Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Emmanuel Peter Cherehani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na Mheshimiwa Naibu Spika wetu. Kwanza nikumshukuru Mwenyezi Mungu Muumba wa Mbingu na Dunia kwa uhai na niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa fedha nyingi ambazo anatupa hasa kwenye Majimbo yetu. Pia, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Kassim kwa kazi nzuri aliyoifanya juzi kukimbia na kuwahi kwa wahanga wenzetu waliopata tatizo pale Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ninampongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa kutoa mapendekezo kwa kijana wetu Majaliwa aliyeokoa wananchi wenzetu ya kwenda kwenye mafunzo ya Kijeshi ya Uokoaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tu kidogo kwamba tumekuwa tukiwapa support vijana hasa wanapo - support kwenye matukio mazito kama hayo, ninaiomba Wizara ya Mambo ya Ndani iendelee kutoa mafunzo kwa wavuvi wote nchini hasa walioko kwenye bahari zetu ili wajue namna nzuri ya kuokoa hasa katika kipindi kigumu cha majanga kwenye bahari, mito na maziwa yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye hoja yangu, naendelea ku-declare interest yangu kwenye suala la kilimo. Kilimo chetu bado kinategemea mvua. Mvua leo hii tunakaribia miaka miwili na huu ni mwaka wa tatu tunapata mvua chini ya wastani, kitu ambacho ni hatari sana kwenye uchumi wa Taifa letu. Kwenye taarifa ya Waziri wa fedha Ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, kwanza nimpongeze kwa Bajeti nzuri aliyotupa kwenye kilimo kutoka Bilioni 254 sasa wakulima tumepata kwa mara ya kwanza toka uhuru Bilioni 90, na pointi, hongera sana, sisi kazi yetu tuendelee kukuombea sana kwa Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu kubwa ambayo mimi najikita ni kwenye Kilimo cha Umwagiliaji. Kuna mradi mkubwa sana wa maji kwenye nchi hii wa Ziwa Victoria. Mradi huu unatoka katika Mkoa wa Mwanza eneo la Iherere lakini bomba hili limepita zaidi ya kilometa 245 kwenda Tabora Mjini. Bomba hili linapita Solwa, Misugwi, Kahama, limeenda Shinyanga Mjini, limeenda Kishapu. Sasa hivi limeenda Nzega, Tabora na Igunga lakini tuulizane, bomba hili kote linakopita linapita kwenye mashamba ya wananchi ya wakulima wetu ambao wanategemea mvua, Serikali na Wizara yetu ya Kilimo pamoja na Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali na Wizara yetu ya Kilimo pamoja na Wizara ya Maji wanashindwaje kukaa pamoja kwenye maeneo ambako linapita bomba wakachimba Mabwawa makubwa ya maji wakachepusha maji kupitia kwenye bomba hili. Wakulima wetu walioko Jirani na bomba hili waendeshe kilimo cha umwagiliaji. Leo hii niseme tu hata kwa Ndugu yangu Waziri wa Kilimo pale bomba linapita kwenye barabara nzuri kwenye mbuga ya wakulima wanaolima mpunga lakini ukipita pale unashuhudia kabisa wakulima wa mpunga unakauka hakuna maji, lakini pale limepita bomba kubwa la maji. Kwa nini wananchi hawa wasichimbiwe Mabwawa makubwa ili maji ya umwagiliaji waweze kulima kiangazi, waweze kulima kipindi chochote, leo hii wanategemea mvua? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwenye mpango wako huu hatujaona kujikita kwenye mradi mkubwa wa Mabwawa ya umwagiliaji, maji haya ni mengi sana, lakini wananchi hawa wanaopelekewa maji haya ya kunywa wakati mwingine wanashindwa kulipia bill kwa sababu…

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimependa mchango wa Mheshimiwa Cherehani jirani yangu. Wiki iliyopita nafikiri siku tatu zilizopita, nilichangia kuhusu design ya miradi ya kimkakati katika nchi yetu. Hapa nauona msisitizo mwingine kwamba tunapo-design miradi yetu tuiangalie miradi strategically and comprehensively ili kutibu matatizo mengi zaidi kuliko kutibu tatizo moja. Kwa hivyo tatizo letu la kukosa mvua na kupungua kwa chakula lingeweza kutatuliwa na mradi wa kupeleka maji kutoka Ziwa Victoria, kwa kuweka hata mabomba mawili moja ya maji ambayo yako treated na moja la maji ambayo hayako treated. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante Doktari. Mheshimiwa Cherehani

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante taarifa hii naipokea kwa sababu kweli maeneo haya hata kama ni Kamati ya Wizara ya Maji itakapotembelea maeneo haya nenda pale Solwa kwa Ndugu yangu Mheshimiwa Ahmed, wananchi wale unakuta hata bwawa la kunyweshea mifugo yao hakuna, lakini bomba la maji limepita, nenda pale Kishapu, hakuna hata eneo la kunyweshea, zao la pamba linapokosa mvua linazidi kupukutika na kushuka uzalishaji lakini hakuna bwawa lililochimbwa kwa ajili ya kuchepusha maji haya wananchi waweze kufaidika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda pale Msalala kwa Ndugu yangu Mheshimiwa Kassim Idd hakuna Bwawa lolote lililochimbwa kwa ajili ya kunyweshea maji, leo ninaenda Igunga kwa Ndugu yangu Mheshimiwa Ngassa eneo hili lote lilitakiwa liwe na maji, mabwawa yachimbwe yajazwe maji, lakini leo hii hata kwenye tumbaku ambako mwaka huu tuna uzalishaji wa zaidi ya tani 140,000, Serikali na wakulima wetu wanaelekea kupata zaidi ya Bilioni 600 lakini hakuna mabwawa, sasa mbegu zinakauka lakini angalia fedha zinazoingia. Mimi ningeendelea kuiomba Serikali mahali ambako tunakoeleza uzalishaji mkubwa waweke nguvu kuhakikisha Taifa linapata mapato makubwa tuweze kumsaidia Mheshimiwa Rais.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tutamsaidiaje Mheshimiwa Rais? Mheshimiwa Rais anatutafutia fedha, anatupa fedha nyingi lakini fedha nyingi tunashindwaje kuzipeleka mahali ambako tunaweza tukapata fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mwananchi tu wa kawaida leo anashindwa kulipia bill ya maji kwa sababu hana vyanzo vya kuweza kupata mapato. Madhara yake pamoja na kumpelekea maji ya Ziwa Victoria anaamua kwenda kutafuta maji ya kisima lakini tungempelekea bwawa akalima bustani yake, akalima mahindi yake vizuri, akalima mpunga wake vizuri, tayari pale atauza kwa muda wowote halafu ataenda kulipia bill zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye tumbaku tunatarajia kuzalisha tumbaku nyingi sana mwaka huu, lakini tunayo changamoto moja na bahati nzuri nimemwona Waziri wangu wa Kilimo na Naibu wako hapa. Tuna mfumo wa makundi ya watu kumi kwenye sekta ya tumbaku. Makundi haya yanafaidisha sana wakulima wazembe lakini pia wakulima waliopo serious na kilimo wanaenda kudumbukia, kwa sababu makundi ya watu kumi mpaka walipe deni lao ndipo waweze kulipwa fedha na wengine. Sasa unakuta kwenye kikundi cha watu kumi kuna wakulima watano wamelaza deni lao. Sasa wanaposhindwa kulipa hawa watano inabidi wawalipie madeni yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwaenyekiti, kwenye Chama cha Ushirika chenye watu 20 watu 15 wamelaza madeni chama kimekufa na hawawezi kukopesheka. Mimi niendelee kushauri kwenye eneo hili, kwa sababu Serikali yetu iko makini na nampongeza Mheshimiwa Waziri yuko vizuri. Tungeomba sasa wakulima wenyewe mmoja mmoja uje utaratibu mzuri waweze kukopeshwa wenyewe kulingana na dhamana zao ili tuweze kuongeza uchumi kwenye maeneo yetu mbalimbali na wakulima waweze kupata mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tuende kwenye Bodi ya Tumbaku. Bodi ya Tumbaku ndiyo inayosimamia uzalishaji wote huu. Uzalishaji ambao ni Mabilioni ya fedha yanaenda kwenye Serikali yetu lakini niombe waendelee kuipelekea fedha. Bodi ya Tumbaku bado ni changamoto, niseme tu hata Mkurugenzi wa Bodi hii ya Tumbaku hana gari. Anasubiria gari inayoenda field ndiyo aje afanye shughuki zake. Niombe bodi hizi za mazao ambazo ziko kwenye mazao ya kimkakati ziweze kupewa fedha za kutosha kuweza kuwa hudumia wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ahsante sana.