Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niwe mchangiaji wa kwanza katika hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mehshimiwa Rais, Mama Samia kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya kwenye majimbo na katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri Wabunge tutakubaliana kwamba kazi imefanyika, tumetoka kukagua miradi mikubwa na midogo hakuna mahali ambapo tumekuta mradi haujapelekewa fedha; hii ni hongera kubwa sana kwa mama na imedhihirisha kweli kwamba kinamama mkiwezeshwa mnaweza wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu, mimi ninatoka Kanda ya Ziwa, tulikuwa na miradi mikubwa sana kule mradi wa Daraja la Busisi, Hospitali ya Kanda ya Chato, Hospitali ya Musoma…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Musukuma kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Musukuma, kwamba tunashukuru anapo-appreciate kuhusu uongozi wa kinamama lakini najua wanawake tunaweza bila kuwezeshwa. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Musukuma nadhani alikuwa ananyoosha pale mwanzo, naamini ulikusudia kusema hiki ambacho amekisema Mheshimiwa Esther Matiko.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, akina mama ni mama zangu walionilea, siwezi kubishana nao. Ni kama alivyosema, na iwe hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miradi yote hii mikubwa niliyoitaja, imepelekewa fedha na inafanyika na inaendelea kukamilishwa. Hongera sana kwa Mama Samia na aendelea kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa ushauri. Njua Mheshimiwa Rais, ana majukumu mengi sana na ndiyo maana tukawa na mawaziri na Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, mnapopeleka fedha nyingi kwenye majimbo yetu, inahitaji ufuatiliaji wa karibu wa watu wenye maamuzi; namaanisha mawaziri. Sasa kumekuwa tabia ambazo nilizungumza hata juzi, ile kwamba Waziri anataka kutembelea halmashauri tano mpaka sita kwa siku, hii haina ufanisi mzuri katika kutusaidia kwenye fedha mnazozipeleka kwenye majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni vizuri mkaenda specifically kwenye halmashauri moja mkasikiliza siku nzima, mkaona miradi na kusikiliza matatizo ambayo yako kwenye ile halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba kumshauri Waziri Mkuu, ule utaratibu wake wa kupelekewa kero na kwenda kutatua moja kwa moja kwenye halmashauri, ningeomba aendelee nao. Ukisikiliza Wabunge wengi humu hawawezi tu kutamka moja kwa moja, kila Mbunge ana matatizo kwenye halmashauri yake, na ukileta Mawaziri unaambiwa mchakato unaendelea, tunaunda Tume, tume hazitoi majibu. Inakuwa kama tunapeleka fedha halafu kama hatuwezi kuzisimamia; bado Watanzania hawatatuelewa.

Mheshimiwa Spika, nimeona mtandaoni tangu jana au juzi, kuna clip inazunguka ya Mheshimiwa Mpina; na ninayezungumza ni mimi usiingie kwenye kumi na nane. Na ile clip imechukua sehemu ambayo imeashiria mimi nimezungumza kwenye mchango wangu, halafu imeunganishwa ikawepo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Mpina.

Mheshimiwa Spika, mimi kweli nililalamika sana kuhusiana na Bwawa la Mwalimu Nyerere kulingana na taarifa iliyoletwa na Waziri wa Nishati, na ni mjumbe wa Kamati. Baada ya yale majibu sikukata tamaa nilifuata utaratibu kwenda kwa Mwenyekiti, na Mwenyekiti na Wajumbe tukakubaliana tukakuomba kibali cha kwenda kuukagua mradi.

Mheshimiwa Spika, mimi ni balozi, naweza kusema ule mradi umeenda mara mbili ya ulivyokuwa umeachwa na Hayati Dkt. Magufuli, nimeenda kukagua mara nne. Kwa hiyo, tusitengenezeane ajali. Na sisi kama Kamati kwenye taarifa yetu mtaisikiliza mtaiona. Matatizo tuliyoyagundua si mradi, ni wataalam walimdanganya Waziri.

Mheshimiwa Spika, sasa nikisema mimi naomba ninukuliwe mimi, na mtu akitaka kutumia hansard yangu nina haki yangu kama Mbunge nisichukuliwe kwenda kutengeneza uzuri mtu.

Mheshimiwa Spika, mimi ni muathirika mkubwa sana wa Mheshimiwa Mpina. Nikimuangalia Mheshimiwa Mpina na hotuba aliyoitoa; mimi basi yangu mimi Mheshimiwa Mpina amei-cease mpaka leo inaozea kituoni, ilikutwa na Samaki watatu, hebu angalia samaki tatu... (Makofi)

T A A R I F A

MHE. DKT. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa najaribu kuieleza Serikali, kwamba mambo haya ni vizuri tukayaangalia vizuri, kwa sababu sisi Wabunge tunapokuwa tunalalamika, huwa wanaona wenzetu kule chini kama tunawaonea. Lakini unavyowatendea wenzio ukitendewa na wewe uvumilie msumari uingie.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba kushauri. Kama alivyozungumza Mbunge wa Arusha, Mheshimiwa Gambo, kwamba kuna mfumuko mkubwa wa bei. Hili ningeomba kutoa ushauri wangu kwenye Serikali kwamba ukiangalia leo bei ya mafuta tunanunua mpaka 3,000 huko Kijijini.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba Serikali ichukue suala hili kama suala la dharura, tuone namna, hata kama ni kupitisha bajeti ya dharura. Serikali yetu kwa sasa inakopesheka, tumefanya hivyo mara nyingi, ilishuka bei ya korosho Serikali tukakaa hapa tukaipitishia tukaenda ku- rescue suala la korosho, sasa kuna mfumuko wa bei ya mafuta (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua kuna fedha ambazo tuliweka kwa ajili ya miradi ya maji, tuliweka kwa ajili ya miradi ya barabara, tunaweza tukaona namna kama ni kiasi gani kimebaki tukaziondoa hata tukaenda kukopa ili tufidie.

Mheshimiwa Spika, kwa hali ya kawaida, mafuta shilingi 3000, na tunakoelekea yatapanda mpaka 3200 Serikali isikae kimya, kazi ya Serikali ni kuwalinda watu wake. Sasa hili lionwe kama suala la dharura ili kama kuna uwezekano, walete agenda yoyote ya dharura hapa tuweze kutafuta fedha yoyote tuweze kushuka mfumuko wa bei hasa kwenye mafuta.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la TARURA, kila Mbunge anaitegemea TARURA hapa. Ukienda ofisi ya TARURA hapa Makao Makuu utapishana na Wabunge 10, 20 kwa siku. Lakini kumekuwa na shida sana kwenye TARURA, ukisikiliza Waziri alienda pale wakasema wanaunda Tume hakuna mwelekeo.

Mheshimiwa Spila, leo sisi tunakuwa Wabunge wengine wawili kwenye halmashauri moja. wameondoa meneja wa kila halmashauri wameweka meneja wa Wilaya. Lakini unamuondoa yule uliyemshusha unambakisha pale pale na cheo ni kimoja, na wote walikuwa ni mameneja; kazi hazienda wilayani huko.

Mheshimiwa Spika, na ukiangalia, TARURA ndilo tegemeo letu kila mtu hapa ndani; tunatoa fedha nyingi; na leo Rais kawaongeza zaidi ya bilioni 900 lakini fedha walikuwa nazo, hata kipindi mwaka wa kwanza wamebaki na bilioni 72, mwaka wa pili bilioni 100, mwaka wa tatu bilioni 130, hizi ni ripoti CAG. Kwanini sasa tusione namna ya kuiboresha TARURA ikakaa vizuri ili hizi fedha zisibaki kama bakaa zitumike kwa sababu ukihoji humu kila mtu ana barabara mbovu. Lakini fedha zinabaki na bado tunaendelea kuwaongeza.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa mwisho, naomba sana; Mhesimiwa Shabiby alizungumza juzi hapa, suala la mafuta kuagiza kwa bulk procurement, hili suala hata kama tungeongeza hela bado mafuta hayawezi kushuka. Biashara huria ndio muoarobaini wa hili suala, aruhusiwe kila mtu alete mafuta, kazi yetu Serikali tukusanye kodi, kazi yetu Serikali ipime TBS mafuta ni mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mafuta yako mengi sana huko ya njia za panya yanini tungeshusha bei za mafuta. Sisi hatuna sababu ya kuanza kusimamia mafuta ya warabu, sisi tunachotaka ni mafuta yashuke bei. Tukiruhusu kila mtu alete mafuta watu wataunga na mitaji, wataleta mafuta ya wanavyojua wenyewe, sisi tutakusanya kodi na tutasimamia suala viwango, mafuta yatashuka bei. Nashukuru. (Makofi)