Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa maoni yangu kwenye mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya Serikali na hatimae mapendekezo ya mpango wa maendeleo ya Taifa wa mwaka 2023/2024. Kwa sababu ya muda tu na kwa sababu ninayo mengi ambayo ningetamani na mimi nishauri ili yaweze kuingizwa kwenye utekelezaji wa mpango na hatimaye yaingizwe kwenye bajeti ili tutakapokuwa tunajadili mwakani basi mengi ambayo yanawagusa wananchi kwa ujumla wake Waziri wa Fedha pamoja na Serikali kwa ujumla wake, wawe wameyaweka kwenye bajeti ili angalao yalete ahueni kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza mchango wangu nichukue nafasi hii kwanza kupitia kidogo taarifa ya Mheshimiwa Waziri kuhusiana na mtikisiko wa uchumi wa kidunia. Pamoja na mambo mengine ametaja sababu mbili ambazo ndiyo zinasababisha sasa mtikisiko wa kiuchumi kidunia, moja ni vita inayoendelea Ukraine, lakini la pili amezungumzia mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka tu nishauri kwenye hili la mabadiliko ya tabianchi ukisoma vizuri taarifa ya Mheshimiwa Waziri, niombe tu alipe mkazo kwa sababu, mabadiliko ya tabianchi sit u kwamba, yanakwenda kuathiri uchumi wa nchi, lakini pia yana madhara katika afya ya kibinadamu kwa ujumla wake. Kwa hiyo, nilikuwa natamani sana lipewe kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanadamu tunaishi kutokana na ikolojia inayotuzunguka, lakini sote tunakubaliana kwamba, ikolojia ile imeanza kuathirika kutokana na shughili nyingi za kibinadamu, miti imeanza kukatwa na maeneo mengi sana yameanza kuathirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, hivi ninavyozungumza nchi wanachama wa Jumuiya ya Dunia wako Misri wanajadili juu ya mabadiliko ya tabianchi. Ningeomba sana Mheshimiwa Waziri uone namna ya kulijazilisha vizuri, namna ambavyo Serikali tumejipanga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kabla ya mwaka 2030 na kuendelea ili angalao isije ikafika huko tukakutana na changamozo hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema ya kwangu yatakuwa yale ambayo yanawagusa wananchi ambayo ningetamani yaingizwe kwenye bajeti. Kwanza, Mheshimiwa Waziri ningetamani sana bajeti ya mwakani pamoja na mpango wa bajeti hiyo ambao unakuja mwakani ili angalau tuweze kuujadili na kuupitisha, ni vema Wizara yako ingejipanga namna ya kuboresha na kuongeza mapato ya Halmashauri, hasa Halmashauri ambazo ziko pembezoni mwa mipaka ya nchi, lakini Halmashauri ambazo mapato yake yako chini ya bilioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetamani mpango wako na bajeti ujikite sana tutakapokuja kujadili uone namna ambavyo unakwenda kuzisaidia hizi Halmashauri ili angalao zisiendelee kutegemea vyanzo vilevile kila mwaka. Mfano nitatoa, zipo Halmashauri ambazo zinategemea vyanzo viwili tu vya mapato. Ningeshauri sana kwenye Wizara yako kwa sababu huwa mnatenga fedha za miradi ya kimkakati na nimekuwa nilisema sana hili kwa Mheshimiwa Waziri. Muone hizi fedha za miradi ya kimkakati mpeleke kwenye Halmashauri ambazo mapato yake yako chini ya bilioni moja, lakini mapato yake hayako stable. Tungetamani kwenye bajeti ya mwakani inayokuja tupate angalao kujua fedha za miradi ya kimkakati zinazokwenda kwenye Halmashauri ambazo mapato yake hayako stable mnakwenda kuzisaidiaje? Kwa sababu, huko mbele haya mapato mwisho wake utafika yatakwisha, maana yake hizi Halmashauri hazitaweza kujiendesha. Kwa hiyo, ningetamani kwenye mpango na bajeti yako Mheshimiwa Waziri uone namna ya kulifanya hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kwenye mpango na bajeti tutakayokuja kuijadili mwakani, Mheshimiwa Waziri kwa sababu tunaishi na watu, ipo fedha ambayo inatolewa na Halmashauri ya asilimia 10 kwa ajili ya akinamama, vijana na watoto. Fedha hizi zinatolewa kulingana na kiasi ambacho Halmashauri zinakusanya. Zipo Halmashauri ambazo kiwango cha fedha wanachokusanya ni kidogo sana kiasi kwamba, kinachokwenda kwa vijana kwa ajili ya mikopo na akinamama hakitoshelezi. Ningetamani kupitia mpango wako uje utuambie nini mnajiandaa, hasa Halmashauri ambazo zinakusanya fedha kidogo kwa ujumla kwa vijana wa watu 10 unakuta mfano fedha wanayopewa ni Milioni Moja au Milioni Mbili ambayo haitoshi hata kujiendesha kwenye kikundi hicho ambacho kipo. Mnao mpango gani kama Wizara na Serikali kusaidia hizi Halmashauri ili fedha inayokwenda angalao kikundi kimoja kikipata fedha kiweze ku-sustain?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili katika hilo ningetamani kwenye mpango na bajeti yako Mheshimiwa Waziri, ni vyema ukaona namna ya kupitia utaratibu na sheria za mfumo huu wote ambao unatoa fedha zinazokwenda kwenye miradi kwenye hivi vikundi vya vijana, akinamama na walemavu. Ningetamani mpango wako na bajeti hiyo ije iseme namna mlivyojipanga kama Serikali kupitia upya namna ya utoaji wa fedha, namna ya kupata vile vikundi, namna ya pesa zinavyopata kwa sababu, hawa ndiyo wananchi ambao wametuzunguka huko, hawa ndiyo wangetamani kwenye bajeti ya mwakani waone namna ambavyo inakwenda kushughulika na changamoto zao kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika hilo ningetamani kwenye mpango na bajeti yako Mheshimiwa Waziri utuambie ni namna gani mnakwenda kujenga kama Serikali, barabara za lami kwenye maeneo ambayo yanaunganisha kati ya nchi na nchi, kwenye maeneo ya miradi ya kimkakati ambayo kimsingi yanaweza yakainua uchumi wa nchi, pia kwenye Mkoa na Mkoa? Ningetamani kwenye bajeti yako pamoja na mapendekezo utakayokujanayo mwakani ili mtuambie kwenye Halmashuri ambazo kimsingi zinagusana nchi na nchi angalao wapate kidogo barabara za lami ili ku- sustain na kuibua uchumi wa nchi ile pamoja na zile Halmashauri na hatimaye ninyi kama Serikali naamini mtakuwa mmepata mapato mengi sana, ningetamani hilo pia Mheshimiwa Waziri uje utwambie ni namna gani ambavyo mmejipanga? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Waziri katika hilo, uone namna ambavyo unaweza ukapitia Sheria za Manunuzi na utekelezaji wa maeneo mbalimbali. Sheria za Manunuzi ambazo ziko TARURA, RUWASA na maeneo mengine kwa sababu, naweza nikakutolea mfano Mheshimiwa Waziri; tumepitisha bajeti mwezi wa Saba, leo tunazungumza ni mwezi wa Novemba tunakwenda mwezi wa Disemba, bajeti ya fedha, fedha za mipango tulizopitisha kutekelezwa kuanzia mwezi wa Saba mpaka leo hakuna Mkandarasi site, hakuna kazi, maana yake ni nini? Hizi Taasisi zote bado zipo kwenye utaratibu wa kimanunuzi. Ningetamani kupitia ofisi yako upande wa fiscal policy au upande ambao wanahusika na mambo nya sera na sheria uone ni wapi ambapo tunakwama? Ni kwa nini tunapitisha bajeti mwezi Julai, lakini utekelezaji wake unakwenda zaidi ya miezi Minne katika utekelezaji wake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake ni kwamba, hata unaposema umeona kwenye bajeti yako wanasema angalao mwakani kuanzia Januari mpaka Juni, tunategemea uchumi wetu ukue kwa asilimia 5.3. Unaweza usikue kwa sababu, inawezekana mvua hizi zinazokuja barabara nyingi zitakuwa hazijatengenezwa. Hivi ninavyozungumza na wewe maeneo mengi umeme bado haujafika sawasawa, ninavyozungumza na wewe maeneo mengi bado miradi ya maji tuliyopitisha bajeti haijaanza kutekelezwa, hawa wote ukiwauliza ni utaratibu wa kimanunuzi ambao kimsingi ndiyo unasababisha hizi shughuli ziweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetamani kwenye mpango na bajeti ili mje muone namna gani ambavyo mnaweza mkapitia, ili fedha inapotoka ya Serikali inakwenda moja kwa moja kwa mwananchi na isichukue muda mrefu na ikaleta maswali mengi sana kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningetamani nilizungumze na tulilisema hapa Mheshimiwa Waziri na umelisema kwenye hotuba yako ni pamoja na usimamizi wa fedha mnazopeleka. Umesema kwenye hotuba yako kwamba, utaimarisha na kupeleka fedha kuimarisha simamizi hizi, ofisi ndogondogo za Ukaguzi za CAG ambazo ziko kwenye Halmashauri. Mimi nikuongezee lingine, pamoja na mipango yako na bajeti tafuta namna ambavyo utaongeza usimamizi kwa kuwalipa fedha Wasimamizi Wakuu wa fedha za miradi huko ni Madiwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye mpango na bajeti inayokuja mwakani ningetamani na penyewe uone namna hawa wasimamizi wa kwanza ambao leo unapeleka zaidi ya Bilioni Mbili kwenye Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, msimamizi wa kwanza wa kuhakikisha fedha inatumika ni Diwani. Sasa lazima angalao kwa kuwa unaandaa fedha za kwenda kulipa namna ya usimamizi - CAG, angalia namna ambavyo unaweza ukaweka mpango mkakati mzuri wa kuwalipa wale Madiwani ili kazi zao ziweze kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Waziri ni kuhusiana na ulinzi na usalama. Mimi niko kule Rorya na maeneo mengine, ningetamani sana kwenye mpango wa Serikali pamoja na bajeti muone namna ambavyo mnaweza mkapeleka fedha kwenye maeneo ya Maziwa na Bahari Kuu kuimarisha ulinzi na usalama wa maeneo yale. Niliwahi kutoa mfano hapa tunalinda sana maeneo ya maliasili na ndiyo maana tumeweka Jeshi Usu, ukienda kwenye madini kule wanalinda, lakini ukienda maeneo ya Maziwa na Baharini huku hakuna ulinzi wa rasilimali samaki na hakuna ulinzi wa wavuvi wanaovua maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano na niliwahi kusema hapa, ukienda Rorya leo wavuvi kila siku wanalia kupigwa na kunyang’anywa nyavu zao, kupigwa na kunyang’anywa samaki, hakuna ulinzi. Kinachohitajika kule ni feasibility ya ulinzi angalao Askari waweze kuonekana, lakini hawapo. Nini ambacho ningeshauri katika hili kwenye maeneo ya Maziwa na Bahari, kwenye mpango wako na kwenye bajeti Mheshimiwa Waziri, uone namna unaweza kupeleka fedha kwa mfano maeneo ya Kanda ya Ziwa yote na Mkoa wa Mara ambao wanaathirika na hii shughuli ya kupigwa na kunyang’anywa samaki. Peleka fedha watu hawa waweze kununua mashine, ipo mashine pale Rorya ambayo ukubwa wake na utumiaji wa mafuta ni mkubwa sana kwa siku wanatumia zaidi ya lita 600 hawawezi Askari wale kuimarisha ulinzi maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekuwa wakiiomba Serikali iweze kuwasaidia kupata mashine ndogo za watt power 40 mpaka 50 ili waweze kuratibu ulinzi wa maeneo yale ya Kanda ya Ziwa.

Mheshimiwa Spika, wavuvi wanapigwa sana, watu wanafilisika kule. Ningetamani kwenye ulinzi na usalama wa maeneo ya bahari Mheshimiwa Waziri nione namna mlivyojipanga kuimarisha rasilimali samaki kwenye maeneo ya maziwa ili angalao kuondokana na hili ambalo limekuwa likienda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ningelisema hapa ni kuhusiana na kilimo. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kwa namna anavyokwenda, lakini ningetamani pia hii block farming ambayo inaendelea ingeenda na kasi kwenye maeneo mengi ya nchi, pia iende sambamba na hili suala linalokwenda la utambuzi wa udongo ambao unafaa kwa aina fulani ya zao, hasa kwa Mikoa ambayo haina mazao ya kimkakati na mazao ya kibiashara, ikiwemo na Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili likienda haraka litatusaidia sisi kulingana na yale mabadiliko ya tabianchi ambayo kimsingi yanatuathiri maeneo mengi na ndiyo yanatusababishia baadae ukame na njaa, kutakuwa hakuna chakula. Block farming inaweza ikatusaidia hasa tukiendana na kilimo cha irrigation kwenye maeneo mengi kwa kutambua mazao ya kibiashara kwenye Mikoa ambayo haina, ili kukingana na kuepukana na hili linalokwenda. Ningetamani sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha mtakapokuja kutenga fedha muendane kwanza na haya yote mliyoyapamga, lakini mwakani muende mtenge fedha kwenye Mikoa ambayo haina mazao ya miradi ya kimkakati ili kuweza kuimarisha na kuwapa fedha ili waweze kubuni, hasa Mkoa wa Mara ambao kimsingi umekuwa ukiathirika kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie moja kama muda utakuwa unaniruhusu. Lipo suala la utekelezaji wa umeme wa REA na hapa tumekuwa tukijibiwa sana, mimi ningetamani sana kwa baadae kuna umuhimu wa kuja kupitia kanuni ya majibu ambayo kimsingi huwa yanatolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa umeme wa REA leo ninavyozungumza ambao kimsingi unakwamisha shughuli na bajeti tuliyopitisha, tusipolisema leo maana yake hata mwakani litakwamisha shughuli na bajeti tunayopitisha. Wakandarasi maeneo mengi hawako site au hawatekelezi, lakini Serikali imekuwa ikisema kufikia mwezi wa 12 tutamalizana na hili zoezi, haliwezekani Mheshimiwa Waziri. Mimi ningetamani kama linawezekana adhabu yoyote itolewe kwangu mimi itakapofika mwezi wa 12 kama Wakandarasi watakuwa wamemaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakupa mfano, Vijiji 13 Mkandarasi ametekeleza Kijiji kimoja tu ndiyo umeme unawaka, ana mwaka mmoja na nusu. Leo tumebakiza mwezi mmoja ukisimama ndani ya Bunge ukasema ndani ya mwezi mmoja utamaliza Vijiji 11 haileti maana. Mimi ninaomba sana fedha hizi za miradi, hizi ambazo zinachochea ukuaji wa uchumi kwenye umeme na maji zitoke kwa wakati, lakini usimamizi wake uweze kuwa imara sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)