Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. CAN.RTD Ali Khamis Masoud

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mfenesini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Napenda kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia na kunipa pumzi ya kusimama hapa pia niwashukuru wapigakura wa Jimbo langu la Mfenesini kwa kunipa nafasi hii adhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi kama lilivyo jina lake, ina majukumu ya kuhakikisha usalama wa Taifa letu kwa mipaka yake yote ya angani na ardhini. Wizara hii kwa kipindi kirefu sana, kwa uzoefu nilionao imekuwa na matatizo mengi mno na mengi yanasababishwa na ukosefu wa fedha ya kutosha ya kuendesha vifaa pamoja na huduma za wanajeshi.
Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia ulinzi kama ulinzi, lazima vitu viwili vyote vihusihwe kwa pamoja, ukihudumia askari/wapiganaji, basi lazima pia uhakikishe unahudumia vifaa vyao pia wanavyovitumia kufanyia kazi za ulinzi. Usiweke vipaumbele kwa watu halafu vifaa ukavidharau, uzoefu mkubwa nilionao katika vifaa vyetu vya kijeshi vya Tanzania, tuna vifaa vizuri vingi tu, vya kisasa kabisa, lakini bado hatujavipa uzito wa kuvihudumia ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, vifaa vya nchi za wenzetu, nchi nyingi duniani, vifaa vyao vya kijeshi vinachakaa, vinaharibika kwa sababu ya kutumika sana kwa mazoezi na mambo kadhaa, lakini vifaa vyetu Tanzania vingi vinaharibika kwa kukaa bila kufanya kazi. Vifaa hivi ni kama binadamu, binadamu ukiwa unalala tu na kuamka, kula na kulala, siku utakayotoka pale baada ya miezi mitatu ukiambiwa ukimbie kilometa moja tu huwezi kuondoka na vifaa vyote vya kijeshi ndiyo vinatakiwa viwe katika mfumo huo, lazima viwe vinatumika, vinafanya kazi, magari wanaya-run, ndege zinarushwa kwa mazoezi na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukitaka kurusha ndege utaambiwa mafuta hakuna, ukitaka kufanya hiki utaambiwa mafuta hakuna. Baada ya muda fulani, usije ukategemea vimetokea vita una vifaa vya kutosha, unavyo vifaa vya kutosha lakini havina uwezo mkubwa wa kufanya kazi unayoitegemea. Niiombe sana Serikali iwe inatoa kipaumbele cha hali ya juu katika kuhakikisha kwamba vifaa vyetu vya kijeshi vinatunzwa ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine nizungumzie suala lililozungumzwa sana na baadhi ya Waheshimiwa hapa Bungeni, hasa la Jeshi la Akiba. Ni kweli wanajeshi wastaafu nao ni moja ya wanajeshi wanaotegemewa endapo ikitokea dharura ya janga la vita ndani ya nchi. Wengi walishaomba kuongezewa pensheni, lakini ninaomba pia Serikali iangalie utaratibu mpya wa kuhakikisha wananjeshi hawa sasa wanawalipa kila mwezi badala ya miezi mitatu mitatu, siyo rahisi, wengi tunaishi kwa kubahatisha kule mitaani, kukopa na kadhalika, siyo rahisi mtu leo akaenda kukopa halafu akamlipe mfanyabiashara baada ya miezi mitatu! Ninaomba sana Serikali iliangalie suala hili na ilipe kipaumbele chake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wengi wamekuwa wakisimama hapa, wanapenda sana, hawafurahi bila kuizungumza Zanzibar. Mimi niseme tu, wanajeshi kama wanajeshi, anaposimama Mheshimiwa Mbunge hapa Bungeni halafu akasema vifaru vinatembea, hivi anakijua kifaru. Vifaru vinatembea mjini, wanajeshi wanafanya mazoezi, wanajeshi wakafanye mazoezi mitaani! Mtu anapokuja hapa azungumze kitu halisi, azungumze kitu anachokifahamu. Najua huyu Mheshimiwa hakijui kifaru haijui APC, hajui chochote, ndiyo maana anazungumza kifaru kinatembea mtaani, siyo kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapozungumza hapa tusipotoshe wananchi, tusiwapotoshe wananchi tukawaambia kwamba majeshi sasa yameanza kuingia mitaani. Mimi ninachofahamu, nilikuwa mwanajeshi pia, ninachokifahamu Jeshi linaweza kuingia mtaani kwa kitu kimoja tu, kumetokea labda kuna kitu kimeonekana kimeingizwa kwenye mtaa na Jeshi likafanya quadrant search, basi! Lakini Jeshi kama Jeshi, mazoezi yote ya Jeshi yanafanywa porini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unapotuambia vifaru vimeingia mitaani, binafsi sikuelewi na najua na wewe pia hujui kitu ndiyo maana ukasema hivyo. Lazima tukubali Jeshi letu bado linafanya kazi kwa nidhamu na kwa kulingana na sheria na Katiba ya nchi. Tunachotakiwa kufanya hapa tuhakikishe Jeshi letu linahudumiwa, linapatiwa uwezo wa kutosha wa kununua vifaa vyao kwa wakati wowote wawe tayari endapo tumevamiwa ama limetokea janga lolote wawe tayari na uwezo wa kufanya lile jukumu walilopewa na Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana na napenda kusema wapo Waheshimiwa wanasimama hapa Bungeni, mishipa kabisa inawatoka, anakwambia kule Zanzibar uchaguzi haukuwa, mtu kazungumza lugha zote hapa leo, nimeshangaa anapozungumza mapinduzi, huyu katoka wapi, katoka shimoni leo, mapinduzi hayajui? Huyu naomba akatafsiri nini maana ya mapinduzi halafu aje atuambie, siyo vizuri watu wazima wenye heshima, Wabunge, kuja ndani ya Bunge hapa mkatoa lugha za ajabu, tabia hii siipendi, naomba irekebishwe kabisa. Watu tuje hapa tufanye kilichotuleta kulisaidia Taifa letu kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mbunge mmoja alisimama hapa akasema ile kesi kule Zanzibar haijaisha bwana, wasifikiri imekwisha. Mimi namwambia hivi, kesi ya Zanzibar tuliimaliza Januari 12, 1964. Kama kuna mtu hapa au taasisi yoyote leo inayoweza kumuondoa Dkt. Shein, basi ifanye lakini nakwambia Dkt. Shein atakuwa Rais wa Zanzibar kwa miaka mitano na hakuna mtu wa kumuondoa.
Mheshimiwa Spika, mtu anayesema yeye Mzanzibari mimi ninamwambia nimezaliwa. Sisi Wazanzibar tunasema hivi, Dkt. Shein hakuna atakayemuondoa na huyo anayesema kuna kesi na alete na sisi tupo tayari kufa na nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, najua watu wengine yanawaudhi kwa sababu hawana uchungu na Zanzibar. Mtu yeyote mwenye uchungu na Zanzibar na anayeijua Zanzibar, maneno mengine yanayosemwa hapa yanauma sana. Nataka niseme, wakati tukiwa nje hatujawa Wabunge wengine hapa, tulipokuwa tunaona vikao vya Bunge vinavyopita, mambo yanayofanyika humu ndani, watu wengi kule nje yanawakera sana, yapo mambo yanawakera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilipofika ndani ya Bunge tukajikuta tupo watu wengi wapya humu ndani ya Bunge nikafikiri labda safari hii tutakuwa salama, lakini kumbe bado tunarudi kulekule. Niseme tu na niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, yaliyopita tumeshamaliza, anayesema kwamba ule siyo uchaguzi…
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)
SPIKA: Utulivu Bungeni! Mheshimiwa nakulinda endelea!
MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Spika, anayesema ule uchaguzi si halali sisi tunasema ni halali, anayesema Rais wa Zanzibar siyo halali namwambia atakaa pale kwa miaka mitano na hakuna wa kumwondoa. Kilichotuleta hapa tukifanye kwa ajili ya Taifa lakini malumbano mengine yasiyokuwa na maana tusiyalete hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, najua watu wanachukia sana…
SPIKA: Jamani, Kanali anaongea halafu raia mnapigapiga kelele! Huyu ni Kanali wa Jeshi. Endelea Mheshimiwa Kanali! (Kicheko)
MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ninayoyasema kuna watu yanawakera, lakini tukubali tu kwamba sote tunaipenda nchi yetu, tuna wajibu wa kuhakikisha usalama wa nchi yetu unadumishwa. Niwaombe wenzangu Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania bado muendelee kudumisha nidhamu iliyokuwepo Jeshini, tutekeleze majukumu yetu kwa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na mimi naunga mkono hoja.