Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Janejelly Ntate James

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye bajeti ya Waziri Mkuu. Kwanza, nampongeza Waziri Mkuu kwa uwasilishaji mzuri ambao ume- cover mambo yote ya Kitaifa. Pia nampongeza Mheshimiwa Mama Samia kwa jinsi alivyoendelea kuinua maisha ya watumishi; na aliyowaahidi yote alitekeleza. Nina imani kubwa hata lile alilowaambia la mishahara, basi mwaka huu litatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu nitajikita ukurasa Na. 58 aya 107. Tunashukuru sana bajeti ya Waziri Mkuu imekuja na vitu vyote walivyofanya, jinsi walivyokagua mikataba ya kazi, jinsi walivyokagua Usalama, lakini kuna jambo wamelisahau ambalo ni muhimu sana kwenye ushirikishwaji wa watumishi. Hawajatuletea taarifa ya Mabaraza ya Wafanyakazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mabaraza haya yako kisheria kwa Tamko la Rais Na. 1 la Mwaka 1970. Mwalimu Nyerere alishaona mbali kuhusu ushirikishwaji wa watumishi. Ofisi ya Waziri Mkuu kina kitengo ambacho kinakagua Mabaraza ya Wafanyakazi; na CAG sasa hivi anakagua ukaaji wa Mabaraza ya Wafanyakazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika kwenye baadhi ya taasisi na Wizara, Mabaraza hayafanyiki kisheria inavyotakiwa. Wanafanya Baraza moja la Kupitia Bajeti kwa sababu wanajua isipopitishwa, haitapitishwa hapa Bungeni, lakini lile Baraza la kupitia utekelezaji wa bajeti na kupanga mikakati ya taasisi au Wizara, hayafanyiki.. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaweza tukawa tunasema bajeti hazitekelezwi vizuri, watumishi hawafanyi kazi vizuri, lakini ni kwa sababu hawapati ule ushirikishwaji. Hawapangi ile mikakati ya taasisi. Baadhi ya Wizara wanachofanya, wanafanya siku hiyo hiyo mabaraza mawili. Nimekaa huko, nimeishi huko najua. Wanaanza na utekelezaji, kesho yake wanafanya upitishaji wa bajeti.

Je, sasa mikakati waliyopanga itaingia kwenye bajeti wakati bajeti imeshapitishwa? Naomba Ofisi ya Waziri, kuhusu Mkuu ukaguzi wa Mabaraza, mkayakague kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee mifuko ya jamii. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais, amepeleka fedha kweli kweli kwenye mifuko ya watumishi ili wastaafu wetu walipwe. Hata hivyo, wastaafu wamebaki na changamoto mbili, huwa zinaniumiza sana. Mtumishi kabla hajastaafu kwa hiyari, Serikali humpa barua kwamba ujiandae kustaafu kwa miezi sita; lakini inapompa barua, haijiandai kutafuta zile documents zake zinazotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu kaanza kazi mwaka 1970, leo akifikia kustaafu, unamwambia barua ya kuajiriwa atafute yeye, kuthibitishwa kazini atafute yeye, ya cheo cha mwisho atafute yeye. Atavipata wapi? Mtumishi huyo ameshahama zaidi ya taasisi kama kumi, anaipata wapi barua ya ajira ya kwanza? Anapata wapi barua ya kuthibitishwa kazini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwashauri tu, mnapompa barua ya miezi sita ile kwamba unaenda kustaafu, pangeni na zile documents zake peleka kwenye mfuko, tuwasaidie hawa wastaafu wetu kuumia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingineni ya kutokupeleka makatako ya watumishi ipasavyo.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kumpa taarifa mwongeaji kwamba siyo tu documents zinazotafutwa kwenye maeneo mbalimbali, imefika wakati mtumishi anaacha kazi, halafu anaenda kudai pensheni yake, wanamwambia tajiri yako alikuwa hajalipa michango, kwa hiyo, hatuwezi kukupa hata pensheni. Kwa hiyo, kwa kweli ni jambo gumu sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Janejelly, taarifa hiyo.

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea hiyo taarifa na ndiyo point niliyokuwa naenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Taasisi na Wizara hazipeleki makato ipasavyo; wanakaa, hawapeleki. Kwa hiyo, mtumishi anapofikia kustaafu, akienda kwenye mfuko, anaambiwa una gap la miaka miwili, una gap la miaka mitatu; shughulikia. Sasa huyu ameshatoka ofisini na nafasi yake imeshachukuliwa, anashughulikia kupitia wapi? Kwa nini kwenye hiyo miezi sita mwajiri asiangalie kama mtumishi wake anayo hayo mapengo akayaziba mapema? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Ofisi ya Waziri Mkuu, mifuko iko chini yenu, hebu mjaribu kupeleka hata maelekezo ndani ya Wizara na Idara za Serikali wawasaidie hawa wastaafu kupanga vitu vyao kabla hawajastaafu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, anapopandishwa daraja, hawarekebishi; na hili suala liko kwa watumishi wa Halmashauri na walimu. Sasa anafanyiwa kokotozi kwa cheo kile kilichokuwa cha zamani, analipwa malipo pungufu, sasa kuja kupata hiyo tofauti itamchukuwa hata miaka minne au mitano au anafariki kabla hajalipwa. Naomba na hilo mliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye michezo. Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mwana-sports namba moja, lakini hii michezo ya Idara ya Wizara za Serikali tumeifanyia utani. Leo hii bajeti zote zitapita hapa, lakini angalia kila Wizara imeweka bajeti kiasi gani kwenye michezo? Michezo hii ina faida kwa watumishi, huwa inatufanya tunafahamiana, tunashirikiana na tunajenga afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yalipokuja maelekezo ya Katibu Mkuu Kiongozi kwamba kila Wizara ishiriki michezo, sasa taasisi nyingine wanachofanya, wanapeleka mshindani wa baiskeli mmoja na wacheza bao wawili. Wanasema taasisi imeshiriki na Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupitia kiti chako, Ofisi ya Waziri Mkuu itilie mkazo hili la michezo ndani ya Idara za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asubuhi hapa Menejimenti ya Utumishi wa Umma wamejibu swali kuhusu watumishi waliosimamishwa kazi na kesi zao hazijaisha. Zinachukuwa muda mrefu; miaka mitatu mtumishi yuko nyumbani anasubiri hatma ya kesi yake. Mtumishi huyu anaporudi kazini, utendaji umekwisha, muda wa kustaafu umefika; na hapa katikati mnapoteza ambapo angeweza kupata hata promotion nyingine, anastaafu kwa cheo cha chini, lakini ni kwamba eti evidence hamna. Sasa kama ushahidi huna, ulimsimamishaje huyu? Naomba tuangalie hawa watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa Serikali Kuu, lakini kipindi ambacho nimekuwa Diwani kwenye Halmashauri, nimegundua mengi kwenye Halmashauri zetu, watumishi wananyanyaswa kiajabu. Naomba tu, ukiangalia watumishi wa Halmashauri, mwajiri ni TAMISEMI, mpandisha daraja ni TAMISEMI, lakini ikifika nidhamu, tunasema Baraza la Madiwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuliangalie kwa makini sana hili. Hata nidhamu yao irudi kwa yule anayemwajiri. Tunawaumiza sana watumishi ambao wako Halmashauri. Naomba hili tuliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, tuangalie mahusiano ya viongozi na watumishi wao. Viongozi wengi wamekuwa ni watoa maelekezo, sio wa kushauriwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja mkono. Ahsante.