Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Mimi nitachangia mambo mawili. Jambo la kwanza ni jambo la ATCL na pili litakuwa ni jambo la kilimo na mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais Mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwa sababu mpango wa kununua ndege tano tayari kuna malipo ya fedha ameshayafanya na ndege tano zinategemea kuingia nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nizungumzie ATCL kwa maana ni nini inatakiwa tusaidie kwenye mpango na kama ambavyo kamati imeshauri. ATCL ina ndege 11 lakini tuna changamoto kubwa sana katika uendeshaji wa Shirika letu la Ndege la ATCL. Changamoto yetu ya kwanza ni kwenye suala la gharama za tiketi. Gharama zetu za tiketi kwenye Shirika la Ndege zimekuwa ziko juu sana, kiwango ambacho hadi Mbunge anafikiria kusafiri kwa ndege anaona ni bora asafiri kwa gari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaweza kutolea mfano wa gharama ya tiketi ya ndege kutoka Katavi kuelekea Dar es Salaam. Unazungumzai shilingi za Kitanzania 800,000, 600,000, 700,000. Nauli ambayo unaweza ukaitumia kusafiri kuelekea Rwanda na ukaelekea na mataifa mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe kwenye mpango wa Serikali waweze kuisaidia ATCL na kupunguza gharama za uendeshaji, kwa maana ya hizi tiketi. Tunajua ATCL inakodi ndege kutoka TGFA (Tanzania Government Flight Authority), ambapo analipa zaidi ya dola 1,500,000 kila mwezi kwa kukodishiwa ndege. Kwa hiyo ni vyema ATCL ikapewa jukumu la kuendesha hizi ndege in full capacity ili hizi gharama ziweze kushuka chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Mtanzania ukisimama ukamwambia ATCL nauli zake ziko sawa wakati katika nchi hii na Taifa hili tulishaona fastjet a private company, a private entity ilishawahi ku-operate na akarusha airbus kwa 100,000, 90,000, 150,000 lakini leo hii ATCL ambayo ni ndege ya Serikali ni kodi za watanzania ina viwanja nchi hii, inapaki nchi hii bado gharama zake za tiketi ziko juu. Kwa hiyo ninaomba kwenye mpango wa Serikali ione ni namna gani ya kuisaidia ATCL. Kwenye ATCL pia, hii ndege Watanzania wanavyoenda kulala saa tatu usiku na ndege zinaenda kulala kwa sababu hazina viwanja vya kuruka vyenye mataa. Kwa hiyo niombe ATCL isaidiwe kutoka kwenye TAA (Tanzania Aviation Authority) waweke mataa kwenye viwanja vingi ili ndege zi-operate zaidi usiku kuliko ku- operate mchana. Haiwezekani ukaona ndege 11 tukienda kulala na zenyewe zinaenda kulala (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kwenye Mpango wa Serikali, ni fedha chache, ni fedha kidogo kulisaidia Taifa hili mchana watu wafanye kazi, mtu asiwaze flight. Ni jambo linahuzunisha sana. Ukienda Bukoba Kiwanja cha Ndege usiku hakitui, ukija Dodoma unaambiwa Kiwanja cha Ndega usiku hakitui, ukienda Tabora Kiwanja cha Ndege usiku hakitui. Ni vyema tukaondoka kwenye hili ombwe tuisaidie ATCL. (Makofi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili tunaomba ATCL pia wasaidiwe control tower ziongezeke. Moja ya changamoto kubwa ambayo ATCL inaipata, Mfano Bukoba hakuna control tower ya ndege wanatumia ya Mwanza. Ni vyema ATCL, TAA wakaisaidia ATCL iweze kuongeza Tower kuongozewa ndege kwenye maeneo tofautitofauti kama pale Tabora. Kwa hiyo ninakuomba sana shirika hili la ndege ili liwe na msaada kwa nchi yetu, liwe msaada kwa Watanzania na watu waendelee kupanda ndege kama walivyokuwa wanapanda kwenye Fastjet, wajisikie amani kwenye Taifa hili. saidieni hili shirika, geuzeni madeni yaliyoko kuwa mtaji ili shirika lisonge mbele, wasitumie sehemu ya tiketi kuwa ndiyo sehemu ya kutengeneza faida. Oncourse lazima watengeneze faida lakini hatuhitaji muda wote wawe wana-maximize super profit kwa kuwaumiza Watanzania ambao walitegemea kodi zao ziweze kuwasaidia kwa ajili ya Taifa lao, huu ni mchango wangu kwenye suala la ATCL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo mengine ni kwenye mpango wa mambo ya kilimo. Tunakubaliana kabisa tuna hekta zaidi ya milioni 29 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Naomba nisema, hatujaona mpango mkakati wa Serikali wa kusaidia kuboresha mazingira. Leo hii tunazungumzia mvua hakuna, hali ya hewa imebadilika. Lakini hatuzungumzii upandaji wa miti kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tunaenda kuzungumzia umwagiliaji, maji mtatoa wapi kama mvua hakuna? Maana yake ni kwamba lazima tupande miti, ni lazima tuhamasishe Watanzania kupanda miti. Otherwise tuseme kwamba tunamsubiri Mheshimiwa Rais aanzishe kampeni ya kupanda miti nchini, wakati Rais anahangaika kutafuta fedha kuna mambo kama Taifa, tuamue tukiwa ndani, Rais ashtukie watu tunafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano mmoja. Tunajenga Bwawa la Mwalimu Nyerere, mimi ni Mbunge wa Makete, Jimbo la Makete ndilo linalo-offer maji kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere. Tunamwaga maji kuelekea Mbarali, yanatoka Mbarali yanaelekea Ruaha, yatoka Ruaha yanaingia Rufiji kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, lakini hakuna mti hata mmoja mliohamasisha, then mnategemea mkifukuza wananchi kutoka kwenye mita 60 ndiyo itakuwa solution ya kutunza vyanzo vya maji? siyo sahihi. Lazima tuhamasishe upandaji wa miti kwenye Taifa letu. Anzeni kampeni hii mapema, huu ni mpango, tengeni bajeti, na fedha ziko nyingi. Kusafisha Coco beach si usafi wa mazingira tu ni kazi ya Halmashauri ya Kinondoni. Kamam Taifa lazima tuwe na mpango mkakati kwa ajili Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili liende sambamba na timu ya Mawaziri nane walivyoenda Mbarali, wamesema kuanzia leo vijiji 48 vilivyoko karibu na Hifadhi ya Ruaha viondoke. Nataka kuita hii as a Mbarali crisis, kwa nini? leo hii unaenda kuondoa vijiji 48 kwa sababu tu unasema wako karibu na vyanzo vya maji na wananchi hao kupitia Ilani ya CCM tuliwaambia kwamba tutali-solve hilo tatizo kwa kukaa nao mezani tukiwaambia wanambarali kwa sababu nyie mnalilisha Taifa, kwa mwaka jana tu Mbarali imelisha ekari tani 600,000 za mchele…

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunawaambia watu wa Mbarali vijiji 48 waweze kuondoka…

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na nimpe taarifa mzungumzaji kwamba, hata kule KIA - KADCO inataka kufuta kijiji kimoja chenye ekari 15,000 na vijiji vingine viwili kwa madai kwamba wako kwenye eneo la Kiwanja cha Ndege na kiwanja hiki kinadai eneo lake ni kilomita za mraba 110,000. Lakini ukubwa wake ni kilomita za mraba 12…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Pallangyo sasa unachangia naona.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa yake. Mbarali vijiji 48 unaviambia viondoke kwenye hifadhi ya maji. Wananchi wamesema tuko tayari kukaa mita 100 ili maji yaendelee kupita tunajua uhitaji huo. Lakini nizungumze hivi, leo hii tunazungumzia mgao wa umeme kwa sababu ya kupungua maji, leo hii tunazungumzia mgao wa maji kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi. Leo hii na kesho tunaenda kwenye Dinner table ya nchi yetu kwa mgao wa chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbarali anayelisha tani 600,000 za mchele kwa mwaka unamwambia leo akusanye virago aondoke. Huyu Mbarali ana viwanda visivyopungua 30, huyu Mbarali ana ajira za Watanzania zisizopungua 100,000, huyu Mbarali unayemzungumzia ana makazi ya watu na watoto wako pale, huyu Mbarali amekutwa na GN ya mwaka 2008 wakati wao walikuwepo toka mwaka 1972. Huyu Mbarali unayemzungumzia ni Mtanzania mwenzangu, ana familia na watoto anaosomesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawaziri nane wanaoenda kuzunguka kwenye kijiji hiki wanatumia ripoti za maeneo yale ndio wanaenda kuamulia. Tunawaomba msitengeneze vidonda mnakokwenda, nendeni mkaponye matatizo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Mheshimiwa Mwigulu umesaini mikataba 15 Mbarali yenye thamani ya shilingi bilioni 54 ya umwagiliaji, mmesema yakajengwe mabwawa Mbarali, Waziri wako ameenda kufuta hivyo vijiji 48, mpo mnaleta hapa mpango wa kwamba nyie mmesaini mikataba ya umwagiliaji 48…

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati kule mmenda kufuta…

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaenda kujenga wapi hayo mabwawa?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sanga kuna taarifa.

T A A R I F A

MHE. ASKF. JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa mzungumzaji kwamba kile kitendo cha Mheshimiwa Waziri wa Fedha kusaini mikataba ya kuwasaidia wananchi, halafu mwingine akaja kukifuta ndicho nachoita kukosa mipango ya muda mrefu. (Makofi)

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa. Waziri wa Fedha nachokwambia mikataba 15 uliyoisaini yenye thamani ya shilingi bilioni 54 Kamati ya Mawaziri nane imeenda kufuta hilo eneo unalokwenda kujenga hayo mabwawa. Kwa hiyo ujue kwamba Serikali nyie wenyewe hamuelewani sasa sisi wananchi tutaelewanaje sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Chama cha Mapinduzi iliwaambia wale wananchi kuwa tutawalinda maslahi yenu, tutalinda haki zenu, tutalinda kwa sababu Mto Ruaha umesimama nyie mlikuwepo. Leo hii Kamati ya Mawaziri nane inaenda kufuta. We are going to the dinner table of this country na watu wenye njaa. Wabunge hatuwezi tukakaa hapa tukajadiliana wakati wananchi wetu wako under crisis kule. Wabunge hatuwezi tukajadiliana hapa sisi tumeshiba, wenzetu kule wanafukuzwa wanazalisha tani 600,000 kwa maslahi ya watu binafsi. (Makofi)