Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Nicholaus George Ngassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha dira madhubuti katika kuongoza nchi yetu na kuna maeneo manne ambayo mpaka sasa tunasema Mheshimiwa Rais ameupiga mwingi.

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza ni kusimamia ulinzi na usalama wa nchi yetu, eneo la pili ni kusimamia maendeleo na ustawi wa Taifa, eneo la tatu ni kuimarisha utangamano na Jumuiya za Kikanda pamoja na uhusiano wa Kimataifa na eneo la nne ni kulinda tunu za Taifa letu ikiwepo umoja, amani, mshikamano, kulinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, lakini pamoja na Muungano wetu. Hongera sana Mheshimiwa Rais tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu akupe afya njema uendelee kutuongoza vyema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, nimesimama kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, pia nimpongeze Mheshimiwa Kassim Majaliwa pamoja na Wasaidizi wake kwa kuendelea kufanya vyema katika kusimamia shughuli za Serikali, pia na kuziratibu shughuli za Serikali pamoja na Bunge.

Mheshimiwa Spika, mimi nitachangia maeneo mawili ya kisera. Eneo la kwanza nitaongelea suala la usimamizi madhubuti wa fedha za umma na eneo la pili nitakalochangia ni suala la uchumi shindani, uchumi jumuishi kwa ajili ya maendeleo ya watu.

Katika mchango wangu moja utajikita kwanza katika kupitia document niliyonayo, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, hotuba ya Mheshimiwa Rais ya mwezi Aprili mwaka jana 2021 na Sheria ya Fedha za Umma (Public Finance Act, No. 6, ya 2001), lakini pia na Sheria ya Fedha za Umma za Serikali za Mitaa (The Local Government Finance Act) ya mwaka 2019. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina mifumo mbalimbali ya udhibiti wa fedha za umma, mimi nitajadili mifumo miwili. Mfumo wa kwanza ni unaosimamiwa na ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Hesabu za Serikali kwa maana ya Internal Auditor General na mfumo wa pili ni ule unaosimamiwa na Ofisi ya Mdhibiti na Msimamizi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa maana ya CAG, chini ya ofisi ya National Audit Office ambayo ni Ofisi ya Ukaguzi ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, unapokwenda kwenye Halmashauri zetu kwa sasa tunasema kwenye Majimbo, mama pochi lake limefunguka fedha nyingi zinakwenda. Pamoja na fedha hizi nyingi kwenda tunahitaji mifumo Madhubuti ili tuweze kuzisimamia fedha hizi ili ziweze kutoa matokeo kama ambavyo tunatarajia.

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza ni kuhusu ukaguzi wa ndani kwenye Halmashauri zetu. Unakwenda kwenye Halmashauri kwa mfano Halmashauri ya Wilaya ya Igunga tuna Kata 35 na tuna Vijiji 119, lakini tuna Mkaguzi wa Ndani mmoja tu. Ukisoma Sheria ya fedha ya Serikali za Mitaa na Sheria ya Fedha za Umma inataka hawa watu pamoja na majukumu yao mengine ya ukaguzi, lakini wahakikishe wanafuatilia ile michakato yote ya shughuli zinazofanyika kwenye Halmashauri ambako fedha za umma zinakwenda. Kutokana na uchache wa hawa watu wanajikuta muda mwingi wanaishia kukagua risiti za manunuzi na kukagua vocha za malipo, wanashindwa kuangalia michakato ya fedha zinakokwenda kwa ajili ya kuleta mwandeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndugu zangu, viongozi wangu na chama chetu sasa inabidi tuangalie hili suala tuweze kuongeza rasilimali watu katika hili eneo ili tuweze kusimamia vizuri rasilimali zetu za fedha. Kwa hiyo, katika hili jambo tuwe makini tuhakikishe tunaongeza watu, tuongeze rasilimali watu, tusijikite katika kuwajengea tu uwezo. Unapokuwa na mtu mmoja anasimamia ukaguzi katika Halmashauri moja ambayo ina Vijiji vingi na Sheria hii ya Fedha ya Serikali za Mitaa inasema kabisa huyu mtu anatakiwa kukagua mpaka akaunti za Halmashauri za vijiji, sasa vijiji 119 yuko mtu mmoja katika hali ya kawaida vinaweza kumzidia na asiweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbadala wake ni nini ama alternative? Sheria hii ya Fedha za Umma mwaka 2010 ilifanyiwa maboresho na Bunge likapendekeza kuanzishwe kitengo kinaitwa kitengo cha usimamizi wa vihatarishi Serikalini (Risk Management Unit). Baadhi ya sehemu wameanzisha idara kama Benki Kuu ya Tanzania na baadhi ya maeneo wameanzisha vitengo, lakini bado kuna changamoto kubwa kwenye Halmashauri nyingi wameweka ma-champion tu, ambao utendaji kazi wao pia ni mdogo.

Mheshimiwa Spika, faida ya kuwepo vitengo vya usimamizi wa vihatarishi ni nini? Yule mtu wa ukaguzi anapoendelea kuhangaika na ukaguzi wa vocha zile za malipo, anapohangaika kukagua risiti za manunuzi huyu mtu wa vihatarishi yeye anaangalia zile process na kuhakikisha anatoa assurance kwa hizi taasisi zetu za Serikali, Wizara, Idara za Serikali pamoja na mamlaka mbalimbali. Kwa hiyo, niwaombe Serikali kupitia Wizara ya Fedha na kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu waweze kulisimamia hili ili Idara zetu, Wizara zetu na Taasisi zetu wahakikishe vitengo vya vihatarishi vinaimarishwa katika Taasisi zao ili viweze kutoa assurance ya michakato mbalimbali ya investments na shughuli mbalimbali za Serikali zinazofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo ningependa kulichangia la kisera, linahusu uchumi wa kisasa, shirikishi na shindani. Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, Ibara ya 18 imeliongelea hili, lakini pia hotuba ya Waziri Mkuu eneo la 14 imelielezea hili. Unapoongelea uchumi shindanishi maana yake lengo letu ni kufungamanisha hizi sekta za uzalishaji na mimi hapa kwa kifupi nitaongelea sekta ya kilimo, lakini pia na sekta ya viwanda.

Mheshimiwa Spika, asilimia zaidi ya 65 mpaka 70 ya Watanzania wako kwenye sekta ya kilimo, sasa kama tunavyoona Serikali imeanza kuweka mikakati mbalimbali ya kuimarisha kilimo tunachokiomba sasa hivi hali ya hewa nchini imekuwa haitabiriki, mvua hazitoshi, pia ukijaribu kuangalia pamoja na kutoa pembejeo maeneo mengi uzalishaji unakuwa mdogo, kwa sababu gani?

Mheshimiwa Spika, hali ya hewa, kuna mabadiliko ya tabianchi, tujikite sana kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji. Niwaombe Wizara ya kilimo, maeneo yenye skimu za umwagiliaji kama kule kwetu Igunga tuna skimu ya Mwanzugi ni kubwa sana, tuna Bonde la Wembele ambalo maji kwa mwaka mzima yanaishia tu yamekaa hayafanyi kazi, waboreshe hizi skimu, wazihuishe ili tuweze kuongeza uzalishaji. Hii itasaidia hata kupatikana kwa malighafi katika viwanda.

Mheshimiwa Spika, naweza nikatoa mfano mdogo hapa, hapa nchini sasa hivi tuna uhaba wa mafuta ya kula, kwa sababu mwaka jana kufika mwezi wa Tisa viwanda vingi vya uzalishaji wa mafuta ya kula vilikosa malighafi uzalishaji ni mdogo. Sisi huku tumeweka tozo za kulinda masoko ya ndani ya mafuta ya kula, tunadhibiti yale masoko ya nje, sasa yanapopungua, soko la ndani bidhaa zimekwisha, tunapoanza kutegemea bidhaa na mafuta kutoka nje matokeo yake yanakuja kama sasa hivi tunajikuta bei inaongezeka na kunakuwa na malalamiko ya wananchi kupanda kwa bei ya bidhaa, hususan mafuta ya kupikia au mafuta ya kula. Kwa hiyo, ninaomba tunapoweka hizi kanuni za kulinda masoko ya ndani, tuhakikishe kabisa tunakuwa na uthabiti wa kuhakikisha sekta ambayo inalindwa iwe na uwezo wa kujitosheleza kuzalisha, kama ni kilimo iweze kuzalisha malighafi za kutosha ziweze kwenda katika viwanda ili tuwe na bidhaa muda wote na tusijikute kwamba tunasababisha mlipuko wa bei.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ambalo naweza kulichangia kwa kifupi sana ni katika suala la uchumi shirikishi, lengo letu pia ni kuhakikisha tunaboresha mazingira ya wafanyabiashara. Niwapongeze Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameweza kuanzisha soko zuri sana la wamachinga hapa ambalo lipo katikati ya Mji. Hii ndio namna ambayo tunaweza tukasema tunaboresha mazingira ya wafanyabisahara wadogo, huwezi ukatoka unasema unaenda kujenga soko la wamachinga kilometa 10 nje ya mamlaka ya Mji inakuwa ni ngumu. Kwa hiyo, unapoweka mazingira kama haya maana yake unaongeza mzunguko wa fedha, lakini pia ajira kwa wananchi, ajira kwa vijana zinapatikana kwa wingi, nasi kama ilani yetu ambavyo tumeahidi basi tunajikuta kwamba, tumeimarisha na tumeboresha biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa ni suala la urasimu. Tuombe kabisa pia Serikali sera zetu ambazo tunaenda tunapoboresha, hizi sera za kuhakikisha kwamba tunalegeza kuhakikisha kwamba tunalinda masoko ya ndani na kuongeza uzalishaji katika sekta ya uzalishaji tujikute tunapunguza urasimu. Mtu anapohitaji kuwekeza kama ni kiwanda au shughuli nyingine yoyote ya uzalishaji mali asijikute anatumia muda mwingi katika kutafuta vibali na kuzungushwa makoridoni.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Naunga mkono hoja asilimia mia moja. (Makofi)