Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie katika hotuba au bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, kama waliotangulia nami nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan na nampongeza wazi kabisa ndani ya sakafu ya moyo wangu kwa sababu ya kazi kubwa anayoifanya, hasa ni katika kutekeleza bajeti ya mwaka 2021/2022. Pamoja na mambo mengine makubwa ya ulinzi na usalama, lakini kiujumla miradi ya kielelezo ameitekeleza vile ambavyo Watanzania hawakutegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miradi mingi Watanzania wanatakiwa waijue ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa SGR ilikuwa takribani asilimia sabini na kitu sasa hivi ni asilimia 95.3 inakwenda vizuri hasa katika vipande vya mwanzo kuanzia Dar es Salaam - Morogoro lakini hata Morogoro – Makutupora hiyo imeenda kwa kiwango kikubwa, lakini mikataba mingi imeendelea katika vipande vilivyobakia.

Mheshimiwa Spika, mradi wa kufua umeme wa maji wa Mwalimu JK Nyerere Megawatt 2,115, nikiwa Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, tumekwenda kule na tumejiridhisha kabisa kazi inakwenda vizuri kama Mheshimiwa Msukuma asubuhi alivyoeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo miradi mingine ujenzi wa bomba la mafuta ghafi, kutoka Hoima Uganda hadi Chongeleani Tanga, tunaambiwa kazi inakwenda vizuri na tumeona ameisaini mikataba ya mwisho.

Mheshimiwa Spika, vilevile mwisho kabisa ujenzi wa madaraja makubwa na barabara, hii hata kule Dar es Salaam wananchi wa Dar es Salaam wanajua kwamba lipo daraja zuri lile la Tanzanite pale Palm Beach ambalo limekamilika na limeshazinduliwa, lazima tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo aliianza akiwa Makamu wa Rais akaipokea vizuri na sasa ameenda nayo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nitajielekeza katika maeneo kama mawili hivi eneo la TARURA, lakini vilevile na eneo la ardhi na hasa katika ukurasa wa 142. Upande wa TARURA tunashukuru sana katika kipindi kilichopita tumeona hapa TARURA ilikuwa ina changamoto kubwa na tumelia sana humu ndani mpaka tukaenda kwenye tozo, tukaweka tozo kwenye mafuta ya petrol na diesel ili tuongeze zaidi ya bilioni 396 kwenda kwenye TARURA, zitusaidie kwenye majimbo yetu na Mheshimiwa Rais aliongeza zaidi ya milioni 500 hadi bilioni moja, wengine bilioni moja na nusu kuweza kwenda kwenye majimbo na tumeona kazi nzuri ambayo imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni tofauti sana na Dar es Salaam, Dar es Salaam kule tunalia sana na hasa kwenye Wilaya ya Ubungo. Hii Wilaya ipo pembezoni na imesahaulika kwa muda mrefu sana. Barabara kule hakuna kabisa ni vumbi, ni mchanga, vumbi na udongo. Tumelia mara nyingi viongozi wakubwa wakija tunasema lakini ukweli kama nchi inao mpango mzuri wa mradi mzuri ambao tumekuwa tukiambiwa, sisi wawakilishi na wananchi wenyewe mradi wa DMDP III, Dar es Salaam Metropolitan Development Program III. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ya kwanza imekuja tumesema hapa Bungeni, hata mwaka jana nilisema kwenye Bunge la Bajeti. Program ile imesaidia Buza, Kijichi, Sinza na maeneo mengine kuna mataa mazuri kule hadi kule Mburahati. Ya pili imeenda kwenye Mto Msimbazi, nami nafurahi kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu. Hii ya tatu tumeambiwa inakuja lakini hatuioni ikija. Bunge lililopita nilisema hapa, Waziri akisimama atuambie inakuja au haiji, lakini hakuna majibu. Sasa hivi tunaambiwa kuna mtaalam mmoja kakaa nayo zaidi ya miezi mitatu au minne kusaini tu ili tuweze kuona, barabara zaidi ya kilometa 107 za vumbi ambazo wananchi walikuwa wanaamini tukipata ile wananchi wa Jimbo la Kibamba na Ubungo wanaenda kufurahi. Tunaomba sana sana kwenye majumuisho tuambiwe DMDP III ipo wapi inakuja au haiji kwenye bajeti inayokuja.

Mheshimiwa Spika, lipo jambo hapa limezungumzwa kwenye ukurasa wa 42; Ujenzi wa Barabara ya Njia Nane Kimara – Kibaha nilisema juzi kwenye swali langu la msingi tunafurahi sana tunaambiwa zaidi ya asilimia 86 sasa hivi zimekamilika zaidi tu palikuwa na ongezeko la kimkataba kwenye zile kilometa 19.2 Kimara - Kibaha lakini kuna shida. Jambo hili lilitekelezeka kisheria; niliuliza hapa sheria gani ilitumika kuwaondoa wananchi wa pembezoni pale kwenye barabara ya njia nane na kuwavunjia bila fidia? Leo ni kilio kikubwa sana tulijibiwa hapa sheria iliyotumika ni ya mwaka 1932, yaani mwaka 1932 baba yangu Marehemu Mzee Mtemvu kaondoka, babu yangu kaondoka, Alhaji Zuberi Mwinyishee Manga Mtemvu kaondoka, hakuna hapa ambaye aliwahi kuwepo. Bunge hili ndiyo linatunga sheria, leo tunaishi na sheria ya mwaka 1932 kweli? Sheria ya 1932 ndiyo inavunja makazi ya watu?

Mheshimiwa Spika, naomba niwakumbushe, mwaka 1974/1975 palikuwa na operation vijiji ambayo ilikuwa ina lengo la kuondoa watu ndani ndani kuwaleta pembezoni mwa barabara ambao walijengewa shule, hospitali na kadhalika na kadhalika na vile vile hizi huduma maana yake ilikuwepo ni rasmi, lakini zipo sheria nyingine ambazo zilikuwa zinatumika. Kuna Sheria ya Mipango Miji, kuna Land Act ya mwaka 1999 Na.5, zote hizi zilikuja na kuondoa sheria nyingine zilizopita. Hata mwaka 1989 hati ya Kiluvya ilitolewa na Mheshimiwa Hayati Kawawa aliipokea mwaka 1989, Kijiji cha Kiluvya, sasa na yenyewe pia ilikuwa ni ya uongo. Hii inaleta sintofahamu tunaomba sana tufahamu jambo hili ili wananchi kama kweli walikuwa wana haki na haijafanyika, basi haki yao iende na zaidi ya hili hata palikuwa na kesi… (Makofi)

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, nataka tu nimpe mchangiaji Mheshimiwa Mbunge wa Kibamba, pacha wangu kwamba, hili suala la fidia hata wananchi wa Ubungo Kisiwani ambao wanatakiwa wapishe Mradi wa DART wanatakiwa walipwe fidia, lakini hatma yake haijulikani mpaka leo.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naipokea tena ukitegemea ni taarifa ya Profesa ambaye si muda mrefu anaenda kuingia kwenye kilio kingine cha bomoa bomoa kutokea Ubungo hadi pale Kimara walipoanzia kwangu. Pole sana nafikiri sasa utakimbizana na hilo ili lisiwafikie wananchi wako.

Mheshimiwa Spika, kuhusu jambo la ardhi, katika ukurasa wa 42 wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kuna muda wengine tunalia juu ya changamoto, changamoto ni kujenga jenga barabara zenye mabonde mabonde na kadhalika na mashimo shimo ya mvua, lakini kuna wakati mwingine ni lazima kama nchi tulilie juu ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, juzi Mheshimiwa Rais alienda kuzindua nyumba za Magomeni Quarter, jambo zuri, nakumbuka zamani nikiwa Diwani pale ndiyo tulianza ule mchakato wa kuvunja vile vijumba na tukaja na malengo yale au mawazo mapana au maono mapana mwaka 2012. Miaka 10 baadaye tunaona Mheshimiwa Rais anaenda kuzindua nyumba maghorofa pale ambapo wananchi na Watanzania wameona, ni leo lazima tuwe na sura hiyo. Leo tuna Tandale kongwe kabisa, leo tuna Magomeni, tuna Manzese lazima tufikie tukajenge majengo ya aina ile.

Mheshimiwa Spika, hili kwenye nchi kadhaa limeshafanyika Misri kule na nchi nyingine, ni jambo jepesi tu, waende kuingia makubaliano na wananchi ambao wanamiliki hati zile katika vile vijumba vyao, wanawapa floor ya chini na floor ya kwanza, floor ya tatu hadi ya kumi wanachukua kama nchi ambayo kimsingi…

MHE. TARIMBA GULAM ABBAS: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, ni lazima haya yote tunaweza kuyafanya…

T A A R I F A

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nataka nimpe taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Mtemvu kwamba yaliyowafika kwake Kibamba pamoja na Ubungo, yaliwafika wananchi wa Jimbo la Kinondoni mwaka 2015, wamebomolewa wananchi wa Magomeni, wananchi wa Hananasif jumla nyumba 94, lakini mpaka leo haijulikani, hivyo kilio chao na sisi Jimbo la Kinondoni tunacho.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nilinde na ni ukweli.

Mheshimiwa Spika, kwenye hoja hii ya makazi ambayo nilikuwa naendelea kuizungumza ni lazima tuzingatie Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa ambao moja ya malengo yake karibu manne, mojawapo ni kuchochea maendeleo ya watu. Unachocheaje maendeleo ya watu wakiwa maskini, wakiwa wanakaa katika makazi ambayo si bora. Kwa hiyo, naliona hili wenzetu vizuri ni lazima wazingatie kwamba sasa tukaboreshe kama Magomeni tulivyoona twendeni Tandale, Manzese na maeneo mengine ya Magomeni ili tuweze kuukuza mji.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Mtemvu anahoja nzuri sana ya uendelezi wa haya makazi, kwa mfano katika majiji yetu yote Mbeya, Arusha, Mwanza na baadhi ya miji ukiangalia kwa kweli makazi yapo holela holela. Kwa hiyo ana hoja nzuri nai- cement kwa Taifa ili serikali iweze kuichukua.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru itabidi nimalizie hapa hapa tu, lakini haya yote haya wenzetu wamewahi kusema kuna Karl Max aliwahi kueleza vizuri juu ya relationship between population growth and economic development. Kwa hiyo, tuweze kuona, lakini hata Mao Zedong, baba wa China alisema country is greatest wealth is its people tutumie idadi ya watu zaidi ya milioni sita ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam kuweza kuongeza mapato na kuweza kuongeza mchango katika pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja iliyo mbele yetu. (Makofi)