Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Eng. Mwanaisha Ng'anzi Ulenge

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwenye kunemesha neema kubwa na mwenye kuneemesha neema ndogondogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukuwe fursa hii sasa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayofanya kufuatilia shughuli za kila siku za Serikali, hakika anaitendea haki nafasi yake hii. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa anayofanya ya kuhakikisha anatuletea maendeleo Watanzania na hakika Mheshimiwa Rais wetu amedhihirisha upendo wake kwa Watanzania wote kwa kuanzisha Wizara maalum ya wanawake jinsia na makundi maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii inaonekana kabisa adhma ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha anakwenda sambamba na malengo 17 maendeleo endelevu ya dunia ya kuhakikisha kwamba hakuna anayeachwa nyuma katika maendeleo endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba Serikali ilianzisha na kuunda Tume ya Sekretarieti ya Ajira kwa mujibu wa kifungu cha 29(1), Sura 298, iliipa mamlaka ya Sekretarieti ya Ajira iajiri kwa niaba ya Serikali. Sasa hili Wizara hii mpya ambayo imeundwa iweze kufanya kazi na kuleta tija kwa makundi yale yaliyolengwa wakiwemo waajiri wangu wanawake wa Mkoa wa Tanga. Naiomba na kuishauri itoe kibali cha muda kwa Wizara hii ili iweze kuajiri Maafisa Maendeleo Jamii Kata na Afisa Maendeleo Jamii ya Vijiji kwa sababu ni wachache mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, peke yake kuna upungufu wa 2,322 Maafisa Maendeleo Jamii Kata, kwenye ngazi ya kata, lakini Maafisa Maendeleo Jamii wa Mkoa kuna upungufu wa 2,284 na Maafisa Maendeleo Jamii wa Wilaya kuna upungufu wa Afisa Maendeleo Jamii 41. Niiombe sasa Serikali itoe kibali kwa mamlaka ya ajira za wilaya na za mkoa na hata ngazi ya wizara hii ili iweze kuajiri kwa muda ili wizara hii mpya ikaweze kuleta tija kwa makundi yaliyolengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kuchangia ukurasa wa 10 mpaka wa 13 wa hotuba ya Mheshimiwa Rais ambao umeeleza mafanikio yaliyopatikana katika kutekeleza mpango na bajeti ya mwaka 2021/2022. Miongoni mwa mafanikio yaliyotajwa ni pamoja na kukamilika kwa kulipa fidia maeneo ya kipaumbele katika mradi wa bomba la mafuta linalotoka Hoima mpaka Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa taarifa zilizopo miongoni mwa maeneo ya kipaumbele ni pamoja na eneo la Mkuza ambapo ndiyo bomba linalazwa mita 30, kwa maana ya 15 kutoka kila upande lakini Mkoani Tanga takribani wananchi 100 hawajalipwa mpaka sasa kutoka mwaka 2018 Juni. Sasa mkisema kwamba mnawalipa maeneo ya kipaumbele vipi wananchi hawa waliopisha eneo la Mkuza mpaka leo hawajalipwa? Tunaishauri Serikali iwalipe wanachi hawa tangu Juni, mwaka 2018 ni miaka minne sasa wameyatoa maeneo yao na mpaka leo bado hawajalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna makampuni ambayo yalikuja tangu Julai mwaka 2019 kuchukua maeneo katika upande ule ambapo mradi utaelekea. Alikuja TPA, alikuja Mihan Gas, amekuja Ngorongoro, amekuja Simba lakini wengi wao pia hawajalipa. Kwa mfano, Black Oil wamechukua hekta 200 hawajalipa mpaka sasa na tathimini ilikwishafanyika vilevile Ngorongoro hekta 100 hawajalipa mpaka sasa na sasa hivi ni takribani miaka minne inakwenda mnawaambia nini wananchi wale wa Tanga waendelee kukaa Idle mpaka lini sasa?

Niiombe na kuishauri Serikali iwahimize makampuni haya yaliyochukua maeneo kule Mkoani Tanga kwa ajili ya bomba la mafuta, wafanye hima na haraka kuhakikisha wananchi wale wanalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani tumeshafanya tathmini na kila kitu leo unakuja kumwambia mnazi wake ulikuwa asilimia 50 sasa hivi mnazi umefika asilimia 100 umlipe kwa thamani ile ya asilimia 50 haiwezekani! lazima wa- consider time value of money kwa sababu ni muda mrefu sasa umepita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nizungumze suala la elimu nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kuwapa mabinti second chance ya kurudi mashuleni baada ya kujifungua na inaonekana kuna baadhi ya watu ni kama wanaona kitu kile hakiwezekani, binafsi yangu nampongeza sana sana Mheshimiwa Rais kwa azma yake hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tujiulize katika Taifa letu hili sisi wanawake tulioolewa tumetoa second chance mara ngapi kwa waume zetu labda wanapotutenda au akina Baba mmetoa second chance mara ngapi kwa wake zenu wanapowatenda, inakuwaje binti aliyepata ujauzito asipewe second chance ya kurudi shuleni? Mimi ninampongeza sana Mheshimiwa Rais amejipanga vizuri, kuhakikisha kwamba no one is left behind katika maendeleo endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshauri sana Mheshimiwa Rais wetu pamoja na Serikali yetu kwamba ili sasa Binti yule ayafikie malengo ambayo Mheshimiwa Rais wetu anayatamani na ninafikiri hii itakuwa legacy kubwa kwa Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha anajenga mabweni nchi nzima kuwapunguzia watoto wanaotembea mwendo mrefu na hapo katikati ndiyo wanapopata vishawishi na kuharibiwa, pia kuwatengenezea mazingira wezeshi ya kuweza kusoma kwa bidii. Naiomba sana Serikali iweke legacy hii wakati huu wa Mheshimiwa Rais wetu mwanamama kabisa, kuhakikisha wajukuu zake na watoto wa kike wanapata mazingira mazuri wezeshi ya kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuongezea hapo, naomba niikumbushe sasa Serikali ikamalizie bweni katika shule ya Sekondari ya Mfundia kwenye Kata ya Kerenge kule Korogwe Vijijini. Bweni limeshajengwa lakini limekaa muda mrefu halijakamilika, binafsi yangu nimekwenda kujitolea kupeleka milango katika bweni lile ili watoto wa kike waweze kusoma, lakini mazingira bado hayajakaa vizuri namuomba sana Mheshimiwa Waziri husika ahakikishe bweni lile kwenye shule ile ya Mfundia Korogwe Vijijini linakamilika na mabinti wetu waweze kusoma. Mtu ukitembea ukifika shule ya Mfundia hakika mazingira is very conducive kwa kupiga book lakini mabinti wanahangaika mazingira siyo wezeshi. Niiombe sana Serikali ikamilishe jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niseme kwamba wakati tukimtazama Mheshimiwa Rais wetu jinsi ambavyo anapambana kwenda sambamba na dunia kama mwenyewe alivyosema ukitaka kwenda mbali nenda pamoja lakini ukitaka kwenda peke yako ina maana utakwenda haraka. Anaonyesha dhamira yake ya dhati kwenda na ulimwengu lakini cha ajabu sera zetu za nchi hii baadhi bado zipo nyuma. Wakati tunafikiria au dunia inazungumza maendeleo endelevu 17 kuna sera bado zipo kwenye maendeleo ya millennia! inasikitisha kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaziomba zile Wizara ambazo bado zina sera zilizopitwa na wakati zirekebishe sera zao yaani kuna Wizara kila uki-google inakuletea sera ya mwaka 2002 wakati tumeshatoka huko sasa hivi tupo mwaka 2020. Tunaomba sana sera hizi ziboreshwe ili kwenda sambamba na mipango ya maendeleo endelevu kama ambavyo Mheshimiwa Rais anayatendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Rais amefanya vizuri kwenye lengo Namba Tano la Maendeleo Endelevu, lengo Namba 10 la Maendeleo Endelevu na hata alipokaa juzi na kutafuta maridhiano ametekeleza lengo Namba 16 la Maendeleo Endelevu ya Dunia inakuaje sasa sera za ndani ya nchi mpaka leo nyingine zipo rasimu unakuwa na rasimu ya sera miaka mitano, miaka saba kwa nini zisikamilike ili kwenda sambamba na maono ya kidunia na maono ya Mheshimiwa Rais wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishie hapa nashukuru sana.