Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi pia ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu. Awali ya yote naomba nianze kwa kumpongeza Rais wetu mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kazi kubwa ambayo inafanywa hasa katika Majimbo ya pembezoni kama Mikumi. Kuna kazi kubwa inaendelea kuna mambo mengi ambayo yalikuwa yameshindikana lakini sasa yanafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Ruhembe kuna daraja kubwa ambalo linaenda kuunganisha Kata za Ruhembe, Kidodi na Ruaha zinaenda kupunguza umbali wa wananchi na wakulima kutoka kilometa 30 mpaka kilomita mbili. Pia kuna kata inaitwa Vidunda ambayo ilishatengwa na haikuwa na mawasiliano ya barabara lakini sasa hivi inaenda kuwa na mawasiliano ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kata za pembezoni kama Malolo, kama Uleling’ombe, Kilangali hata Kisanga ambazo sasa hivi zinaenda kuunganishwa na barabara kuu lakini pia uzalishaji wake wa bidhaa za kilimo unaenda kuunganishwa na masoko. Jitihada zote hizi zinaendana pamoja na uboreshaji mkubwa wa vituo vya afya, shule na maeneo mengine ya huduma za kijamii. Tafsiri yake ni kwamba huko tunakoenda wananchi wengi watabakia vijijini na migration kutoka vijijini kuja mjini itaendelea kupungua kwa sababu ya uboreshwaji wa miundombinu lakini pia huduma za kijamii katika kata na vijiji vya pembezoni. Maana yake nini tunaenda kushuhudia rural transformation ambayo haijawahi kuonekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali hapa je ni kwamba elimu inayotolewa na vyuo vyetu inaakisi maendeleo haya ambayo yanaendelea vijijini? Kozi ambazo zinatolewa na vyuo vyetu zinaandaa vijana wetu kurudi vijijini na kwenda kutumikia maisha katika kata na maeneo ya pembezoni? Ninapoona tunaendelea ku-admit wanafunzi katika vyuo vyetu vikuu katika kozi ambazo hazitoi ajira, sioni kama kuna seriousness katika ku-transform vijiji vyetu na hasa katika kata za pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye hili kwa sababu Ofisi ya Waziri Mkuu inasimamia sera, lakini pia ajira vijana na hata walemavu, ningependa sana kuona uratibu katika huu Mfuko 10% za wanawake, vijana na walemavu za TAMISEMI zinaratibiwa vizuri kuwa sehemu ya kutoa majibu ya changamoto katika maeneo yetu ya pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali yetu, mwaka 2014 ilifanya study ya kuangalia kiwango cha ujuzi wa nguvu kazi na katika study hiyo tulikuwa tumeona kwamba lengo ilikuwa ni kuangalia namna ya kujenga uwezo unaohitajika katika soko la ajira, watu kujiajiri na kuajiriwa. Tuliona matokeo ya utafiti ule, asilimia 79.9 ya nguvu kazi ilikuwa chini ya kiwango cha ujuzi, kwa maana low skilled, 16.6% ni semi skilled kwa maana kiwango cha ujuzi katika soko la ajira kilikuwa ni kiwango cha kati. Tuliona 3.6% ya nguvu kazi katika ajira na ujuzi wake ni chini ya 3.6% ambao walikuwa ni higher skilled na ndiyo matokeo yake Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali ikaja na mikakati minne ya kukuza ujuzi kwa maana utarajali internship, lakini pia urasimishaji wa ujuzi ambao umepatikana nje ya mfumo kukuza ujuzi wa wafanyakazi na wale waliojiajiri lakini pia uanagenzi kwa maana ya friendship.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hizi program zilikuwa ni muhimu sana na kwa kweli kwenye baadhi ya maeneo tumeona matokeo chanya. Ombi langu ni vyema sasa tukafanya study kuona ni jinsi gani tunaenda ku-transform hizi program nne kuona kwamba zinaenda kutatua tatizo la ujuzi kwenye nguvu kazi ya vijana wetu katika soko la ajira. Hapa tunaweza tukajifunza kutoka katika Nchi kama za Ujerumani ambazo zilifanikiwa sana, Nchi ya Finland, Korea lakini hata China juzi hapa tuliona wameamua kubadilisha Vyuo vyao Vikuu zaidi ya 600 kuwa polytechnics na vocational kwa ajili ya kufunza ama kutoa ujuzi kwa vijana wao ili waende kuzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika hili tuna la kujifunza, kama wenzetu wana Vyuo Vikuu 600 na wameona kabisa module ya elimu wanayoitoa pale ni nadharia zaidi, haiendi kujibu changamoto ya ajira, wamebadilisha kwenda kutoa ujuzi, kuna jambo kubwa la kujifunza kwao. Je, tunavyobadilisha vyuo vyetu vya kati kwenda kuwa Vyuo Vikuu na kutoa degree za nadharia, tunapotoa graduates 5000, 10,000 ambao wamesomea procurement wanaenda kuajiriwa na nani wanaenda kufanya kazi wapi hawa? Tunapoenda kutoa ajira ama graduates 10,000 wanasheria. Je, wahalifu wameongezeka kwenye hii nchi? Mahakama zimeongezeka? Shughuli zao ni nini wanaenda kuwaajiri wapi, je, kuna mkakati wa kuenda ku-absorb hili kundi kubwa ambalo lina graduate kutoka kwenye vyuo vyetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mambo haya tukiyatafakari kwa kina, tunaona kwamba kuna umuhimu wa ku-review elimu tunayoitoa kwenda kujibu changamoto za ajira zetu. Study hii ambayo imefanyika 2017 leo ni 2022 ni miaka mitano utekelezaji wake umefikia wapi kuna umuhimu wa kuifanyia tena study ili kujua je, asilimia hizi ambazo zilitajwa 2014 zimebakia kama zilivyo ama vipi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Ofisi ya Waziri Mkuu inashughulikia pia majanga, majanga mengi ukiondoa yale ya kiasili kama matetemeko na mafuriko, mengi tunaweza tukayadhibiti. Migogoro ya wakulima na wafugaji ni moja ya majanga ya Taifa hili ambayo tunaweza tukayadhibiti kama tunajipanga. Vyuo Vyetu vya Ufundi vyuo vyetu vya kati, vinaweza vikawa sehemu ya suluhisho la changamoto hizi kama vitaenda kutoa elimu ama ujuzi kwenye kilimo, kwenye ujenzi, kwenye miundombinu na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili ningeomba kusisitiza vyuo vya ufundi na vyuo vya kati vipewe jicho la kipekee. Tuna sheria ambayo 4% ya private sector inatoka ama inalipwa kwenye skill development levy. Bunge lako hatujui zinatumikaje ni vizuri tukajua kwa sababu lengo la skill development levy ni kuendeleza ujuzi wa nguvu kazi yetu. Je, fedha hizi zinaenda kwenye lengo lililokusudiwa na sheria? Tunajua 2% inaenda kwenye mikopo ya higher learning, lakini hizi 2% zinatumikaje katika kujenga na kuendeleza ujuzi wa vijana wetu? Ni swali ambalo tunatakiwa kulijibu na katika jibu lake linaweza kutupa changamoto ambazo tunazo lakini majibu ya kukosekana kwa ajira kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili ninapozungumzia 2% ya skills development levy, ni zaidi ya shilingi bilioni 150. Bilioni 150 inaweza ikatumika sehemu kwa ajili ya kuwanunulia vifaa vijana 90,000 ambao wanasoma katika vyuo vyetu vya VETA, wakatoka pale na vifaa vya kuanzia kazi, wakajiajiri na wakaajiri vijana wenzao na sisi tukapunguza mzigo wa vijana wetu kukosa ajira katika soko la ajira. Katika hili tunahitaji uratibu taasisi zetu za SIDO, VETA, TIRDO wana wajibu wa moja kwa moja ku-incubate vijana ambao wana ari ya kujiajiri na kuajiri wengine. Changamoto ya bureaucracy katika leseni na vitu vingine imekuwa ni zuio kwa vijana wengi kujiajiri. Sasa taasisi hizi zinapaswa kubeba jukumu la kulea vijana wajasiriamali ambao wanatumia ujuzi wao ambao wameupata kwenye vyuo vyetu vya ufundi kujiajiri na katika kuwalea wanapaswa kuangalia hizi compliance kama TBS, OSHA, Weight and Measures wanazi- meet katika kipindi cha uangalizi. Hilo linaweza likatusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, suluhisho la…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)