Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kipekee namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai kwetu sote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kuunga mkono hoja ya Waziri Mkuu na niseme kwamba, wasilisho lilikuwa makini na tumelielewa vizuri, ila kuna mambo machache. Niende moja kwa moja katika ule ukurasa wa 28 ambapo amezungumzia yale mazao ya kimkakati, katika zao mojawapo lililotajwa pale ni zao la kahawa ambalo linalimwa Kilimanjaro na kwingineko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kusema kwamba, zao lile sasa ni kama halipo tena kwa sababu vitu vitatu ambapo kahawa inahitaji ni pamoja na maji ya kutosha, mbolea ya kutosha, lakini pia na ufanisi wa kusimamia. Ni bahati mbaya sana kwa ajili ya tabianchi ile mifereji ya asili sasa haipo tena na inahitaji ifufuliwe upya, lakini pia uoteshaji wa miti umekuwa hafifu ili maji yaendelee kutoka. Kwa hiyo, nimesimama kumuomba basi ili tunapoelekea kuweza kufufua tena kahawa wale Maafisa Ugani ambao wamepewa zile pikipiki juzi na Mheshimiwa Rais waweze kutembelea kaya kwa kaya ili waone kwamba, jambo hilo linafanyika. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jambo hilo jema na zito, jambo la maendeleo, kwa kuwapa hao Maafisa Ugani pikipiki hizo ili waweze kuwatembelea wakulima hao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo kwenye kilimo ningependa pia kuzungumzia mifugo. Toka niingie Bunge hili huwa kila nikisimama naomba wakati Marais wetu wanapokwenda nje waweze basi hata kutuombea sisi wanawake ambao tunafanya ufugaji wa zero grazing mitamba ambayo ni bora. Nakumbuka kabisa nikiwa mtoto Mwalimu Nyerere alikwenda huko Denmark, lakini pia Rais wa Kenya alikwenda na wa Uganda wote walikwenda safari mbalimbali, mitamba bora ikaja katika nchi zao tukaweza kupata cross breeding ya high breed kutoka katika ng’ombe wa jersey, phrasian, ng’ombe wakawa wanatoa maziwa bora sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya sana Kenya wanatoa maziwa mengi sasa hivi na wanauzia Tanzania, Uganda hali kadhalika, lakini Tanzania mazaiwa yetu ni kidogo pamoja na zile lita alizotuambia hapa leo asubuhi Waziri Mkuu katika ule ukurasa wa mifugo, lakini bado uzalishaji wa maziwa ni kidogo sana Tanzania. Kwa hiyo, ninaomba basi kwa wale ambao hawafugi ng’ombe wengi wa kuswaga wanawake wamekaa na wanawake wa Kilimanjaro wamenituma, ni lini watapatiwa mitamba bora kwa sababu, mtamba mmoja kutoka katika ranch ya Tanzania ni Shilingi Laki Nane, siyo rahisi kwa Mtanzania wa kawaida kwenda kununua mtamba kwa Shilingi Laki Nane ni hela nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba katika ule ukurasa wa kilimo wamezungumzia ushirika hiyo mitamba ipitishwe kwenye vyama vyetu vya ushirika kama zamani. Tukishapata ndama wakizalishwa ndama wazuri tunaambiwa kopa ng’ombe, lipa ndama kwa hiyo, tutarudi tena kule Mwalimu alikotuwezesha kulipa mitamba bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda pia kuzungumzia ule ugawaji wa ile asilimia 10. Tuna 4, 4, 2, lakini imekuwa ngumu sana kwa wale ambao wako kwenye vikundi kufaidika. Watu sasa Shilingi Laki Tano haitoshi kwa hiyo, kukopa kiasi cha Shilingi Milioni Mbili kwenye kikundi ni kitu kidogo, tumekiongea hapa, wenzangu wameongea kwa herufi kubwa, tulikuwa tunaomba sasa waruhusiwe kila mtu kukopa. Wakope na katika Wilaya ambazo zina hela za kutosha kama kule Ilala basi mtu aruhusiwe kukopa mwenyewe kutoka huko au agawiwe halafu arejeshe, kule ambako wapo wachache vikoba basi vipewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini imekuwa ni ngumu, wanawake hao wanapata mikopo kidogo sana. Makundi maalum, na ukikuta wenzetu ambao wana ulemavu wa viungo inakuwa ngumu, sasa wale wanakuaje kwenye kikundi? Tulikuwa tunaomba Serikali ikubali sasa watu wale wakopeshwe mmoja mmoja na arejeshe kama anavyopenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja ambalo linaniumiza kichwa na bahati nzuri niko kwenye Kamati ya Bajeti, zinaingia Wizara nyingi sana, lakini inaweza ikaingia Wizara wote ni suti, ni akina Baba tu mwanamke ni mmoja. Ninaiuliza Serikali ni lini italeta Muswada hapa Bungeni katika ajira za wanawake sasa ziwe hamsini kwa hamsini jumla? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana haiingii akilini tukianza chekechea tunaanza idadi moja wavulana na wasichana, sekondari tunaenda pamoja, chuo kikuu tunaenda pamoja, inapokuja kwenye ajira wanaopata promotion au kuonekana wanaweza zaidi ni wanaume. Ni wapi hapo mnapotuacha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mkienda vitani, wanaume wakienda vitani wanakwenda na sisi tunabaki nyumbani tunachunga nyumba. Hata ile vita ya Iddi Amin tuliiona, lakini wanaume wanakuja wanakuwa kwamba, wao ndiyo wawe kule kwenye, Wanajeshi wanasema beret, unapiga beret, sisi wanawake tuko tu chini. Imefika wakati sasa na ninamshukuru Mungu sana kwamba, tuna Rais mwanamke na tumeona wanawake wanaweza na wanaweza sana. Nasi sasa uletwe Muswada hapa waajiriwe hamsini kwa hamsini iwe ni kwenye ajira za Serikali… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Malizia.

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naona hilo jambo la hamsini kwa hamsini sasa lisiwe ni upendeleo ila lipite kisheria kabisa. Fifty-fifty ni wajibu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)