika miradi yetu ya maendeleo tumeweka malengo kwamba tutakuwa na miradi ya maendeleo ambayo itakwenda kuchochea ukuaji wa uchumi ambayo ni ujenzi labda wa barabara. Barabara hizi zinakwenda kufungua fursa za kukua kwa uchumi, halafu barabara zile hazijawekewa muda lini zinakwenda kukamilika. Maana yake ni kwamba, yale malengo hayasaidii mpango huu wa muda mfupi kufikia mpango wa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tuna barabara inajengwa kuanzia Itono – Ludewa kwenda Manda, kilometa 211. Serikali inasema barabara hii imeanza ujenzi na ujue tupo kwenye utekelezaji wa Mpango huu wa Miaka Mitano, maana yake tuko mwaka wa tatu. Tumeanza ujenzi wa kilometa 50 kuanzia Lusitu mpaka Mawengi na umekamilika kwa asilimia 95. Sasa swali langu ni hili hapa, huyu mkandarasi kapewa kazi ya kujenga barabara hii kwenye Ilani ya CCM yenye urefu wa kilometa 211. Anatupa kukamilika kwa kipisi cha kilometa 50 kwa asilimia 95 ina maana gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo hajatuambia hizi asilimia 161 zinazobaki atakamilisha katika hii miaka miwili iliyobaki. Hapa ndipo kunakuwa na tatizo la mpango na tusipowekana sawa maana yake ni kwamba, tutakuwa tunaweka hii mipango halafu haitimii. Sasa tumeshamaliza dira ya maendeleo ya miaka 25 na Serikali ya CCM inaitambua hiyo na imeeleza kwenye ilani kwamba, itaisimamia Serikali yake kuhakikisha inaandaa mpango mwingine wa dira ya miaka mingine 25, maana yake itakwenda mpaka 2050.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najaribu kuuliza kama hatutawekeana malengo kwamba, ninyi mwaka huu mkiingia katika hii barabara jengeni kilometa 40, mwaka unaofuata tutajenga kilometa 42, mwaka unaofuata tutajenga kilometa 42, mpaka miaka mitano tufikishe zile kilometa 211 hii mipango yetu tutakuwa tunafikiaje? Kama watu watakuja tu ofisini, sisi tumejenga kwa asilimia 95 kilometa 50, ndizo ulizotumwa? Wewe umetumwa kutengeneza kilometa 211, tuambie hiyo asilimia uliyojenga katika hiyo kilometa 211, usituambie katika hizo ulizoamua wewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni sawa na unakwenda kumkagua mkandarasi mradi, halafu anakwambia nimekamilisha kwa asilimia 90 kipande hiki, wakati wewe unajua kipande kile ni kidogo sicho ulichompa. Kwa hiyo, tunataka mpango unaokuja sasa uwe una time ya kutuhakikishia kwamba, hizi barabara tunazosema zinafungua uchumi wa Taifa letu katika miaka mitano zinaishaje? Kwa mwaka wa kwanza zinajengwa kilometa ngapi, ngapi, kwa miaka inayofuata mpaka tutakapofikia kwenye zile ambazo tunajua kabisa kwamba, ndani ya miaka mitano tutakuwa tumekamilisha ile barabara yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaendelea kujenga hizi barabara kwa kilometa moja, kilometa mbili, tunafungua uchumi. Kwa mfano, barabara ya Iringa MR mpaka Itunundu kilometa 70, kila siku wanajenga kilometa moja moja miaka 70 watakua lini kwenda kwenye uchumi wa kukua kwa asilimia nane na watu watakuwa answerable vipi? Yaani unamuulizaje mtu kwamba, wewe Wizara yako ya Uchukuzi imefanya kazi nzuri kama hukumwekea lengo kwamba, lazima barabara hizi zinazofungua uchumi ujenge kwa asilimia 40 au 50?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndio kwenye shida ya mpango. Kwa hiyo, mipango tunayokuja nayo huku mbele ifanyiwe mapinduzi tuambiwe barabara hii uliyosema unaijenga kwa miaka mitano umejenga kilometa ngapi? Nimejenga kilometa 150; hizi zilizobaki unamaliza ndani ya hii miaka miwili iliyobaki na kama hujamaliza kwa nini? Hapo ndipo tutakuwa tunakwenda sawa na mipango mingine yote duniani, lakini tukienda hivi itakuwa kama ile michezo ya kuchezea vile viberiti chekundu cheusi, chekundu cheusi, kila mtu atakuja atatuambia hapa sisi tumejenga kilometa mbili kwa asilimia 90. Kilometa mbili kwa asilimia 90 out of kilometa ngapi? Haya ndio maswali ya kujiuliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kikubwa ambacho kipo kwenye huu Mpango; pamoja na kwamba tunakusanya fedha, udhibiti wa fedha zetu umeendelea kuwa weak. Tumeelekeza sana kelele nyingi kwamba, Serikali za Mitaa ndiko fedha nyingi zinakopotea, lakini iko miradi hapa ambayo imewekwa na Wabunge wengine wameisema na yenyewe inapoteza tu fedha za Serikali, haina tija. Katika karne hii kuipatia taasisi fedha, unaipatia taasisi fedha bilioni moja, inakwenda kufanya ubunifu na ndio wanasema inakwenda kuwa ni kitivo cha kubuni zana za kilimo vijijini kama CARMATEC, unaipatia bilioni moja, inakuja imekutengenezea mikokoteni ya kuvutwa na ng’ombe nane. Imetengeneza sijui mashine za kubangua korosho mbili, huu ni utani wa uwekezaji kwa watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu ambao tunatumia gharama kubwa tumewekeza, tunawafundisha, tunawapa mafunzo, especially vijana. Tunawapeleka katika majeshi, kwa mfano JKT, wanafanya kazi kubwa sana ya kuwafundisha wale vijana uzalishaji mali, uhodari, ushujaa na wale wanaweza kufanya kazi popote. Wao JKT lengo lao la kuanzisha si kwamba kutoa ajira kwa vijana, lakini sisi Serikali ya CCM imetutuma kuandaa ajira milioni nane. Hawa vijana wanaangaliwa vipi? Wanaachwa vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, unamwachaje mtu ambaye umesham-train anaweza kufanya kazi, anaweza kulima, anaweza kutengeneza, anaweza kupambana na mazingira ya Kitanzania, kulala popote akaweza kulima, akafanya nini, ukamuacha kama kijana wako, kama nguvukazi, kumwendeleza na wakati umeshatumia gharama kubwa ya uwekezaji kwake. The same applies tunafanya kwa watu tunaowasomesha, tunafanya kwa vijana ambao wanamaliza vyuo vikuu, hatuna mpango kabambe kwamba, vijana wamemaliza, hawa wana elimu hii, vijana hawa wamemaliza SUA wana elimu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunahangaika mpaka vijijini; China waliamua kwa pamoja wakasema sasa tunachukua vijana milioni tano, tunawapeleka vijijini na wengine tutawapeleka nje ya dunia wakajifunze namna ya kufanya kazi. Hawa nao waende vijijini kule, wakakae na wanakijiji, waangalie wanafanya nini, halafu watupatie njia mbadala za kufanya mambo wanayofanya kisasa zaidi. Sisi tuna mpango gani kwa vijana wetu na hizi milioni nane? Hizi ajira milioni nane tulizopewa na chama? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rasilimali watu na rasilimali vitu hatuweki vizuri. Leo tuna LNG, mradi wa gesi, taarifa imekuja hapa kwamba, mradi ule wa gesi tumejenga barabara kuzungushia eneo lile, ndio kazi zilizofikiwa kwa bilioni nne karibu na. Tumezungushia barabara kwenye ule mradi, halafu mambo mengine yaliyofanyika kwenye mradi ule tunaendelea na utafiti wa kisayansi, tunaendelea na utafiti wa kuweka mipango, sasa kipi kinaanza kati ya kuku na yai? Unaanzaje kujenga barabara na kuzungushia eneo ambalo bado unaendelea kufanyia utafiti wa kisayansi, hujajua kwamba, utatakiwa uweke mitambo ya kiasi gani? Kwenye hizo barabara hiyo mitambo itapita au haitapita?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante. Kengele ya pili.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba Mheshimiwa Waziri akija hii miradi mingine ambayo haina tija aitoe na taasisi ambazo zinachukua hela hazina tija zitolewe. Ahsante. (Makofi)