Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia Mpango wa Maendeleo wa 2022/2023. Kabla ya hapo, naomba kuchukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya na niwaombe tu Watanzania wenzangu tuendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kawaida Rais anaanza kujiandaa kugombea miaka kumi au miaka mitano, lakini Mheshimiwa wetu, Mheshimiwa Rais hajajiandaa na amekabidhiwa nchi na nchi inakwenda vizuri. Kwa hiyo, ni jambo zuri sana la kumtia moyo pamoja na kumpongeza, hakujiandaa, lakini ameweza kufanya mambo yote ambayo yanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kitendo ambacho kinaendelea kwenye jimbo langu, ambapo wanafanya tathmini, lakini naomba, ikumbukwe kwamba, hii tathmini inayofanyika hili zoezi limechukua muda mrefu sana tangu mwaka 1997. Kwa hiyo, naomba Wizara watakapomaliza kufanya tathmini, hawa watu walipwe. Naiomba Serikali kabisa iwalipe hawa watu isije ikawafanyia tathmini halafu ikawaacha tu hivyohivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kuchangia Mpango wa Maendeleo; ukurasa wa 78, Biashara na Uwekezaji. Tukiongelea Mkoa wa Dar-es-Salaam sehemu yoyote ambako tunahitaji Serikali uchumi ukue ni lazima kuwe na usalama. Mkoa wetu wa Dar-es-Salaam kwa muda mrefu umekuwa na matukio mbalimbali, hasa matukio ya panya road na kuna sehemu mikoa mingine inawezekana ikawa na mambo hayo, lakini sisi tuna hao panya road.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali katika mpango huu wa 2022/2023, kuwe na mpango maalum ambao utakuja kuwafanya wananchi ambao wanakaa Mkoa wa Dar-es-Salaam au na majiji mengine, mfano kama Mbeya, Arusha, Mwanza, waangalie watafanya mpango gani ili kuona kwamba, hawa vijana kwa sababu, vijana wengi ambao wanashiriki kwenye haya mambo ya panya road au na wizi mwingine mbalimbali ni vijana wengi ambao hawana kazi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri aje na mpango ambao unaweza kuwasaidia vijana wetu waweze kupata kazi waachane na haya mambo ya panya road. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na Mkoa wa Dar-es-Salaam pia, hapo hapo. Mkoa wetu wa Dar-es-Salaam mwaka 2018 kwa sababu, sehemu yoyote ambayo tunahitaji uchumi ukue ni lazima tuwe na usalama. Mwaka 2018 kulikuwa kuna mchakato unaendelea kwamba, wanataka waanze sasa kuweka kamera za barabarani na wenzetu wa Zanzibar tayari wameshaweka. Hili jambo limeshapita siku nyingi, lakini leo ni 2022 hizi kamera hakuna, wala hakuna kitu chochote ambacho kinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wetu wa Dar Es Salaam kama kungekuwa na usalama wa kutosha ina maana wafanyabiashara wengi wangekuwa wanaweza kufanya biashara zao masaa 24 lakini sasa hivi ukiangalia Mkoa wa Dar es Salaam, mtu ambaye anafanya biashara yake ya M-Pesa biashara tu ya kawaida ni lazima Saa 12 awe amefunga kwa sababu usalama ni mdogo. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iingize kwenye mpango huu wa maendeleo ni jinsi gani itakuja na mpango wa usalama katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia Mkoa wa Dar es Salaam ni Mkoa ambao ni lazima utofautishwe na Mikoa mingine, kwa sababu huwezi kusema inafanana na Mkoa wa Iringa au Mkoa wa Dodoma. Dar es Salaam ndiyo unaoongezea Serikali mapato. Kipato cha Taifa kwa asilimia Themanini kinatoka Dar Es Salaam. Kwa hiyo ni lazima tunaposema Dar es Salaam ni Mkoa ambao kwanza una watu wengi na ndiyo Mkoa ambao umeongoza katika sensa kwa watu wengi. Ni Mkoa ambao una watu waliotoka sehemu mbalimbali, ukiachilia hilo ndiyo Mkoa ambao una airport kubwa ya Kimataifa, Bandari na Reli. Kwa hiyo, tunaomba katika mchakato huu wa maendeleo Mkoa wa Dar es Salaam utengenezewe page yake tofauti kutokana na unyeti wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Dar es salaam ni Mkoa ambao una mambo mengi na una biashara kubwa na wafanyabiashara wengi. Sisi hatulimi, watu wetu wanategemea kufanyabiashara ndogo ndogo, biashara kubwa pamoja na wafanyakazi. Kwa hiyo, tunapouangalia Mkoa wa Dar es Salaam tuungalie kwa mambo tofauti tusije tukauweka uwe sawa na Mkoa kama wa Mkoa wa Singida au Mkoa wa Dodoma, ni Mkoa tofauti na naomba uwe na mambo yake tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 104, umeongelea ardhi na makazi. Mkoa wa Dar Es Salaam mvua zikinyesha…

MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kumpa taarifa Mheshimiwa mzungumzaji kwenye suala la usalama na comfortability ya Wawekezaji ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Pia suala la fire ni tatizo kubwa sana. Dar es Salaam wanayo magari matatu tu ambayo yana umri sawa na umri wangu zaidi ya miaka 30 hadi leo. Ipo haja Serikali kuweza kuweka mkakati madhubuti wa kuweza kuongeza magari ya fire.

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante taarifa naipokea. Nilikuwa naongelea kuhusu suala la ardhi na makazi ukurasa 103 hadi 104. Mkoa wa Dar es Salaam tukienda kwenye masuala ya miundombinu labda na Mkoa wa Mbeya na Arusha. Dar es Salaam kutokana na geografia ya Mkoa wenyewe ulivyo na wingi wa watu, ukienda kwenye masuala ya makazi naomba Mheshimiwa Waziri aangalie ni jinsi gani watakuja na mkakati katika suala la miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe mwenyewe ni mkazi wa Dar es Salaam unajua kwamba hakuna Mwekezaji atakuja wakati wa masika Dar es Salaam, pale Mnazi mmoja pamejaa maji ndiyo anatoka airport mvua ambayo imenyesha saa moja, aje aseme kwamba hii ni sehemu nzuri ambayo mtu anaweza kuwekeza haiwezekani! Kwa hiyo, ni sehemu ambayo mvua ikinyesha ni taabu na isiponyesha ni taabu. Kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Waziri aangalie ni jinsi gani kutakuwa na mkakati wa kuiwezesha Dar Es Salaam iweze kupendeza, hata mvua ikinyesha isionekane imenyesha na hata isiponyesha ionekane haijanyesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili linahusiana na suala la DMDP, mwaka jana hapa tulikaa tukaongea suala la DMDP ni jinsi gani Serikali inaenda kujenga Bonde la Mto Msimbazi, tukaambiwa kwamba huu mradi unaanza mwezi Machi, lakini mpaka leo huu mradi haujaanza na wala huo mpango sijajua umefikia wapi, tumeongea hapa mara nyingi tu kuhusiana na masuala ya DMDP. Kwa hiyo, mimi nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri kwamba hili suala la DMDP na miundombinu ya Dar es Salaam asilifananishe na Mikoa mingine, kwa sababu hata hizi fedha zitakazokopwa kwa Dar es Salaam kurudishwa haitachukua muda kama Mikoa mingi ukizingatia Dar es Salaam wafanyabiashara ni wengi, pia watumiaji barabara ni wengi na magari mengi ambayo yanapita, kwa hiyo ni rahisi sana kurudisha hizi pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri amalize huo mchakato ambayo walikuwa nayo kwa ajili ya hiyo miradi ya DMDP ili Bonde la Mto Msimbazi liweze kujengwa, pia barabara za DMDP ambazo tulikuwa tumezipanga tangu mwaka jana kwamba sasa zinaenda kujengwa barabara za DMDP ziweze kujengwa, maana tangu tumeongea mpaka sasa hivi hakuna kitu chochote ambacho kinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)