Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia fursa hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kutoa shukrani kwa Serikali, Jimbo la Musoma Vijijini linaridhika sana tunapata miradi na ni Jimbo pekee ambalo ukitaka mradi wako utekelezwe njoo Musoma Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani ya pili ni kwa Serikali kwamba, kuna wajanja-wajanja ambao hawakutekeleza miradi yetu vizuri sasa Serikali imeanza kutumia vyombo vyake kufanya uchunguzi. Nitoe pongezi Serikali kuamua kufanya uchunguzi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani nyingine ni ya kufufua mradi ulioanzishwa na Mwalimu, wote wameongea hapa kilimo cha umwagiliaji na eneo ambalo Mwalimu alikuwa amelitenga mwaka 1973/1974 aanze kumwagilia kwa hekta 2,500 kule Bugwema natoa shukrani kwa Mheshimiwa Rais alivyokuwa Musoma Vijijini tukamuomba kwamba, ule mradi uanze na ninadhani bajeti itakayosomwa ya kilimo itaelezea jinsi ambavyo Bugwema Irrigation Scheme itafufuliwa na ninadhani tutalisha Tanzania nzima na nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mbali ya hayo ya Jimboni nije kwenye hoja ya Waziri Mkuu, ambayo naiunga mkono. Mimi nitaongelea sehemu mbili kuhusu sera na ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sera. Kama Taifa inabidi tuwe na sera nzuri sana ya mambo ya utafiti, maendeleo ya utafiti na ubunifu (Research Development and Innovation). Yote tunayoyaongea haya tukitaka kufanikiwa lazima tuwekeze kwenye utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mwaka 2020 nchi ambayo ilitumia pesa nyingi kwenye utafiti ukilinganisha na GDP yao ni Belgium na Sweden, ndiyo zilitumia asilimia
3.5. Nchi za Kiafrika mwaka 2006 tulipitisha kule Sudan Azimio kwamba, angalau tutumie asilimia moja ya pato letu la Taifa kwenda kwenye utafiti. Nchi nyingi za Afrika hazijafika huko, waliokaribia ni South Africa, Kenya na Senegal na wako 0.8 Tanzania tuko 0.5. Kwa hiyo, ninaomba kwa ajili ya sera na ofisi ya Waziri Mkuu kwa sababu ndiyo inachukua kila sekta hii tuongeze.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hiyo 0.5 nadhani haijatoka kama ipasavyo, maana yake tukichukua GDP yetu kama sasa hivi ni Dola tuseme Bilioni 60. Ukichukua asilimia Moja ya hiyo, karibu ni Dola Milioni 650, ukichukua 0.5 ni zaidi karibu Dola Milioni 300, sidhani kwamba, tunatumia. Maeneo ambayo tunapaswa kuweka mkazo kwenye sera ya utafiti, nimechukua ni maeneo matano na Kiswahili chake wataalam watakuwa wanatafsiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwanza ni mambo ya space science na technology. Tunataka kilimo bora, lazima tujue mambo ya space science. Tunataka uvuvi, tunataka utalii, lazima twende kwenye space science na technology. Wengi wakisikia space wanadhani ni kitu kikubwa sana kinatisha, hapana! Tunahitaji kuwa na satellites.

Mheshimiwa Naibu Spika, sikilizeni ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, Kenya wana satellite, Uganda watarusha moja mwaka huu, Zambia watarusha mwakani moja, Rwanda wanayo moja, Egypt wanazo tisa, Nigeria wanazo saba. Kwa hiyo, kwenye mpango wa utafiti na vyuo vyetu lazima tuanzishe degree programs ambazo zinajielekeza huko kwa sababu, satellite siyo kitu cha ajabu, tunahitaji kwenye mawasiliano na hata kwa mambo yetu ya hali ya hewa na madhara mengine ambayo yanaweza yakatupata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni haya maeneo ninayoyataja karibu dunia nzima imeweka macho hapo ni life sciences, mambo ya kilimo, mambo ya mazingira, lazima tuwekeze kwenye life sciences.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni nuclear sciences. Nuclear siyo kwa ajili tu ya kutengeneza mabomu, lakini vifaa vingi sana vya hospitali vina nuclear science na technology ndani yake. Eneo hili hatujawekeza, lazima vijana wetu tuanze kuwasomesha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la nne ni environmental sciences. Wengi wameongea, mazingira hata yale ya Mto Mara tungekuwa na wataalam wengi yasingetupata yaliyotupata.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho la tano, kama tuna fedha zinatosha basi tuweke kwenye artificial intelligence. Hilo ndiyo eneo jipya ambalo tunakwenda, lakini tukitaka kufanya hayo pendekezo langu moja kubwa na ninaomba nilirudie ni lazima ile COSTECH ibadilike, COSTECH isiwe idara ndogo ni lazima tutengeneze kitu kinaitwa National Research and Innovation. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ile COSTECH tuibadilishe iitwe National Research Foundation and Innovation. Mambo yetu yote tunayoyataka ya utafiti na wapate hizi fedha ambazo tunazipigia hesabu, Mamilioni ya Dola.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine nilipenda kuchangia ni ajira. Wengine wote wameelekeza hukohuko kwamba, Tanzania kama tunataka kutoa ajira siyo ya kuajiriwa Serikalini, hatutaweza. Saa hizi tuko watu karibu Milioni 65 wanaoajiriwa hawajafika hata Milioni Moja, mahali ambapo watu wataajiriwa ni kwenye kilimo, kwenye uvuvi na ufugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huko tunakotaka kwenda ni kwa sababu sasa hivi duniani tuko watu karibu Bilioni Nane na hesabu imepigwa kila mwanadamu anahitaji chakula kwa siku kinachokwenda kwenye kilo 1.4. Kwa hiyo, tulime mazao ambayo tutaenda kuyauza huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia mazao yanayopendwa, vyakula vinavyopendwa duniani ni 12, nitavitaja kwa haraka haraka; salad, chicken , cheese, rice tea, coffee, milk, eggs, apples, soup, yoghurt na bread.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ndivyo vyakula vinavyopendwa sana duniani. Vyakula vyote hivi tuwe na mpangilio wa kuzalisha kuuzia dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ili tufanye hivyo tunahitaji kuwa na kilimo cha umwagiliaji kama ambacho tutakuja kufanya kule Musoma Vijijini kwenye Bonde la Bugwema. Lile bonde ni kubwa ni zaidi ya hekta 10,000. Kwa hiyo, turudi pale Mwalimu alipotaka kuanzia, hebu tuanzie hekta 2,500 halafu viwanda tunavyovijenga ni lazima viwe viwanda ambavyo vimejiegemea sana kwenye mazao ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu tunaolima pamba tungetaka kuwa na ginneries, tulitaka kuwa na viwanda vya nguo, ambao tunafuga kama kule kwangu Musoma Vijijini na Mkoa wa Mara tunataka tena tuanze kuwa na viwanda vya maziwa na cheese na butter kama ambavyo dunia inahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukienda kwenye kilimo nashukuru sana hawa vijana wa magwanda kweli wanachapa kazi, lakini lazima tushindane na wakubwa. Nimechukua hapa takwimu zinaonesha namna ambavyo wale wakubwa wanalima na sisi tujaribu kwenda angalao hata asilimia 10 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukichukua mchele China inaongoza duniani inazalisha tani milioni 150, Tanzania tujipime.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimechukua ngano China ya kwanza. Karibu mazao mengi ni wachina.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, hiyo ni kengele ya pili, malizia kwa sekunde tatu.

MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sekunde tatu; ni kwamba, tujitahidi hata wanigeria tuwazidi kuvuna mihogo ambao wao wana tani milioni 60 sasa Tanzania angalau tufikishe tani milioni 40. Ahsante.