Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Napongeza maandalizi yote ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika hotuba hii ya bajeti utekelezaji na makadirio ya mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Spika, ningependa kuanza kwa nukuu ya baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliyeitoa katika speech yake, ilikuwa kwenye Kiingereza ikisema the situation and challenges of education in Tanzania tarehe 22 Oktoba, 1984. Katika nukuu hii alisema; not being selected to enter form one does not imply that they have failed yaani hao wanafunzi it is result of the very few form one places which exist.

Mheshimiwa Spika, hii maana yake ni nini? Nataka nitumie nafasi hii kuipongeza Serikali kwamba nyakati hizo tulikuwa tunakosa nafasi za kwenda kidato cha kwanza, sio sababu labda tulifeli, ni kwa sababu nafasi zilikuwa chache. Sasa napongeza Serikali kwa sababu tumejionea mwaka huu fedha tulizopata ambazo ni mkopo ambao of course tutalipa sisi wenyewe Watanzania, jinsi mgawanyo umeelekeza hadi kugusa maeneo ya elimu na hivyo watoto wetu kujiunga na kidato cha kwanza katika awamu moja bila kusubiri second or third selection. Napenda kupongeza sana Serikali katika jambo hili.

Mheshimiwa Spika, pia napenda kupongeza Serikali kwa shughuli ambazo zinaendelea katika majimbo mbalimbali ikiwemo Jimbo la Mafinga Mjini ambapo napongeza pia utaratibu wa kutujulisha Wabunge, hapa nina barua kutoka TAMISEMI ikinieleza kuhusu milioni 500 za ujenzi wa barabara katika Jimbo la Mafinga Mjini na kazi inayoendelea. Kwa hiyo sisi watu wa Mafinga tunaona pamoja na changamoto zingine zote, kazi iendelee tunaiona kwa vitendo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nijielekeze katika jambo hili ambalo hata mwaka jana nilisema. Kama Taifa, viko vitu lazima tujitosheleze ndani, nilisema kuhusu sukari, mafuta ya kula, bidhaa mbalimbali ambazo katika nyakati ngumu kama hizi ambazo zinazoendelea huko kwa wenzetu, maana yake kama tunajitosheleza hata kama ni kupanda kwa bei hakuwezi kupanda kwa bei kama unavyotegemea kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kazi ya Bunge mojawapo ni kushauri, sasa nashauri. Ukienda katika ukurasa wa 57 wa kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu anazungumza ambavyo Jeshi la Kujenga Taifa linafanya kazi nzuri ya ujenzi, kandarasi mbalimbali, nataka nishauri wakati wa amani duniani kote, wakati wa utulivu majeshi ya ulinzi kazi yake ni uzalishaji. Kwa hiyo nataka kushauri tuwape JKT hii kazi, nilikwenda na Kamati Chita nimejionea kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, tuna maeneo mengi yana rutuba, tuthubutu, for two years hatutaagiza mafuta kutoka nje, unless tutake wenyewe. Tulime alizeti za kutosha, tuwape kazi ya kutafiti mbegu zinazotakiwa, tulime ufuta, tutaondokana na kutumia mabilioni ya fedha kuagiza hizi bidhaa nje na bei kupanda. Tukifanya hivi, tutawapa wananchi wetu unafuu mkubwa sana katika Maisha. Kwa hiyo naomba na nashauri jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, ukienda pia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukurasa wa 80 unatoa msisitizo wa mambo muhimu katika mwaka wa fedha tunaoelekea, ni kutoa msukumo katika kutekeleza vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano na vipaumbele hivyo vinajumuisha kuchochea uchumi shindani na shirikishi. Pia kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza biashara na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, ninapozungumza hapa watu wa Mufindi, Mafinga, Njombe na Kilolo tuko katika hali ya taharuki baada ya kuambiwa kwamba Serikali sasa ina mpango wa kuanza kuagiza nguzo kutoka nje. Sasa sijajua kama kuagiza nguzo kutoka nje ina-reflect Mpango wetu wa Maendeleo wa Taifa kama ambavyo hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inaeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa miaka sita saba Serikali imetuamini tume-supply nguzo katika miradi ya REA, TANESCO. Hapa napenda nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa January Makamba, tulipopata taarifa hii nilimwendea na immediately akaitisha kikao baina ya wazalishaji, TANESCO na yeye, kutaka kujua ni sababu gani zinaifanya TANESCO ifikirie kuanza kuagiza nguzo kutoka nje, wakati hapa tunasema kwamba vipaumbele vya mpango wetu ni kuchochea uchumi shirikishi. Huu ni ushirikishwaji gani, nguzo tunazo unaagiza nguzo kutoka nje, ni kwa sababu gani.

Mheshimiwa Spika, katika kikao kile TANESCO wanasema kwamba ni suala la uwezo. Kwa mwaka uzalishaji wa nguzo ni zaidi ya milioni tatu, consumption ni milioni moja unawezaje kusema kwamba ni uwezo. Pili wanawema ubora, narejea hotuba ya Waziri Mkuu kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani, sasa kama ni suala la ubora uki-supply nguzo laki moja ukakuta nguzo 500 hazina ubora ni jambo la kawaida, hata viwandani soda kuna nyingine unakuta ziko flat. Kwa hiyo kama tuko serious kupunguza makali ya wananchi wetu, yako mambo ni lazima tuyasimamie kwa nia ya ile dhana tunayosema local content. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi ninapozungumza, kwa mfano, katika nguzo kuna chain kubwa ya uchumi. Yuko mtu ambaye anazalisha, ana shamba, yuko mtu anakuja kununua kwa mwenye shamba, yuko mtu atapewa kibarua cha kuangusha nguzo na kuzimenya, yuko mtu atapakia kwenye fuso, yuko mtu atasafirisha kwenda kiwandani, yuko mwenye kiwanda ata-treat atanunua dawa, yuko mwenye semi-trailer atasafirisha kwenda Mwanza, Kigoma na kadhalika. Hawa wote katika utendaji wao wa kazi pako sehemu wananunua mafuta. Wakinunua mafuta Serikali inapata fuel levy. Sasa chain yote hiyo all of a sudden tunataka tuiondoe. Je, tunaondokana na hili jambo la kujenga uchumi shirikishi na shindani?

T A A R I F A

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nataka tu kumtaarifu Mheshimiwa Cosato anapoendelea kuchangia kwamba katika Wilaya ya Kilolo tu peke yake kuna kiwanda cha nguzo kikubwa na kina wawekezaji wanatoka nje ya nchi, ambazo hizo hizo ndio nchi ambazo zinatarajiwa kuagizwa hizo nguzo na wanatumia mashine kama hizo hizo zilizoko kwenye hizo nchi. Kwa hiyo afahamu tu kwamba na wana nguzo za kutosha, hata hivi tunapozungumza ambazo hazijachukuliwa na Serikali. Nilitaka tu kumfahamisha hilo. Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa David Cosato Chumi, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hii na naongeza, Halmashauri zetu asilimia 60 ya own source zinategemea mazao ya misitu. Ninaposema mazao ya misitu ni nguzo, mirunda, mbao na mazao mengine kama plywood. Nguzo tu peke yake zina-make one third ya mapato yetu. Kwa mfano sisi Mafinga mapato ya ndani ni karibu bilioni 4.5. Maana yake unapoanza kuagiza nguzo kutoka nje unatuondolea mapato ya bilioni 1.5, ndio maana narejea hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, je, huku ndio kuchochea uchumi shirikishi na shindani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninachotaka nikiseme, kuwajengea wananchi wetu uwezo ni pamoja na local content kuifanya kwa vitendo, lakini kinyume chake huku kama tunavyosema, bei za mafuta zinapanda, bei za sukari zinapanda, lakini tena yale mazingira machache yanayowaongezea kipato nayo tunataka tuwanyang’anye, je tutajenga uchumi shindani na shirikishi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, itoshe tu kusema kwamba jambo hili Serikali ijitafakari na iliangalie mara mbili.