Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu kipenzi, mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Kwa ridhaa yako naomba basi nitumie style ya Mayele kumshangilia Mama Samia Suluhu Hassan kwani anaupiga mwingi sana. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ninavyochangia hapa nina furaha sana baada ya kumwona Mwenyekiti wa Yanga Bunge, Mheshimiwa Gulamali baada ya kunikabidhi kadi yangu sasa ya Yanga kwanza. Sasa najijua ni mwanachama halisi wa Yanga. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika maeneo matatu na moja nianze na suala zima la nishati. Nianze kuipongeza Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa ambayo inaendelea kuifanya, chini ya Waziri wake Mheshimiwa January Makamba na msaidizi wake Mheshimiwa Byabato. (Makofi)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nimempongeza mwanachama wa Yanga kwa kuonyesha kadi yake na sio kadi tu, ni kadi ya viwango ya timu ya wananchi. (Makofi/Vigelegele/Vicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Kassim Iddi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ninapokea taarifa hiyo na ninaomba nimshangilie na yeye kwa style ya Mayele. (Makofi/Kicheko)

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba Yanga wanajitahidi kuigaiga ila tunawaomba waje na kadi za viwango. Simba ya Kimataifa tuna mpaka VISA Card, tuna kadi ya wanachama ya kiwango, ukiangalia kadi yao, yaani hadi wanatia huruma. Kwa hiyo, naomba mchangiaje aje achukue hizi kadi za Simba ili wakaboreshe za kwao zaidi kupitia Mwenyekiti wake wa Tawi. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo siipokei kwani Mheshimiwa Nicholaus Ngasa, Mbunge wa Igunga, ameniambia kuwa na kadi ya Yanga pia nimeanza kukopesheka kuwa na sifa. (Makofi/Kicheko)

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, naomba tu kumpa taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Iddi kwamba, wananchi wanamsikiliza na hayo sio waliyomtuma, kwa hiyo aongee masuala ya wananchi. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo siipokei kwani waliyonituma hapa ni wananchi na nazungumzia wananchi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, basi naomba niende moja kwa moja kwenye mchango wangu. Kwanza nianze kwa kuwapongeza Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya na hapa niwe mkweli kwamba, suala zima linaloendelea kwa sasa na hasa kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya wachangiaji jana juu ya upandaji wa bei za mafuta katika nchi yetu hii ya Tanzania. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kwamba katika mfumo huu ambao umeanzishwa na upo, mimi kama Mbunge wa Jimbo la Msalala, naendelea kuwaomba waendelee kuuboresha mfumo huu wa uagizaji wa mafuta. Kwani ni mfumo ambao ni bora sana na hata nchi zingine za jirani wanakuja kuiga mfumo huu hapa Tanzania. Ukiangalia Nchi za Malawi, Zambia tayari wamekuja kujifunza namna bora ya Serikali ya Tanzania tunavyofanya katika uingizaji wa mafuta ya pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hoja ambazo zimeibuka kwamba soko la mafuta liwekwe huria na wapewe wawekezaji binafsi waweze kuingiza mafuta. Nataka tu niuambie umma wa Watanzania kwamba, suala zima la uingizaji mafuta kwa pamoja lina faida zake katika nchi yetu hii ya Tanzania. Moja ya faida ya uingizaji wa mafuta kwa pamoja ni national security. Leo hii tunaangalia Nchi za Rusia na Ukraine vita inayoendelea kule, leo kama nchi tukiiachia soko huria la mafuta, upi sasa uhai na usalama wa nchi yetu hii? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba watu tunaochangia katika suala zima hili la mafuta tuweke uzalendo mbele, kuhakikisha , kwamba tunachangia ili kuleta manufaa ya nchi yetu. Nimeona wengi katika suala hili la mafuta wanachangia kuangalia masilahi yao binafsi. Niseme tu kuanzia leo utaratibu huu uendelee kwa sababu, ni utaratibu ambao unalinda uhai na usalama wa nchi yetu. Pia, leo kama mafuta yataachiwa liwe soko huria, sisi kama wafanyabiashara… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Kassim Iddi ngoja kwanza ni kazi yangu kuwalinda Wabunge humu ndani. Wale wenye mawazo tofauti na ya kwako umewasema hapo kwa ujumla kwamba wanachangia kwa masilahi yao binafsi; na Kanuni zetu zinasema mtu akiwa na masilahi lazima ataje na maslahi yake ya kifedha.

Sasa nataka kukurahisishia una njia mbili; moja, ni ya kusisitiza kwamba wana maslahi, kwa hiyo, sisi tutawataka wao walete hayo maslahi ambayo na wewe unayajua. Au ni kuondoa hiyo kauli ili kila Mbunge humu ndani awe huru kutoa mawazo yake, lakini kama unao uhakika huo, basi utalisema kwa namna hiyo. (Makofi)

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, naomba kuondoa kauli hiyo, lakini niendelee kusisitiza kwamba, tunapokwenda kuchangia ni lazima tuangalie maslahi ya wananchi wetu ambao wametutuma.

Mheshimiwa Spika, niendelee kwa kusema kwamba upatikanaji wa mafuta kwa bei ambayo iliyopo sasa ni utaratibu ambao ni wa Serikali umeendelea kudhibiti mfumuko wa bei kupanda na kushuka na kuhakikisha kwamba, hao waagizaji wa mafuta wanaagiza kwa pamoja, sambamba na kutangazwa tender ya pamoja ili kuweza ku- control bei ya soko la Kimataifa. Kwani tunafahamu kwamba hata visima vya mafuta vinavyouza mafuta haviuzi moja kwa moja kwa muuzaji wa mafuta ama kampuni yoyote, isipokuwa wameteua ma-agent kwenye nchi zao huko ambao wanauza mafuta kwenye nchi nyingine hizi za jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee kusisitiza kwamba utaratibu huu Serikali iendelee kuuboresha vizuri, lakini niishauri tu kwamba hapa suala ni kuhakikisha ya kwamba wanajitahidi sasa, kuangalia zile gharama na kodi mbalimbali ambazo zimewekwa waweze kuzifanyia kazi, waziondoe ili kupunguza gharama ya mafuta. Tukumbuke sakata hili linafanana moja kwa moja na sakata la vinasaba. Wapo waliokuja hapa wakasema Kampuni ya GFI haifai inatunyonya na Serikali ilisikia ushauri huo ikaenda kuondoa na kuwapa TBS. Hata hivyo, baada ya siku tu kupita wale wale waliokuwa wanaipiga vita GFI walirudi wakaanza kusema kwamba sasa TBS haina uwezo, baada ya kuona sasa mianya ya mafuta yameanza kuingia ambayo yanachakachuliwa. Kwa hiyo, niombe tunapokwenda kujadili hili suala hasa katika kuzingatia usalama wa nchi yetu tuweke uzalendo mbele.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuchangia sasa upande wa TAMISEMI. Hali ya barabara katika maeneo yetu ni mbaya sana na hasa nizungumzie sasa kwenye Jimbo langu la Msalala. Barabara ni mbovu sana. Leo hii tunazungumzia ukuaji wa kilimo kwenye maeneo yetu, leo hii tunazungumzia ukuaji wa viwanda kwenye maeneo yetu, lakini vyote hivi haviwezi vikaenda sambamba kama miundombinu ya barabara haitarekebishwa. Niombe Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Naibu Waziri nadhani yupo hapo ananisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto kubwa sana kwenye maeneo yetu haya, hasa katika usimamizi wa fedha ambazo zinakwenda kwenye kukarabati barabara. Leo hii utaona tender nyingi za barabara zinatangazwa wakati wa mvua. Niendelee kuwaomba Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa pamoja waweke mkakati sasa wa fedha hizi ambazo tutakuwa tumezipitisha kwenye bajeti, ziende zikaendelee kukaa pale hata wakati wa mvua zisiende zikachukuliwa tena huko mbele. Pia, waweke usimamizi madhubuti katika kuhakikisha kwamba wakandarasi wanaopatikana kwenye maeneo yale ni wakandarasi ambao moja, wana sifa za kuhakikisha ya kwamba wanatekeleza miradi ile kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, wakandarasi hao wawe financially fit kwa ajili ya kuhakikisha kwamba miradi ile wanakwenda kuitekeleza bila kusuasua na wala kutegemea mikopo kwenye mabenki. Kwani kuwapa wakandarasi ambao hawana uwezo kwenye maeneo yetu ndio kunapelekea kucheleweshwa kwa barabara nyingi sana.

Mheshimiwa Spika, leo hii nitazungumzia miradi katika eneo langu la Kata ya Jana, Kata ya Mwaruguru, Kata ya Mwanase, maeneo haya ni wakulima wa mpunga. Nimpongeze Mheshimiwa Bashe kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kugawa vitendea kazi kama pikipiki na kuendelea kuthibitisha kwamba mama yetu Samia Suluhu ametoa fedha nyingi kwenye kilimo. Matunda hayo hayawezi yakaenda kuleta matokeo kama barabara zetu kwenye maeneo ya uzalishaji zitakuwa ni mbovu. Leo hii tunaongea barabara hizo hazipitiki. Niiombe Wizara wajaribu kuangalia namna gani na njia bora ya kuhakikisha kwamba barabara hizi zinaanza kutengenezwa mapema kabla ya mvua, ili wananchi sasa wa kwenye maeneo yale waendelee na uzalishaji katika maeneo hayo. (Makofi)