Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Vincent Paul Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu kwenye bajeti yake ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni nzuri sana imegusa maeneo mengi ya nchi hii. Kwanza kabisa napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Rais ameupiga mwingi sana. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana ya maendeleo ndani ya nchi yetu na nje ya nchi. Ukiangalia katika Jimbo langu la Nkasi Kusini lilikuwa na Kata 11 kituo cha afya kilikuwa kimoja tu, ndani ya uongozi wa Mama Samia Suluhu Hassan nimejengewa vituo vya afya vine! Mama Samia safi. Madarasa yamejengwa, Vituo vya Afya vimejengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maji. Kwenye changamoto ya maji kuna miradi mingi kichefuchefu ndani ya Wilaya ya Nkasi pamoja na Mkoa wa Rukwa mzima. Naomba ile miradi kichefuchefu ipewe Jeshi la Ulinzi. Jeshi la Kujenga Taifa tumeona linafanya kazi vizuri sana kwenye miradi mbalimbali, ile miradi kichefuchefu basi wakabidhiwe Jeshi ili iweze kwenda kwa haraka na kumalizika kwa muda mfupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, upo mradi wa maji Mlale, upo mradi wa maji Kizumbi una miaka nane sasa hivi bado umetekelezwa ninaomba Wizara ya Maji ikae chini miradi hii ikabidhiwe Jeshi la Wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Nkasi Makao Makuu ni aibu, ina changamoto kubwa sana. Nadhani Tanzania nzima Wilaya ya Nkasi haina maji, ninaomba kuna mradi wa Ziwa Tanganyika lakini tuwe na mradi wa dharura kwa sababu huu mradi wa Ziwa Tanganyika utachukua muda, tuwe na mradi wa dharura wa kuokoa maisha ya watu wa Wilaya ya Nkasi. Ipo mito, mto Mfwizi na Mto Zimba, mito hii ni vyanzo sahihi havikauki maji kiangazi na masika, ninaomba Wizara ya Maji ije itengeneze mradi wa maji kwenye hii mito miwili Zimba na Mfwizi maji ya mserereko yaweze kwenda Wilaya ya Nkasi kama mradi dharura ambao utaweza kunusuru maisha ya watu wa Wilaya ya Nkasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije Ziwa Tanganyika. Ziwa Tanganyika toka tunasoma tunaulizwa Ziwa lenye kina kirefu majibu ni Ziwa Tanganyika, Ziwa hili hakuna meli hata moja, hakuna usafiri wowote ndani ya Ziwa Tanganyika. Kwa hiyo, uchumi wa Mikoa ya Kigoma, Rukwa, Katavi ume- paralyze japo bajeti ipo ya kutengeneza meli Liemba na Meli MV Mwongozo, naomba hili la meli Ziwa Tanganyika liwe dharura ni janga kama UVIKO! haya ndiyo maeneo ya kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwona Mheshimiwa Rais anahangaika kufungua milango ya kiuchumi, Congo imeingia Afrika Mashariki, amejenga Ubalozi lakini miundombinu inayoelekea kwenye lango la uchumi bado ni shida, niiombe TARURA iongezewe bajeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais alitupa Bilioni Moja na Milioni Mia Tano kwa ajili ya Miundombinu katika Majimbo yetu, Mheshimiwa Rais Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la TARURA iongezewe kuna barabara ya Ninde, Kizumbi, Wampembe, kuna vilima hizi barabara hazipitiki. Ndani ya Jimbo langu Kata Nne magari hayaendi, ikifika masika ndiyo kabisa. Kwa hiyo, meli usafiri wa ndani ya Ziwa Tanganyika meli hakuna na hizi Kata zipo ndani ya Mwambao wa Ziwa Tanganyika, usafiri ndani ya Ziwa hakuna, barabara hakuna kwa hiyo, wale watu unaweza ukapata picha wanaishi maisha ya namna gani, hata mzunguko wa pesa hakuna! Kwa hiyo wanamaisha magumu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba Wizara ya Miundombinu suala meli Ziwa Tanganyika ni janga ifanye kama dharura imeingiza kwenye bajeti lakini bajeti inaweza ikatumia miaka miwili mitatu wananchi wanateseka hakuna mawasiliano na nchi za jirani za Congo, Zambia na Burundi ambao ndiyo chanzo cha uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa ajira nashukuru sana Ndugu yangu Mama yangu Jenista Mhagama amesema Rais atatangaza ajira, nipende kumshukuru sana. Ajira hizi wafanye utafiti zielekee vijijini kwa sababu kuna shule zina Walimu wawili, vituo vya afya vina Muuguzi Mmoja, mfano Nzinga kuna Muuguzi Mmoja, Mwinza kuna Muuguzi Mmoja, Kizumbi kuna Wauguzi Wawili, kwa hiyo wanapotoa ajira hizi waelekeze maeneo ambayo kuna upungufu wa Wauguzi au watumishi wa afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuja kwenye Mahakama, hotuba ya Waziri Mkuu hapa ilionyesha mahakama nyingi nchi nzima zinajengwa lakini nchi hii tuwe na vipaumbele kuna maeneo ambayo ni nyeti kila Mbunge humu akikaa akaorodhesha maeneo nyeti kwa sababu mahitaji ni mengi, vipaumbele vipo vingi, lakini tufike sehemu fulani tuwe na maeneo ambayo yanaweza kuchangia pato ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano ndani ya Jimbo langu ipo Kata ambayo Hakimu anatumia stoo ya mazao ndiyo anahukumia kesi mule ndani! Mheshimiwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Pinda alifika tumemkuta hakimu yupo ndani ya godown. Kwa hiyo, tungeanza kuwatoa kwanza Mahakimu ambao wanatumia ma-godown ndiyo tuanze kukarabati hizo nyingine na tujenge hizo nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa mawasiliano. Nina Kata tano kwangu Jimboni hakuna mawasiliano kabisa. Simu hamna na zipo mwambao kwao hata uhalifu na hata usalama wa nchi hii unakuwa hatarishi. Mfano Kata ya Kala, Kata ya Wampembe, Kata ya Ninde, Kata ya Kizumbi, hizi Kata ndiyo uvuvi unafanyika mkubwa sana hakuna mialo, miundombinu mizuri, hakuna masoko hakuna vituo vya Polisi, kwa hiyo mtu akivua leo hii akiuza jioni anavamiwa anachukuliwa nyavu ananyang’anywa fedha. Ninaomba Wizara ya Mambo ya Ndani baada ya bajeti hii anapohitimisha aje aseme Kala Kituo cha Polisi kinaanza kujengwa lini? Kwa sababu mimi kama Mbunge wao tumeshachanga fedha cement tumejenga imefikia kwenye renter ni wao Wizara ya Mambo ya Ndani kuja kumalizia pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya mwaka mmoja wamevamiwa mara nne wananyang’anywa dhana zao za uvuvi, wananyang’anywa fedha, wanapigwa baadae wanahamia ng’ambo wakisha wadhulumu wakishawaibia, wakishawavamia kwa sababu hakuna Kituo cha Polisi. Kwa hiyo watu biashara zao hawafanyi kwa sababu hakuna amani, hakuna mialo kama miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti hii sijaona ujenzi wa masoko ukanda wa Ziwa Tanganyika ambako ndiko mazao ya samaki inatakiwa kuwe na kituo cha Kitaifa cha masoko ili mtu anapokwenda kufanya biashara yake ya mahindi kupeleka Congo kuwe na kituo.

Mheshimiwa Naibu Spika, njooni mjenge soko Wampembe, Mheshimiwa Jafo amefika Wampembe anakufahamu, njooni mjenge Wampembe soko la biashara la mazao ya Samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu lina changamoto kubwa sana, upande wa vituo vya afya. Nimesema toka nimeingia kituo cha afya kilikuwa kimoja nacho kilijengwa kwa kuchukua fedha za zahanati. Ina maana mpaka tunavyoongea hivi ni ndani ya Mama Samia ndiyo vituo vya afya vinajengwa Vinne. Hakuna vituo vingine. Kwa hiyo, ni shida sana jiografia ya Jimbo langu la Nkasi Kusini kidogo lilikuwa limesahaulika upande wa miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba TARURA waongezewe fedha ili tuweze kumaliza changamoto ya barabara mwambao mwa Ziwa Tanganyika pamoja na Jimbo la Nkasi Kusini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)