Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza kabisa, nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri Mkuu na Mawaziri wetu wote kwa kazi nzuri wanazoendelea kuzifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kilimo. Tumekuwa tukishuhudia upungufu mkubwa wa vitu kama mafuta kutokuwa na mkakati mzuri ambao ungeweza kutuondoa kabisa kwenye hiyo dhiki ya mafuta. Niongelee kuhusu block farm mashamba ambayo yanalimwa kwa pamoja na yakiangaliwa na wataalam wetu. Najiuliza tu hivi kila Wilaya ingekuwa na block farm kubwa ambayo zile Wilaya zinakubaliana na alizeti, zikalima alizeti kuanzia heka 2,000 mpaka 3,000, naangalia ndani ya mwaka mmoja au miwili kweli tungekuwa bado tunapambana na kadhia hii ya mafuta ya kula? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo ni swali kubwa ambalo najiuliza nalo na niiombe Serikali iwe serious sasa kwenye suala zima la kilimo, ili kuokoa fedha zetu nyingi ambazo zinakwenda nje ya nchi kwa ajili ya kununua mafuta. Najaribu kuwaza tu kama tungeweza kulima heka 3,000 za mafuta kwenye Wilaya ndogo kwa mfano kama Urambo, heka moja wangeweza kupata shilingi milioni moja na nusu mpaka mbili tuseme wamekosa kabisa wamepata Sh.700,000/=. Ina maana Wilaya hiyo ingepata shilingi bilioni 2.1, ni ajira tosha kwa vijana wetu ambao tunahangaika nao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mwaka vijana wanamaliza Chuo Kikuu kuanzia 80,000 mpaka 100,000, hata Serikali ilete ajira gani hatutaweza kumaliza kuwaajiri. Ni lazima kwa makusudi mazima tuanzishe mashamba haya ambayo yatakuwa ni ajira kwa vijana wetu, lakini yatakuwa ni mwendelezo wa uchumi kwa Taifa letu. Tumemwona Mheshimiwa Rais anafanya makusudi mazima kuhakikisha anaweka mbele suala zima la kilimo, kwa ajili ya kupandisha uchumi lakini kwa ajili ya ajira pia kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais juzi tumeona ametoa pikipiki ambazo haijawahi kutokea kwenye historia ya nchi hii. Ametoa vipima udongo, binafsi nilikuwa sijui hata kama kuna vipima udongo, lakini Mheshimiwa Rais ametoa kwa nchi nzima. Yote hii sasa ibaki Wizara husika pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha na sisi tunakuwa serious katika kusimamia hii. Najaribu kufikiria tu je, Ma-DC wote wangepewa kwa maandishi kwamba ni lazima kila wilaya iwe na block farm, ni lazima kila wilaya ilime shamba la kimkakati leo hii tungekuwa na kilimo kiasi gani? Pia na Ma-RC wetu ambao wanafanya kazi nzuri, lakini bado kwenye kilimo tunahitaji msisitizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tungekuwa tunashindanishwa labda katika mikoa na wilaya kwamba ni DC gani alikuta wilaya yake inalima alizeti kwa asilimia nne akapandisha ikaja asilimia 10 au asilimia 15? Hii ingetusaidia sana. Kwa hiyo niiombe Serikali sasa iwe serious kwenye suala zima la kilimo na viongozi wetu ambao ni Ma-DC na Wakuu wa Mikoa, wawekewe viwango, ni lazima tuone mkakati wa kuhakikisha kilimo kinasonga mbele hasa kilimo cha kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwetu Tabora tuna DC wetu mzuri sana anaitwa Comrade Nawanda. DC huyo ametafuta Kijiji kimoja Ikomwa akatenga eneo la block farm kwa ajili ya Kijiji cha Vijana tu. Tunaamini vijana pale wakikaa kama 3,000 au 4,000 tutakuwa tumepunguza tatizo kubwa la ajira, watu wengi wanaotaka ajira tutakuwa tumewapunguzia pale. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kumwomba Naibu Waziri Katambi, anakwenda Shinyanga njia yake ni Tabora. Tunaomba akipita Tabora aje apite pale Ikomwa aone shamba letu lile la vijana lililotengenezwa na DC wetu wa pale Tabora Mjini, ili aweze kutupa mawazo lakini ku-empower kwa kitu chochote kile ambacho ataona kitasaidia na vijana wenziwe watakuwa wamepata ajira. Tunamwomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona pale Manyoni kuna block farm ya korosho, inakwenda vizuri mno, karibu viongozi wote wa Kitaifa wamewekeza, wana mashamba pale kwa nini tusifanye kwa nchi nzima kwa zao linalokubalika? Kwa hiyo, niiombe sana Serikali ili kutoa tatizo hili ni lazima tuwe serious na tupitie kwa Wakuu wetu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuwapa maelekezo kwamba ni lazima kila wilaya na mkoa wake wapate block farm.

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi sasa kwenye Mkoa wangu wa Tabora niongelee kuhusu barabara. Niiombe Serikali sasa ituunganishe watu wa Tabora kutoka Tabora kwenda Mbeya kupitia Ipole. Mpaka sasa hivi kutoka Sikonge kwenda Ipole kuna lami, kutoka Chunya mpaka Makongorosi kuna lami, lakini kuna eneo dogo lililobaki hapo katikati ambalo liwekwe lami basi tutoke Tabora mpaka Mbeya kwa lami. Niombe barabara ya kutoka Tabora kwenda Mambari, Mambari – Itobo, Itobo – Kagongwa ili iunganishe kwa lami kutoka Tabora – Mambari – Igongwa; na barabara hii ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi toka 2010. Tunashangaa Serikali inashindwa wapi kuimalizia barabara hii ambayo itakuwa ya ukombozi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naongelea tena barabara ya Tabora, Ulyankulu ambayo ina kilomita 90, tunaomba sana ijengwe kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niongelee suala zima la afya. Nimetoka kuuliza swali hapa kwenye Kituo cha Afya cha Town Clinic pale Tabora, kile kituo ni cha zamani sana na kiko mjini, sio kituo cha afya ni zahanati lakini zahanati hii inazalisha watoto 10 mpaka 20 kwa siku. Tunaiomba Serikali ipeleke pale Wodi ya Wazazi pamoja na Theatre, ili kusaidia mrundikano wa watu wengi wa Tabora Mjini wanaokwenda pale. Pale inakwenda Kata ya Chemchem, Kata ya Mbugani, Kata ya Tambukareli, Kata ya Ng’ambo, Kata ya Kanyenye, Kata ya Gongoni, ni kituo ambacho kinahudumia watu wengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali yetu ya Wilaya ni nzuri lakini imejengwa pembezoni mwa Mji watu wa Mjini wanashindwa kwenda. Pia niongelee upungufu wa watumishi wa afya katika Mkoa mzima wa Tabora. Igunga tunatakiwa ikama yetu tuwe na watumishi 1,021, lakini tuna watumishi 386 tu unaweza ukaona tofauti ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Nzega DC watumishi 300, lakini tuna watumishi 172, Nzega TC watumishi 300, tuna watumishi 181. Hivyo hivyo, kwenye wilaya zote watumishi ni wachache sana tuna asilimia 60 ya upungufu wa watumishi kwa mkoa mzima ningeweza kutaja kote, lakini sitaji kwa sababu ya tatizo la muda. Kwa hiyo, pia tulikuwa tunaomba Kituo cha Afya kijengwe Kata ya Kakola ambayo itahudumia watu wa Ikomwa, itahudumia watu wa Uyui na pale kuna Kituo kikubwa cha Reli ya Stiegler’s, itasaidia sana hata mtu akipata ajali. Kwa sababu ni Kituo kikubwa cha Reli, basi itasaidia kuwatibu watu pamoja na watumishi. Kwa hiyo, tunaomba pale papatikane Kituo cha Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena niongelee suala zima la mgogoro wa ardhi. Kwenye Kata ya Mbugani pale Tabora kuna mgogoro wa ardhi wa muda mrefu sana tulishausemea sana humu Bungeni, baina ya Wanajeshi na raia wa pale toka mwaka 2016 mgogoro huu mpaka leo haujapatiwa majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara husika ikakae na wale Wanajeshi, ikae na wananchi pamoja na watu wote wa ardhi iamuliwe kama ile ardhi imeshachukuliwa na Jeshi basi wananchi hao walipwe fidia. Tabora kuna maeneo makubwa sana wapewe haki yao, wapewe fedha zao ili waweze kuendelea na maisha mengine.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)