Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Yustina Arcadius Rahhi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Naelekeza mchango wangu kwenye changamoto hii kubwa ya ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijana wanamaliza kusoma katika madaraja mbalimbali, lakini wanapata changamoto kubwa sana ya kutafuta ajira ili waweze kujikimu kwa maisha. Tunafahamu kwamba kwa demokrasia ya nchi yetu idadi kubwa ni vijana, asilimia 35 ni vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 mpaka 35. Hao ndio nguvu kazi tunayoitegemea, hao ndio wenye ari na morali wa kuijenga nchi yetu ambayo tunafikiria tunaingia kwenye uchumi wa kati, lakini hautajengwa na wazee utajengwa na vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, crises ya ajira ni kubwa sana na sisi wenyewe tunaiona, hebu ona ukitangaza nafasi 100 ya ajira, applicants walivyo wengi ni elfu na zaidi, sisi wenyewe tukija huku Bungeni tumebeba mabahasha ya vijana wetu, wanataka kazi. Wengine wanao-sustain maisha pengine wanafanya kazi ya boda boda au wenye miamala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, boda boda wanakaa vijana kwenye kituo kimoja 20 au 40 akisubiria mteja akiwa na stress ya kufikisha mahesabu ya tajiri wake na ndiyo maana pengine wanapata ajali na wanaishia kukatwa viungo vyao. Nafikiri tuliangalie vizuri hii crises ya ajira na tunaona kwamba kwa mahesabu Word Bank kwamba kila mwaka Tanzania kuna vijana kama 800,000 wanaingia kwenye soko la ajira, fikiria kuna mwaka juzi hawajapata ajira, wa mwaka jana, mwaka huu na hatuwezi kuepuka kwa sababu tunawasomesha na tunaendelea kuzaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona kuna fursa kubwa pengine kwenye kilimo, kama tutakifanya kilimo kikawa kizuri na kikavutua kwa vijana na kilimo kitakachovutia vijana ni kilimo cha bustani ya mboga mboga na maua, kwa sababu ni kilimo ambacho atapata fedha haraka sana. Nafikiria hivyo, lakini changamoto ya vijana hawana ardhi, changamoto ya vijana hawana nyenzo, wala hawana mtaji. Sasa ni kwa nini basi Serikali nilikuwa nafikiria kwa kusaidiana pengine na halmashauri, wakaweza kutafuta ardhi ya kilimo hata kwenye halmashauri, wakawapa hawa vijana kwa kuwasimamia wakazalisha vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano nilikuwa naangalia kijana ukampa nusu heka ya kuzalisha labda mchicha tu ambao anaweza akapata fedha kila baada ya wiki tatu maana mchicha unaweza kuiva haraka. Katika nusu heka anaweza akapata tani nne, sawa sawa na kilo elfu nne, akiuza kwa elfu mbilimbili ana uwezo wa kupata elfu nane, fikiria ni katika wiki tatu, akitoa gharama za uzalishaji anabaki na kiasi cha fedha cha karibu shilingi elfu tano. Sasa ni kwamba sisi tuangalie hiyo namna kuwasaidia hao vijana tukawajengea mazingira mazuri ya upatikanaji wa maji, sehemu ambayo tunaona ni muhimu na maji ni kidogo tukawafungie ile mirija ya kufanya dripping irrigation. Ofisi ya Waziri Mkuu imejenga kitalu nyumba kwenye halmashauri lakini tunaona zile haziko sustainable pengine kwa sababu wangeendelea kujenga vitalu nyumba pengine huko vijijini, lakini vijana wanashindwa kwa sababu ya hizi changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwaacha hawa vijana wakajikatia tamaa kesho ndiyo watajiingiza kwenye makundi ya majambazi na baadaye tutakuwa hatuna usalama na sisi na nchi yetu. Kwa hiyo naomba Serikali itupe jicho la pekee, wakati inaendelea kujenga fursa na ajira pengine kwenye sekta maalum basi waweze ku-accommodate hiki kikundi cha vijana katika kilimo kwa sababu kilimo ndiyo kina fursa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine ni kwenye majanga au maafa. Najaribu kufikiria namna ambayo nchi yetu inashughulikia maafa, Tanzania kama nchi nyingine duniani tunapata maafa mengi, tunapata maafa ya ukame, mafuriko, vimbunga, magonjwa na kadhalika. Sasa kuna sehemu ambayo kwa kweli naipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu na nchi yetu kwamba kwa kweli wanashughulikia maafa tunaona. Kwa mfano yakija maafa labda ya ukame na mazao kukauka pengine kukawa hakuna chakula, Ofisi ya Waziri Mkuu imejipanga na nchi yetu imejipanga na nina imani kubwa kabisa kwa jitihada ya Rais wetu hakuna Mtanzania atakufa na njaa, kwa sababu kuna chakula cha kutosha kwenye maghala ya Taifa NRFA imenunua chakula, kwa hiyo hapo nawasifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasifu pia Kamati za Maafa zilizoko kijijini kama kule kwangu ni mfano mzuri tu Kamati za Maafa Vijijini wamejipanga, wakipata maafa ya misiba wana namna yao wanasaidiana, wamejiwekea level yao ya michango, wamenunua viti, maturubai, masufuria na kila kitu. Kwa hiyo wako well equipped, utaona kwamba ni namna gani sasa watu wameelewa namna ya kusaidiana kwenye maafa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shida yangu ni namna ambayo tunapambana na maafa tunapokuja kwa upande wa mifugo ambao hawajui kusema. Nchi yetu imekuwa ikipata maafa ya kufa mifugo karibu kila wakati ikijirudia rudia. Kama tunafahamu tu kwamba kipindi cha ukame na bahati nzuri watu wa hali ya hewa huwa wanatuelekeza kwamba kipindi fulani kitakuwa cha maafa, hivi mfugaji anapopoteza mifugo yake 10, 20, 30 au hata zizi lake lote boma lake likaisha, hivyo anakosa gani mpaka hapo na hatuna mpango mkakati, hatuna coping strategic kama ambazo tunafanya kwa binadamu, maana kwa binadamu chakula kikipungua tunapeana coping strategic tutakula mara chache chakula chetu tutahifadhi, tusipikie pombe, lakini tunapokuja kwa wanyama, tunawaacha wale wafugaji wana-suffer peke yao, mfugaji anapoteza mifugo yake anabaki maskini. Mifugo hii ni chakula, mifugo hii ni benki yao, mifugo hii ndiyo bima ya afya akiugua mtu ndiyo inatumika, mifugo hii ni kila kitu lakini tunawaachia wanahangaika wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiria kwa nini tusiwe na mkakati coping strategic kwenye mifugo ni nini? Kwa nini hata wakati mwingine basi tusiruhusu pengine mifugo ikaenda kuchungwa pengine kwenye buffer zone au sehemu ambayo ni reserved kwa wakati ule wa mwezi mmoja au miwili ili ku-risk mifugo yetu isife kama tunavyowaachia wanakufa mizoga imezidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tufanye utaratibu mzuri hata wafugaji wakalipia kuliko wajanja wachache wachache wao wanaweza wakaingiza mifugo kwenye game reserved, wakatoa rushwa lakini wengine huku wakiwa na stress ya ukame, mifugo ikisogea kwenye hizi buffer zone wanakamatwa na askari na wanashughulikiwa vya kutosha.

Kwa hiyo, nafikiri Serikali sasa iangalie kwa upande mwingine jinsi ya kupambana na haya maafa. Hata hivyo, nafikiria hivi huyu mfugaji anayepoteza mifugo yake yote akabaki maskini Serikali ina mpango gani? Kwa nini isimfidie sasa mfugaji ambaye amerudi kwenye zero point, ndiyo wafidiwe kwa sababu siyo kosa lake, ana kosa gani kama ni hali ya ukame, yeye ametimiza wajibu wake, amepewa mifugo yake amekwenda kuchunga amerudisha jioni, kwa hiyo anapopata maafa kama haya, Serikali ijipange na ikawafidie wafugaji ambao wanapoteza mifugo yao katika ukame wa namna hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, yanapokuja maafa haya kwa watu binafsi, pengine ya mafuriko, yakachukua nyumba pengine tena za wazazi wetu, ndiyo nyumba ambazo siyo bora au mapaa yakachukuliwa na vimbunga, ninachoona pale ni utashi wa mwanasiasa ambaye yuko pale au ndiyo uwanja wa mwanasiasa, akienda pale na bati mbili au tatu akapigapiga picha ndiyo unafikiri ni solution, kumbe yule mhanga pale pengine amepoteza chakula, amepoteza mavazi, amepoteza kila kitu.

Kwa hiyo nafikiria, Ofisi ya Waziri Mkuu ione namna gani ipambane kwa sababu kwenye shida Watanzania ni sisi na kwenye raha Watanzania ni sisi, tusiache kikundi cha Watanzania wachache wanaokuwa wahanga na majanga haya, wakapata mateso siku zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huo ndiyo mchango wangu na naiunga hoja mkono. Ahsante sana. (Makofi)