Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia. Kwanza namshukuru Mungu kupata fursa ya kusimama kwenye hili Bunge Tukufu kuchangia hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu; na kuna mambo mawili yawekwe mstari vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, unapokuwa kiongozi wa Serikali unaisemea Serikali, unapokuwa Mbunge unasemea wananchi wako. Haya mambo mawili lazima yapigiwe mstari vizuri, la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, ninaomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo ameifanya, hasa katika Mkoa wa Mara, ndio mkoa ambao hauna Hospitali ya Rufaa sasa kwangu inaendelea kujengwa, watu wetu wataishia pale Musoma hawataenda Bugando. Vilevile Musoma kulikuwa na shida ya uwanja wa ndege kwa muda mrefu, ametoa fedha nyingi mkandarasi yupo site, tutapata huduma ya ndege pale katika Mkoa wa Mara. Mheshimiwa Rais pia ametoa fedha katika majengo yetu ya mkoa, na tunamshukuru sana tunaomba aendelee kufanya hivyo kwa sababu Mkoa wa Mara kwa kweli kwa hadhi yake na heshima kubwa ungeweza ufanane na hadhi ya Mwalimu Nyerere, lakini kuna mapungufu ya hapa na pale ambayo naamini kwamba yataendelea kutekelezwa kadri ambavyo Wabunge wenzangu wataendelea kuleta maoni ndani ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwamba, kule Tarime tuna barabara yetu ya Tarime - Mugumu - Serengeti yenye urefu kilometa 86; nimeambiwa hivi asubuhi kwamba kuna mkataba angalau kilometa 25 kutoka pale Mgabili mpaka Nyamongo watajenga. Huu utakuwa ni mkombozi mkubwa sana katika eneo hili. Tuombe aendelee kutoa fedha ili tuweze kupata miundombinu watu wetu waweze kufanya kazi ya kuhudumiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumze mambo maalum katika Jimbo la Tarime Vijijini, na hili ni jimbo maalum ndiyo maana kuna kanda maalum. Sasa ondoa mawazo ya polisi, tuje kwenye huduma za kijamii, maliasili na ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilimuomba Waziri akiwepo Mheshimiwa Ndumbaro tangu mwaka 2020 aende kule Tarime kwenye kata ya Nyanungu, Kwihancha, Korongo na Nyarugoba hakwenda; lakini namshukuru Mheshimiwa Rais aliunda kamati ya Mawaziri wanane wakazunguka walienda wakaishia Musoma Mjini pale kwangu hawakufika, lakini wakanipa idadi na orodha ya vijiji ambavyo Mheshimiwa Rais ametoa kibali kwamba wananchi wale watapata eneo angalau la kuchunga na kutoa huduma kwa mifugo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niliomba kwamba mambo haya, na nimewasiliana na wenzangu wa Mkoa wa Mara, watu wa Serengeti, Mbunge wa Serengeti, Mbunge wa Bunda na mimi Tarime Vijijini; kwamba maeneo haya kuna malalamiko ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo GN ya mwaka 1968 ambayo wananchi wenyewe wanajua wapi kuna beacon na wapi hakuna beacon; na kumekuwa na ugomvi wa muda mrefu katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais ametoa maamuzi ya kutoa baadhi ya maeneo yaende kwa wananchi, lakini bahati mbaya; mimi ninapozungumza hapa nimeona juzi Mheshimiwa Waziri wa Ardhi na Naibu Waziri wa Maliasili walikuwa Musoma na wakatoa tamko, nikauliza wenzangu kikao kinachoendelea mmeshirikishwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, niliposema kwamba nendeni kule site na nikatoa hoja kwa Mheshimiwa Rais alipokuja tarehe tano Februari kule Musoma nikazungumza habari hii ya hifadhi ya Serengeti na malalamiko yaliyopo ya muda mrefu yaondolewe ili sisi Wabunge tupate amani na kuwa na mahusiano kati ya wananchi na Hifadhi ya Serengeti; kwa sababu pia inalazimika kutoa huduma kwa watu ambao wanazunguka pale kwenye mambo ya usalama na kwa ajili ya rasilimali za taifa na yeyote anayekwenda katika eneo lile. Kazi hiyo haikufanyika.

Sasa badala yake wametoka watu hapa Wizara hizi mbili wameenda kule Tarime, Serengeti, Nyamongo, Kwihancha, Gorong’a pamoja na Nyanungu; na wananchi wamenipigia simu kwamba sasa wanakagua mipaka ile. Kule Kwihancha ambako tulisema waende hakuna shida kwa sababu wananchi wameonesha beacon na wamekubaliana na wapimaji na watu wa hifadhi ya Serengeti. Lakini Gorong’a na Nyanungu wameenda kuonesha beacon juu ya mlima ambako kuna vijiji ambako kuna vijiji vya watu. Sasa wananchi wanauliza Mbunge anajua? Mbunge sijui.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kilichoniuma ni kwamba wamekwenda Nyanungu ambako mimi ndiyo Mbunge, watu wamenipigia kura, nikawaahidi wakati wa uchaguzi kwamba nitawatetea na Mheshimiwa Rais amekubali kutenga eneo mchunge. Sasa wale watu wameambiwa kwamba Mbunge wenu ameshirikishwa ingawa hapa hayupo; na ni uongo.

Sasa imagine; pale Ilala pale kwenye Bonde la mto Msimbazi wanaenda kuhamisha watu unaambiwa umeshirikishwa na hukushirikishwa. Kwa nini Waheshimiwa viongozi tunategeana mabomu njiani? Hizi ni ajali! Kwa sababu unaweza kutoa taarifa za uongo kabisa katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Waziri wa Ardhi twende na Wabunge wa Mkoa wa Mara wenye migogoro, twende tukae na wananchi wetu. Hamuwezi kwenda peke yenu kule mnawapa taarifa za uongo, halafu nikitoka Bungeni nikafanye kesi. Mimi si dhaifu kiasi hicho; sitafanya biashara hiyo, tutagombana. Tunataka twende sawasawa pamoja. Kama kuna jambo lipo, Mbunge ameleta Bungeni Waziri amshirikishe Mbunge ampe na background, wapange ratiba waende, kuna haraka gani katika jambo hili? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba, na hili uwe ni ujumbe kwa Waheshimiwa Mawaziri, sina ugomvi nao mimi, ninachosema, Mawaziri hawa tunaweza kuwatengenezea shughuli nzuri Wabunge wakashinda wakae hapa comfortably, lakini kwenda kutoa taarifa ya uongo halafu unasema Mkoa wa Mara unaongoza kuvamia maeneo; sasa hiyo taarifa mmejadili na nani? Unakuta Mwenyekiti wa Kijiji ambaye hawezi ku-argue, unaongea naye halafu unauliza Mbunge niambie, mimi nipo Dodoma nyie mpo huko Tarime Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba hili kweli lifanyiwe kazi vizuri, na iwe ni maeneo yote tushirikishane tu kuna ugomvi gani? Bora nialikwe hata nisihudhurie; lakini sijashirikishwa, watu wanaambiwa Mbunge wenu ameambiwa mnaniwekea bomu hilo ambalo nitakubali tulipukiwe wote siyo mimi peke yangu…

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa madini na mazingira, na hapa naomba Waziri wa Madini na Waziri wa Ardhi na Mazingira wanisikilize vizuri. Katika Jimbo la Tarime Vijijini eneo la Nyamongo kuna malalamiko ya muda mrefu sana, na ni malalamiko ambayo ni very genuine, yanaonekana kwa macho. Nataka nisema, tunayo changamoto ya maji machafu, ni malalamiko ya muda mrefu, tunayo changamoto miradi ya maendeleo, tuna changanoto ya fidia katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Murwambe, Kumalela, Nyamichele tangu mwaka 2012 watu waliahidiwa hawajalipwa nitaomba watu hawa, mgodi umeagiza kulipa tumeongea na Rais wa Barrick duniani wamekubali kulipa naomba haya mambo yafanyiwe kazi.

Lakini ningetaka nisema kwenye miradi hii ya CSR, kengele imegonga ya kwanza. Miradi ya CSR nataka niulize Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI anisaidie. Hivi, mimi ni Mbunge, nilikuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, Naibu Waziri wa Muungano na Mazingira, Naibu Waziri Ujenzi na Uchukuzi, Mbunge wa kipindi cha pili, mwanasiasa wa siku nyingi, nimekaa na Halmashauri yangu, tumejadili mipango ambayo ninayo hapa, ambayo inatoa kero Nyamwaga hospitali, maji Nyamongo na vituo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeuandikia na mgodi correspondences nyingi tukajibiwa, tumeandika tumepeleka TAMISEMI tukajibizana na Profesa Shemdoe, tukajibiwa, barua imetoka imeenda Wizara ya Fedha tukajibizana Tutuba tukakubaliana. Tunataka fedha iende kwenye miradi ya maendeleo. Wako akinamama pale Nyamwaga wanajifungulia barabarani kwa sababu wodi haijakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo kule Nyamongo hii ripoti ya Jafo ya maji machafu imeharibu hali ya hewa kwa sababu watu wanaogopa kunywa maji na kula Samaki, lakini kwenye fedha hiyo ya CSR kuna fedha milioni 900 mgodi wamekubali kutoa maji kwenye chanzo chao, maji yaende pale Kewanja na Nyangoto ili wapate maji. Hizo fedha Mkuu wa Mkoa peke yake ambaye ni mgeni Mkoa wa Mara amekuja ameandika barua kwenda Wizara ya Fedha amezuia fedha zote. Angalia, Mbunge amekaa Halmashauri imekaa, TAMISEMI imeandika, Fedha imeandikwa, Mkuu wa Mkoa bosi mkubwa ameandika barua peke yake miradi sasa imerudishwa Tarime wakajadili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Serikali za Mitaa ninayo hapa inaeleza Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya wata-facilitate na watengeneze mazingira mazuri kuboresha miradi ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge nimekuja hapa nazungumza habari ya fedha iende kule yeye amezuia. Nataka niambiwe utaratibu ukoje? Yaani Baraza la Madiwani limepitisha, sasa huyu mtu mmoja anazuiaje? After all fedha ya CSR hii fedha wala hatupewi cash, tunakaa kwenye vijiji. Kwa mara ya kwanza Tarime baada ya kuwa Mbunge fedha hii ilikuwa inasaidia vijiji 11 tu kati ya vijiji 88; tumekaa na Wenyeviti wa Vijiji, Madiwani wa Kata 26 bila kubaguana vyama, tukakubaliana sisi tufanye kazi ya Tarime Vijijini tupunguze malalamiko na kero, wakaridhia kila kijiji, kila kata ina mradi huu. Ningeomba nielezwe tukileta mipango kwenye halmashauri yetu inakuwa kuwaje tunakwamishana njiani.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante, kengele ya pili hiyo.

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Rais anafanyakazi nzuri naomba viongozi wengine aliowateua wamsaidie, Wabunge mliopo humu mtarudi hapa Bungeni kama kazi nzuri inafanyika kwenye majimbo yenu tushirikishane baada ya kuyasema hayo…. (Makofi)