Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nitumie nafasi hii kumpongeza Waziri wa Fedha, kwa mpango wake mzuri aliotuletea kwa mustakabali mzima wa Taifa letu. Nitumie nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan. Pia nimpongeze kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar ndugu yetu Hussen Ali Hassan Mwinyi kwa ushirikiano wao wa pamoja katika kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee, na nitajielekeza kwenye sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi. Naipongeza Serikali kwa kuwekeza fedha nyingi katika sekta hizi za uzalishaji ambazo lengo lake ni kuimarisha sekta hizi kwa manufaa ya Watanzania. Ni vyema sasa uwekezaji huu mkubwa unaowekezwa na nchi yetu tuone matokeo makubwa pia ya uwekezaji huu kwa sababu ni fedha nyingi sana zimewekezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inategemea sana usalama, hasa usalama wa nchi kwa maana ya mipaka, usalama wa ndani ya nchi kwa maana ya wananchi na mali zao, lakini hapo hapo inategemea usalama wa nchi kwa maana ya chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuelekeze zaidi kuwekeza kwenye NFRA, kwa ajili ya kujiwekea usalama wa chakula ndani ya nchi pindi tutakapofikwa na majanga, maafa na maswaibu mbalimbali ndani ya nchi yetu ambayo yanasababishwa na mambo mengi ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi na mambo ya dunia yanayojitokeza. Kwa hiyo kwenye NFRA tukiwekeza vya kutosha ule usalama wa nchi utakamilika, kwa maana ya mipaka, raia, mali zao na usalama wa matumbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea hapo hapo kwenye sekta ya kilimo, tumeona kwenye mipango kwamba kuna mipango inafanywa kwa ajili ya uwekezaji kwenye sekta ya kilimo, kuimarisha tafiti, kuimarisha mambo ya mbegu bora. Pia kwenye suala la mbolea kuna watafiti wetu wamegundua kilimo ambacho kinaitwa kilimo hai na kilimo hifadhi. Hiki kilimo hai na kilimo hifadhi kinakwenda kulinda na kuhifadhi ardhi na udongo wa nchi yetu na pia kinatoa matunda bora ambayo hayana kemikali zozote za viwandani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaunge mkono watafiti hawa ili elimu hii isambae kwa wananchi wetu waweze kulima bila kutegemea mbolea ambazo wakati mwingine zinakwama kufika kwa wakati, wakajitengenezea wenyewe mbolea zao na mambo yao mengine ya ughani kwa kutumia kilimo hifadhi na kilimo hai. Tumeona matunda yanayolimwa kutokana na kilimo hai na kilimo hifadhi ni matunda mazuri na yana soko kubwa katika soko la dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa kilimo, nashauri tujielekeze sasa kwenye mpango wa muda mfupi na mpango wa muda mrefu, kwa baadhi ya mazao. Tuna uhaba wa sukari, mafuta ya kula na ngano ndani ya nchi. Ni vyema sasa tukajipangia mipango kumaliza tatizo japo kuna zao moja la sukari, ama ngano, ama mafuta; ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, miwili au mitatu. Tuache tabia ya kuagiza nje mazao haya kwa sababu ardhi tunayo ya kutosha, wataalam tunao, fedha tushapata, mitaji kama hii kwenye kilimo. Basi tuseme ndani ya miaka mitatu au minne tutaachana na kuagiza sukari ama unga wa ngano, ama mafuta ya kula. Tujielekeze hivyo tuzalishe ndani ya nchi, tujitosheleze, pia tuweze kupata soko la nje kwa mazao tutakayozalisha ndani ya nchi huku tukiendelea na mazao yetu mengine ya biashara yakiwemo mazao ya bustani, mbogamboga na mazao mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitishwa sana kwa taarifa ya Kamati kuona kwamba Serikali imewekeza fedha nyingi kununua vitendea kazi vya Maafisa Ugani ikiwemo pikipiki, lakini kumbe kuna baadhi ya pikipiki zile hazifanyi kazi iliyokusudiwa eti kwa tatizo tu la kukosa mafuta. Tunawekeza fedha nyingi kwa Maafisa Ugani, tumewapa vitendea kazi, Serikali imetoa ili wawafikie wakulima lakini kweli inashindikana mafuta ya kuweza kuwafikia wakulima wale. Kamati imeelekeza kwamba halmashauri zitenge fedha kwa ajili ya kugharamia mafuta. Lakini haya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, kuna kodi inachukuliwa pale kwa halmashauri sasa si ndio hapo pa kuwekeza ili ile kodi iwe kubwa zaidi tuongeze mapato kwa sababu kilimo kikikua na mapato yanakua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kwenye sekta ya uvuvi tumeona hapa kuna nchi zinaendeshwa uvuvi katika dunia. Tujielekeze zaidi kwenye uvuvi wa Bahari Kuu kama mipango ya Serikali na pia tiliimarishe Shirika la TAFICO na ZAFICO kwa sababu uvuvi wa Bahari Kuu ni chombo cha Muungano. Kwa hiyo kwa upande wa TAFICO zinawekezwa fedha lakini bajeti haikidhi kwa sababu TAFICO inahitaji uwekezaji mkubwa, kwa maana ya kuwekeza fedha pale TAFICO kulifufua. Shirika linahitaji gati na mitambo ya baridi ya kuhifadhia Samaki, shirika linahitaji kila kitu kwa maana na hata baadhi ya majengo tayari yameanza kumomonyoka kwakuwa yanaliwa na dahari. Pale uwekezaji wake ni mkubwa hivyo ni lazima tuwekeze fedha za kutosha ili kulifufua hili shirika kwa haraka, kwa sababu ni muda mrefu sasa tunazungumzia TAFICO lakini TAFICO yenyewe bado haijaanza kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye samaki hatuhitaji mbolea, ugani wala kupalilia. Samaki tunachokitaka ni kuhifadhi matumbawe na kuweka mazingira ya kudhibiti uvuvi haramu, tuvue, hakuna hasara nyingine pale inapayotikana, Mwenyezi Mungu katujalia ile baraka ya Samaki tunawaacha, na Samaki wanatembea kokote duniani, yeyote anaweza akamvua, huwezi kumwekea mipaka. kwamba mimi ninamzuia mpaka shirika langu la TAFICO liwe salama ndipo tuweze kufanya kazi ya kuvua Samaki. TAFICO ikifufuliwa ikapewa mtaji wa kutosha tutaanza kuvuna rasilimali ya bahari kwa wingi zaidi na bila ya gharama kubwa. Gharama yetu ni uwekezaji kwenye TAFICO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nagusia sekta ya maji ambayo imezungumzwa sana, na mimi nashauri kwenye jambo moja. Kuna gharama kubwa ya uendeshaji wa maji katika visima kwa kutumia nishati ya umeme. Ni vyema sasa Serikali ikaona namna ya kupunguza kodi au ongezeko la thamani (VAT) au kutoa ushuru mwingine kuhakikisha hizi mashine za solar za kupandishia maji na kuendesha mitambo ya maji ili kupunguza gharama kubwa kwa wananchi kule vijijini ya kutumia nishati ya umeme…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante…

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naunga mkono hoja.