Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Kwanza nianze sana kwa kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kuwaletea Watanzania maendeleo; akiwemo Mtendaji Mkuu, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, ni kazi nzuri sana ambayo inafanywa kuwaletea maendeleo Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwe wakweli Waheshimiwa Wabunge, katika awamu zote ambazo nimekaa hapa Bungeni, hakuna kipindi tulichopata fedha nyingi katika Halmashauri zetu kama hiki. Tumepata fedha nyingi sana maendeleo. Ombi langu, sasa Waziri Mkuu yupo hapa, tumwambie Rais aende akakope tena fedha ili ziweze kujenga vyoo katika mashule yetu, ziweze kujenga nyumba za walimu katika maeneo yetu. Tumekosa nyumba na vyoo katika shule zetu na pia vifaatiba, Waheshimiwa Wabunge wamesema hapa, katika Vituo vya Afya, Zahanati na Hospitali ambazo zimejengwa. Sasa tukope fedha ili tutimize haya, shughuli ziweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu niwaambie, maendeleo yoyote hayawezi kwenda bila kukopa. Hayawezi kwenda. Hata mimi hapa mjasiriamali, nimekopa mabilioni ya fedha. Lazima ukope ndiyo shughuli zinakwenda. Kwa hiyo, lazima akope ili kusudi ziweze kufanya kazi za maendeleo katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Rais, Waheshimiwa Wabunge hawa na Waheshimiwa Madiwani wetu imebidi tuunge mkono jitihada za Rais. Katika maeneo yetu na sisi tumefanya maendeleo katika majimbo yetu. Nikianza na mimi mwenyewe, nimeunga mkono kwa kujenga madarasa tisa hivi sasa ambapo sasa mengine wanapiga ripu, mengine wanaezeka na mengine yamekwisha. Madarasa tisa kwa pamoja. Madarasa hayo ni kama ifuatavyo: Shule ya Kitisi, madarasa mawili; Shule ya Mwembetogwa, madarasa mawili na ofisi; Shule ya Uhuru, madarasa mawili; Shule ya Ilangamoto, darasa moja; Shule la Kifumbe, madarasa mawili. Jumla madarasa tisa. Madarasa hayo yote yatafunguliwa mwezi wa Sita mwaka huu 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, atakayefungua madarasa haya, wa Kwanza namwomba Mheshimiwa Bashungwa, Waziri wa TAMISEMI, aje afungue madarasa mawili na ofisi; Mkuu wa Mkoa, madarasa mawil; Mkuu wa Wilaya, madarasa mawili; Mwenyekiti wa TASAF wa Zanzibar, madarasa mawili ili Muungano uende vizuri. (Makofi/ Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, si hao tu, ASAS wa Iringa kutokana na jitihada za Rais ameunga mkono kwenye Jimbo la Makambako kujenga darasa moja katika Shule ya Magegere. Pia Mbunge mstaafu Haroun Mwambalali ameunga mkono kujenga darasa moja Majengo (Kilimahewa). Kwa hiyo, nawapongeza naomba kupitia kikao hiki Waziri mwenye dhamana wa TAMISEMI peleka barua kwa ASAS na Haroun kuwashukuru kwa kazi nzuri ambayo wameunga mkono jitihada za Rais. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye changamoto kwenye Jimbo la Makambako. Changamoto ya kwanza, kuna tatizo la fidia katika eneo la Polisi, kuna wananchi pale wanapata shida sana, fedha zilikuja wakasema ni kidogo, tukaomba ziongezwe, fedha zile zikahamishwa zikapelekwa Wanging’ombe. Tunaomba wapewe ili kusudi waondokane na tatizo hili. Fidia ya pili, Idofu kunatakiwa kujengwa one stop center wameshalipwa fidia shilingi milioni 800 bado sh.3,100,000,000/=. Ombi langu, tunaiomba Serikali ilete fedha ili waweze kulipwa wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za kujenga mradi mkubwa wa One stop center zipo tayari, Benki ya Dunia ilikwishatoa muda mrefu zili-expire wamerudia tena. Tatizo la tatu ni fidia umeme wa upepo Makambako, wananchi wale walishalipwa bado ambao hawajalipwa, tunaomba kupitia TANESCO waweze kulipa ili wananchi wale waweze kuondoka maeneo ambayo yanahitajika. La mwisho, la nne, soko la Kimataifa, Serikali ilishalipa fidia bado wananchi 18. Kwa hiyo, tunaomba waweze kulipwa ili kusudi kero hii iweze kuondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tano, wananchi wa Makambako wana matumaini makubwa juu ya miradi ile ya Miji 28. Tunaomba miradi hii imezungumzwa kwa muda mrefu sana. Ombi letu Wabunge tuliopitiwa na miradi hii ya Miji 28, tunaiomba Serikali sasa ifike mwisho miradi hii ianze ili wananchi waweze ku… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, sekunde.

NAIBU SPIKA: Haya sekunde moja.

MHE. DEO. K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho. Posho za Madiwani tunaomba ziongezwe. Madiwani wanafanya kazi nzuri sana za maendeleo katika maeneo yetu, tunaomba posho zao ziongezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Liganga na Mchuchuma tunaomba pia liweze kushughulikiwa. Naunga mkono hoja. (Makofi)