Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Miaka Mitano, mpango wa mwaka mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hali ya uchumi, ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei, maendeleo ya watu na vitu vingine. Hakuna Serikali ambayo inataka kuona watu wake wanateseka, haipo, kwa jinsi ninavyofahamu. Hakuna Serikali ambayo imejidhatiti kusimamia wananchi wake na kuhakikisha kwamba wanaishi katika mazingira mazuri na wanajikwamua kwenye umaskini ambayo inafurahia wananchi wake kupitia katika mfumuko wa bei uliokithiri, uchumi unaokua kwa kasi ya kinyonga na maendeleo ya watu yasiyo maendeleo ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi umekua kwa asilimia 0.4 kwa mujibu wa mpango huu na hotuba ya Mheshimiwa Waziri, lakini mfumuko wa bei bado umeendelea kuishi nje ya malengo ya Serikali ambayo ni kwamba mfumuko wa bei ulikuwa ubaki stable kwenye asilimia 3.0 mpaka 5.0. Tumeshuhudia malengo ya Serikali yakiwa mbali kabisa na hali ilivyo kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumzia maendeleo ya watu maana yake tunategemea kuona watu wakijikwamua kwenye lindi la umaskini. Nimesema mwanzo kwamba haipo Serikali ambayo inatamani watu wake wateseke, kwa hiyo mimi naamini, pamoja na jitihada zote zinazofanywa na Serikali, lengo lao ni kuhakikisha kwamba wanawatengenezea Watanzania mazingira mazuri ya kuishi ili uchumi wa Mtanzania mmoja mmoja ukiwa mzuri Serikali kazi yake ni kukusanya kodi. Kwa hiyo ninaamini nia njema ipo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunajikwamua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zipo sababu nyingi sana zimetajwa kwamba kwa nini tuna changamoto hizi, kwa nini bado mfumuko wa bei hauko stable kwa sababu kuna athari za vitu vingine ambavyo vimetajwa, masuala ya kupanda kwa bei ya mafuta, mbolea na nini. Kuna sababu nyingi ambazo sidhani kama tuna haja ya kujielekeza huko kwa sasa kwa sababu Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri na Kamati wamefafanua vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Deni la Taifa; kwa hali isiyo ya kawaida Deni la Taifa kutoka mwezi Aprili mwaka huu mpaka mwezi Juni mwaka huu, 2022, limeongezeka kwa kiasi cha shilingi trilioni 2.119 kutoka shilingi trilioni 69.44 Aprili mpaka shilingi trilioni 71.559.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunajua kwamba kuhakikisha kwamba tuna-fund miradi ya maendeleo ili tu-move, it’s well and good. Na kwamba Deni la Taifa linahimilika, kwa sababu siku zote tumekuwa tunasema kwamba Deni la Taifa bado linahimilika, Deni la Serikali bado ni himilivu na nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani kwa hapa tulipofika na tunapokwenda, kwenye shilingi trilioni 71.559 ninaomba Bunge hili liweke ukomo wa uhimilivu wa Deni la Taifa. Kwa sababu ni kweli tunakopa kwa ajili ya ku- fund kwa sababu hakuna mtu anakopa akafanye starehe, ndiyo maana nilisema kwamba hakuna Serikali inayotaka wananchi wake wateseke.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa binti yangu, Mheshimiwa Nusrat, kwamba Serikali inakopa kwa factors za kiuchumi, siyo factors za kuwekewa limit. Factors za kiuchumi za nchi ndizo zinazotoa direction ya Serikali kuwa na uwezo wa kukopa ama la. Tukisema Bunge liweke ceiling ya Serikali kukopa tutakuwa tunakwenda kinyume na principles za kiuchumi katika masuala mazima yanayowezesha mambo ya ukopaji katika masuala ya kuendesha Serikali duniani.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nusrat.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenendo wa biashara ya bidhaa na huduma kwenye Taifa letu; tumesema nia yetu ni njema, hatutaki wananchi wetu wateseke na tunataka pato la ndani wananchi walifaidi wenyewe. Lakini kwa sasa hivi hali ilivyo tunaendelea kulipa madeni, it’s well and good kwa sababu tunaona flagship projects na nini, lakini aim si ni kujenga?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sikilizeni tushauri; kwanza kuhusu mwenendo wa biashara na huduma ndani na nje. Taarifa ya Mheshimiwa Waziri na Mpango inatueleza kwamba tumekuwa tuna-import zaidi kuliko ku- export. It’s well and good kwa sababu kwenye taarifa kunaonekana kuna ongezeko la kutoa bidhaa nje (ku- export) kwa asilimia 25, na kwamba tumetoka dola za Kimarekani milioni 8,811 mwezi Juni mwaka jana mpaka dola za Kimarekani milioni 11,116.7.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna progress, lakini ukweli ni kwamba sekta ya utalii – na niwapongeze sana kwa jitihaa zilizofanyika – sekta ya utalii ndiyo imekuza hii; lakini ongezeko la ku-import ni kubwa kwa asilimia 39, limeongezeka kwa asilimia 39 zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana mwezi Juni kwenye ku-import tulikuwa tume-import kwa takribani dola za Kimarekani milioni 9,841 mpaka dola za Kimarekani milioni 13,715, sawasawa na ongezeko la asilimia 39. Tuki-export kidogo tuka-import zaidi tunajikosesha fedha za kigeni, maana na sisi Tanzania mazingira yetu pia ya biashara yanakuwa siyo mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe kwenye mpango huu Serikali ijielekeze zaidi katika kutengeneza mazingira yetu ya bidhaa za ndani ili tupunguze ku- import. Lakini pia kutengeneza mazingira ya kwetu ili tu- export zaidi; na hii ni principle ya kawaida tu ya biashara, wala haihitaji Ph.D, ni suala tu la kawaida, uki-export zaidi unapata mapato ndani zaidi, uki-import zaidi unatumia mapato yako ya ndani zaidi kupeleka kwa watu wengine, kwa hiyo ni biashara tu ya kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe, kwa sababu tunatafuta ubunifu na mbinu zaidi kwa ajili ya kupata mapato kwenye nchi kwa sababu lengo si ni kuhakikisha kwamba Watanzania hawateseki? Sijaona. Nimeangalia mpango mzima, na nimeangalia kwenye hotuba nzima ya Mheshimiwa Waziri, sijaona kitu kinaitwa carbon marketing.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kutokana na mabadiliko makubwa ya tabianchi, nchi zenye misitu ikiwemo Tanzania sasa hivi zinafanya biashara ya carbon. Kwa hiyo nilitegemea kiwe ni chanzo kipya cha ubunifu cha kibiashara kwa ajili ya kuongeza pato kwenye nchi. Kwa hiyo niombe Mheshimiwa Waziri atusaidie kuelewa mpango wa Serikali kwenye masuala ya kufanya biashara ya carbon. Najua anajua carbon marketing.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sehemu ya tatu na ya mwisho; sekta ya madini. Taarifa za Taasisi ya Jiolojia na Utafiti Tanzania (GST) inatuambia kwamba Tanzania tuna takribani critical minerals 24, kwenye utafiti ambao umefanywa na Taasisi ya Jiolojia na Madini Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Profesa amezungumza, lakini nafikiri tusaidiane kuelewa; ukisoma hotuba nzima ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 14 ambao amezungumza yeye kwenye hotuba masuala ya madini, ukurasa wa 68 ambao amezungumza masuala ya madini kwenye mpango, ukurasa wa 24 amezungumza masuala ya madini kwenye mpango, hakuna kitu kinaitwa critical minerals.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tofauti kati ya critical minerals na strategic minerals. Critical minerals ni madini muhimu, strategic minerals ni madini ya kimkakati. Madini ya kimkakati maana yake ni madini ya kusaidia kukuza uchumi. Madini ya kimkakati ndiyo tumeyazoea tangu mimi nasoma; kuna gold, tanzanite, aluminum na madini mengine ya kawaida ambayo yanatusaidia kukuza uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia inazungumza mabadiliko ya tabianchi. Wakati tunatoka kwenye mhamo wa nishati (energy transition) kutoka kwenye nishati ambazo ni chafu kwenda kwenye nishati safi tunategemea kuna soko kubwa la madini muhimu. Madini muhimu ni pamoja na graphite, lithium, helium, nickel, cobalt na mengine, yako 24. Waheshimiwa Wabunge waende kwenye websites za masuala ya energy, kuna International Energy Agency, wana website yao, ukiangalia tu kwenye tablet yako unapata information nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa masikitiko makubwa sana, kwanza Sheria ya Madini ya mwaka 2009 haizungumzi chochote kuhusiana na mhamo wa nishati (energy transition) kuelekea kwenye critical minerals. Na ni well and good kwa sababu tunataka tupate pato la nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Geological Survey of Tanzania, Tanzania ni ya tano kwa kuzalisha graphite lakini ina reserve ya tani milioni 18 ya graphite kweye ardhi. Na naomba niwaambie kwamba GST haina teknolojia ambayo ingetusaidia kujua zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nina uhakika kabisa kuna uwezekano mkubwa sana hiki tunachokisema inawezekana Tanzania ni ya kwanza duniani kwa sababu hatuna teknolojia. Kwa hii teknolojia yetu ya kawaida tu imesababisha tujue kwamba kuna tani milioni 18 kwenye ardhi. Sasa hapo hatujazungumza nickel, hatujazungumza rare earth minerals, kwa sababu hizi iPhones, Waheshimiwa wana iPhones hapa, iPhones zinatengenezwa na aina ya madini ambayo ni critical, yanaitwa rare earth elements.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia mhamo (transition) wa nishati unatusababisha twende kwenye nishati ya jua, twende kwenye nishati ya upepo. Hizo critical minerals 24 nilizosema Tanzania zipo kwa mujibu wa GST, zinatusaidia kutengeneza solar panels, wind turbines – Kiingereza hapo kidogo, lakini sasa hatuna Kiswahili chake – mitambo ya kuzalisha umeme wa jua, mitambo ya kuzalisha umeme wa upepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia inazungumza electric cars, kuna madini ambayo yanatengeneza electric car batteries. Kwa hiyo tuache kuzungumza kuhusu gold…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)