Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, ili niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Mawaziri wake, lakini pia ninapojikita Ofisi ya Waziri Mkuu naomba nizungumzie uchumi kwa wananchi mmoja-mmoja wetu kwa sababu ndiyo tunaowategemea zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii ardhi hatujaitumia kwa kilimo. Pamoja na jitihada mbalimbali ambazo zinafanywa na Wizara hii kubwa, tunapaswa tufikiri upya. Ardhi tuliyonayo yote inategemea mvua, lakini Mwenyezi Mungu ametupa mito, ametupa maziwa, ametupa maji ya chini pia, lakini wananchi wetu wanakuwa na likizo ya miezi sita bila sababu, wakati Mtumishi wa Serikali anakuwa na likizo ya mwezi mmoja kwa mwaka. Ili kuinua uchumi wananchi hawa wanastahili kufanya kazi ikiwezekana miezi kumi ili wapumzike miezi miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tuna upungufu wa mafuta, lakini mazao ambayo yanasababisha tupate mafuta yote tunategemea mvua, mfano michikichi, alizeti, pamba, yote inategemea mvua. Kwa hiyo, naomba ushauri wangu ni kwamba akili zetu zitumike, akili za watendaji zitumike na akili za viongozi zitumike.

Mheshimiwa Naibu Spika, mahali ambapo tuna mito, maji yatumike kwa ajili ya umwagiliaji ndiyo itakuwa mkombozi. Mahali ambapo hatuna mito tuna ziwa, milima itumike kutengeneza mabwawa juu ya mlima. Kama tunatengeneza matenki ya maji, tunashindwaje ku-pump maji kwenda mlimani na kushuka kwenye mashamba ambayo yako kwenye mwinuko hayo ya pamba, alizeti pamoja na michikichi, ili mwananchi aweze kuvuna mazao wakati wote? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo inapokosekana mvua mwananchi anapata hasara, Serikali inapata hasara, viwanda vinapata hasara kwa sababu vinakosa malighafi ya kuzalisha. Ajira inakufa, kodi inakosekana kwa hiyo, tufikiri upya kuona namna ya umwagiliaji tunaweza kuutumiaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mahali ambapo hakuna ziwa maji ya chini yatumike. Tunakwenda nchi za wenzetu zilizoendelea, mashamba yote kuna maji ya chini, maji yameelekezwa kwenye mashamba wananchi wanavuna masaa yote. Tubadilishe kilimo hiki kiwe kilimo ambacho wananchi kweli kinawasaidia, kwa sababu leo tunaweza kuwa tunalalamika mfumuko wa bei ni kwa sababu wananchi wetu hawana fedha, hawana kipato cha kukidhi kununua hayo mahitaji, kwa hiyo, tubadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hapa ije na mpango wa miaka mitano au miaka kumi kwa sababu jambo hili linahitaji fedha nyingi, lakini kama tutaendelea kutegemea mvua nataka nikuhakikishie hatutabadili kilimo chetu, tutapeleka pembejeo, tutapeleka mbolea, tutapeleka viuadudu, lakini kama hawana mvua ya kuivisha, hawana maji ya kuweza kuivisha, hawana maji ya kuweza kuivisha mazao, tunapiga kelele bure. Hatutakuwa tunasaidia wananchi. Multisectoral wenzangu sasa wafikiri hapa kwenye jambo hili ili waweze kuona nje ya box kuhakikisha wakulima hawa tunawasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili. Serikali imewekeza kwenye vituo vya afya, lakini vifaa muhimu ambavyo vinahitajika bado hafijafika. Liangaliwe jambo hili kwenye bajeti hii ili tuweze kupeleka vifaa kuvipunguzia hospitali za Wilaya majukumu yake kwa sababu, kuna vitu ambavyo vinapaswa viishie tu kwenye vituo vya afya, kama Kituo changu cha Kisesa ambacho kwa kweli kinahudumia watu wengi ni kama hospitali ya Wilaya, Mheshimiwa Ummy ananua jambo hili, lakini kituo changu cha Rugeye, Mheshimiwa Ummy anajua jambo hili, kituo cha Kabila, Mheshimiwa Ummy anajua jambo hili, Shishani kinachomalizika, Mheshimiwa Ummy anajua jambo hili. Kwa hiyo, Serikali ione namna ya kuweza kusaidia jambo hili liweze kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zetu zitengenezwe. TARURA tuiongezee fedha kama ambavyo wengine wamependekeza. Huko huduma wanayohitaji wananchi ni kusafirisha mazao yao, kusafiri wakati wote. Uchumi tunaposema umekua siyo fedha mfukoni bali miundombinu ambayo inawawezesha kusafirisha bidhaa zao ndiyo inayohitajika kwa hiyo, kwa kazi ambayo mwaka jana tumeifanya na mwaka huu wa bajeti unaoendelea, tuongeze fedha kwenye TARURA ili tuweze kufungua barabara nyingi zaidi na wananchi wetu waweze kusafirisha mizigo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapohitaji kuendeleza nchi lazima sisi sote tuamue. Hili jambo si la Rais peke yake, hili jambo ni la Watanzania wote. Kila mmoja mahali pake alipo tuamue kubadilisha mawazo yetu ili kuwahakikishia wananchi tunawasaidia kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)