Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja iliyo mbele yetu ya Bajeti ya Waziri Mkuu. Napenda pia kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametukutanisha tena hapa leo kama ilivyo ada kila mwaka kwamba tunakaa hapa kupitisha bajeti, tunaiangalia nchi yetu, tunaipanga kwa sababu tunatafsiri mipango yetu katika fedha.

Mheshimiwa Spika, nina uhakika kwamba tunapopitisha bajeti, ni vyema pia tukapima mafanikio yake. Tunapaswa kuangalia tija iliyotokana na fedha tulizozitoa, lakini pia tunapaswa kuhakikisha kwamba tunapata muda kama huu wa kuweza kusahihisha na kutoa ushauri kutokana na mambo mbalimbali ambayo yametekelezeka au hayakutekelezeka katika bajeti iliyopita.

Mheshimiwa Spika, nina hoja kama moja au mbili kuhusu bajeti ya mwaka huu. Nipo kwenye Kamati ya LAAC, tunakutana na Halmashauri mbalimbali, tunafanya vikao, tunahoji na tunatembelea kukagua ufanisi wa miradi. Yapo mambo mbalimbali ambayo tumeyaona, lakini mimi nitaongelea hoja moja ambayo nimeona ni kero ya aina fulani katika bajeti tunazozitoa na matumizi ya fedha za Serikali.

Mheshimiwa Spika, katika ziara na vikao la LAAC, tumegundua kwamba kuna Halmashauri zinapewa fedha, fedha hizo zinatolewa mwishoni mwa mwaka; tuseme kama kwenye tarehe 15 mwezi wa Sita. Halafu baada ya hapo, hizo fedha kabla hazijafanya kazi yoyote, zinarudishwa Hazina inawezekana kwa kadri ya sheria ilivyo. Je, fedha hizo zinaporudishwa Hazina, Serikali inapata tija gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu fedha zinarudishwa wakati miradi haijakamilika, lengo linakuwa halikutimizwa, lakini fedha zinavyorudishwa kule Hazina, hazirudi tena Halmashauri. Kwa hiyo, miradi inakwama. Unaweza kukuta miradi inakaa miaka saba mpaka minane haijakamilika.

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano kwenye Halmashauri ya Shinyanga, walipewa shilingi milioni 500 mwezi wa Tano mwaka 2021; tarehe 26 mwezi wa Sita, zikarudishwa Hazina. Tumekwenda kuikuta katika Halmashauri ya Mbarali, tumeikuta Busokelo na Msalala. Sasa mambo kama haya Serikali inasemaje? Kwanini itoe fedha na fedha hizo kabla hazijatumika, malengo yake hayajatimizwa, halafu zinarudishwa Hazina? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu kubwa ni: Je, fedha hizi zinaporejeshwa Hazina, zinakwenda kukaa katika kifungu gani na katika Akaunti ipi? Fedha hizi sijawahi kuona hata CAG amekagua na kuzisemea. Nani anakuwa accountable wa fedha hizi? Kwa mfano, unapoenda kwenye Halmashauri wao watakuonesha kwamba tumepewa bajeti, lakini tulikuwa na fedha fulani labda shilingi milioni 500, sasa tumeongezewa shilingi milioni 500, tulikuwa na bakaa, watakuonesha; lakini kwenye bajeti kuu bakaa hii huwa hatuioni. Lazima Serikali itupe maelezo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, tunakwenda kupitisha bajeti ya shilingi trilioni karibu 41, tunatunga sheria ya matumizi na makusanyo. Kwa hiyo, ina maana sheria hii inawezekana inaelekeza kwamba fedha za mwaka fulani zisitumike mwaka huu; na nina uhakika Serikali inaweza ikanijibu namna hii. Ninajua kwamba tunapitisha Financial Bill kwamba sasa twende kukusanya. Tunapitisha fedha za matumizi, sasa tunakwenda kutumia, lakini hizi fedha zinapokwa kutoka kwenye Halmashauri, zinakwenda kuwekwa wapi? Nani anazisimamia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapenda kupata majibu. Tunapenda kuelezwa kwamba hizi fedha hazitumiki kutokana na sheria iliyopo, lakini tunaziweka mahali fulani, tunakuja kuzionesha kama bakaa katika bajeti hii ambayo tunapitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili linatia wasiwasi, tunajiuliza mambo mengi, tunataka majibu kutoka kwa Pay Master General, atuambie kwamba fedha hizi zikirudishwa, miradi haikutendeka; na yapo maelekezo. Nakumbuka mwaka 2021 katika Kamati ya Bajeti na hata Kamati ya USEMI huko walikuwa wakipambana na hili jambo. Kamati ya Bajeti ilitueleza kwamba mwaka 2021 wamesema fedha hizi zifunguliwe akaunti maalum ndani ya Halmashauri. Ukienda, huwezi kupata akaunti hiyo na huwezi ku-trace hizi fedha ukazipata. Kwa hiyo, inawezekana zinatoa mwanya wa kutumika ndivyo sivyo. Sijasema wizi, hapana. Nimesema zinaweza kutumika ndivyo sivyo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tupewe maelezo ili tuone Serikali inapobeba fedha hizi inapata impact gani? Wanaziweka wapi? Nani anakuwa accountable? (Makofi)

WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji.

T A A R I F A

WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa msemaji kwamba kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2021/2022, Serikali ilileta mapendekezo ya kurekebisha sheria iliyokuwa inasema fedha zirudi na sasa fedha hizo hazirudi. Kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu aliyoitoa mwaka 2021 wakati anahitimisha Bunge la Bajeti, fedha hizo sasa zinabaki kwenye taasisi husika, wanachotakiwa ni kuleta Mpango wa Utekelezaji wa fedha hizo, kwa sababu mwaka unakuwa umekwisha na fedha hizo zinabaki ndani ya taasisi husika au Halmashauri husika. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza, unapokea taarifa hiyo?

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, taarifa hii siipokea kwa sababu, tumekuta jambo hili lipo ndani ya Halmashauri. Nafikiri labda tungekuwa tumepata maelekezo mapema. Siwezi kukubaliana, inawezekana ni kweli, lakini lipo. Kama wamefanya hivyo, mbona bado linaendelea? Kwanini liendelee? Kwa hiyo, ndiyo maana nilikuwa nasema, mimi nia yangu ilikuwa…

SPIKA: Ngoja. Kwa sababu umeuliza hilo swali hapo mwisho, nadhani kwa maelezo yake, anasema ni mwaka wa fedha 2021/2022. Maana yake ni kwamba, fedha za mwaka huu wa fedha ndiyo ambazo hazitarejeshwa. Kwasababu hizo nyingine, zilikuwa ni za mwaka uliopita kabla sheria hiyo haijabadilishwa. Nadhani utakuwa umeelewa sasa.

Yaani yale malalamiko ya Halmashauri hayazihusu fedha za mwaka huu, kwa maana ya mwaka 2021/2022. Malalamiko ya Halmashauri ni ya huko nyuma yaani tuseme, mwaka 2019/2020 ama 2020/2021, lakini Mheshimiwa Waziri anachokizungumzia ni kwamba mabadiliko yemeshafanywa na Serikali. (Makofi)

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, sawa. Kwa hiyo, tutaiona katika ukaguzi wa mwaka huu, lakini bado tujue kwamba kuna fedha za nyuma. Labda aseme kwamba Bunge chini yako, lina uwezo wa kumruhusu CAG akakagua hizo fedha zilikuwa zinakwenda wapi? Tusifunge hoja hii kwa sababu huku nyuma kumekuwepo na fedha zilizokuwa zinakaa katika msingi huo na hazijulikani zipo wapi?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hoja yangu niipeleke hivyo kwamba tuone katika ukaguzi wa mwaka huu kama fedha zitakuwa zimeoneshwa kama anavyosema, lakini bado malalamiko yapo ndani ya Halmashauri na wanaandika barua kuomba warejeshwe, bado hawajibu huko Hazina sijui kuna kitu gani, wataendelea kuona, lakini mimi tayari nimetoa ujumbe wangu, tunapaswa nasi kama Wabunge kujua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni bajeti hii, kwa hiyo, tunajaribu kuangalia kila senti ya Watanzania inatumika vipi na kama inakuwa shambolic, tujue ili tuweze kurekebisha mambo ambayo tunayaona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee pia kuhusu ufanisi wa utekelezaji wa miradi hii. Ni kweli ipo miradi ambayo inatekelezwa vizuri na ipo miradi ambayo inatekelezwa chini ya viwango. Niende katika Mkoa wa Kagera huko Bukoba Vijijini, kumekuwa na maeneo mengi ambayo tumekuwa tukilalamika. Kwanza, tumelalamika muda mrefu na ninamshukuru Waziri wa Uwezeshaji umewahi kuwa Waziri wa Fedha, nimewahi kukulilia kwamba sasa huko kwetu ndiyo ukweni, vipi? Kwa hiyo, bado mambo ni mabaya namna hiyo, hatuna barabara tangu uhuru. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kama kuna jimbo ambalo limetelekezwa kabisa na sisi tuna uchungu kusema ukweli hatuna barabara pamoja na mipango hatuna barabara ya lami, hatuna barabara ya kufungua uchumi, lakini kuna maeneo ambayo yanatengezwa kwa fedha za nchi, lakini bado zinatengenezwa chini ya viwango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, naomba niseme kuhusu maeneo ya Chabaramba na eneo la Katokoro, haya maeneo ninayoyasema ni maeneo ambayo yana matingatinga ya miaka nenda, rudi. Ina maana labda hata mimi nimezaliwa yapo, lakini wanaokwenda kutengeneza inawezekana hawafanyi ule upembuzi yakinifu. Nashukuru tumelia sana hapa wametengeneza kule Katokoro lakini lile daraja nimefika mimi mwenyewe this time nilipoenda, limepasuka, lina nyufa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hata lile eneo la Chabaramba limetengenezwa, hata kama mimi sio mtaalam, barabara ipo hapa na ukingo wa maji upo hapa yaani vinaenda sambamba. Sasa nikajiuliza haya ni makosa ya wahandisi na wahandisi katika nchi hii wakati mwingine jamani, si wote lakini wakati mwingine wanatuharibia kazi. Wanaharibu kazi zao kwa sababu, unawezaje kwenda kwenye kazi kama hii halafu ukaandika certificate mtu alipwe. Kwa hiyo, kuna vitu vya namna hiyo. Tumelia kuhusu daraja la Karebe Bukoba Vijijini daraja hili linafanya kiungo na ndiyo inasaidia uchumi wa jimbo letu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)