Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka mara ya mwisho kuchangia kwenye Bunge hili ilikuwa ni siku mbili kabla wewe Mwenyewe Mheshimiwa Naibu Spika hujagombea na tukakuchagua kuwa Naibu Spika wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo nimeona ni budi niweze kusimama hapa nikupongeze wewe mwenyewe kwa ushindi mzito ulioupata pamoja na Spika wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hongera sana kwa ushindi mnono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na pongezi hizo, naomba pia niweze kuchukua fursa hii kwenye dakika zangu za kuchangia kuweza kumpongeza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutenga muda na kufika Mkoa wa Kagera siku chache zilizopita ambapo alitoa maelekezo mahususi yenye lengo la kuwasaidia wakulima wa kahawa kwenye Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa ambayo wakulima wamekuwa wakidhulumiwa sana hasa wakulima wa kahawa. Kulikuwa na utitiri wa tozo mbalimbali ambapo mkulima wa kahawa anatozwa tozo 47; na matokeo ya tozo hizi ni kwamba mkulima alikuwa hanufaiki kabisa na zao lake la kahawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifika Kagera kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, akafuta tozo 42 kati ya 47 na kubakisha tozo tano tu. Hongereni sana Waziri Mkuu na Mheshimiwa Mama Samia. Wakulima wa Kahawa Mkoa wa Kagera na Tanzania kwa ujumla tunaahidi kuiunga mkono Serikali ya Mheshimiwa Mama Samia, tunaipenda na tunaomba iendelee kutuhudumia wakulima wa kahawa na kuhakikisha kwamba wakulima tunaendelea kunufaika na zao letu la kahawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na kuondoa tozo 42 kati ya 47, Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo mahsusi kwa Vyama vya Ushirika kuacha kwenda kuchukua mikopo ambapo mikopo ile mwisho wa siku inakwenda kulipwa na mkulima mwenyewe. Wakulima wa kahawa wanachokita, wanapoandaa mashamba yao, wanapopanda kahawa, zinakuja kutoa matunda baada ya miaka mitatu. Wakulima wanakuwa wamehenya kweli kweli, wanakuwa wameumia kweli kweli. Mkulima anachokitaka, anapovuna kahawa yake, aende kuiuza kwa bei nzuri. Naendelea kuipongeza Serikali ya Mheshimiwa Mama Samia, imetujali sisi wakulima kwa kuondoa tozo hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na kuondoa tozo hizi ambazo zilikuwa zinawakandamiza wakulima, Serikali imeelekeza Vyama vya Ushirika viache kwenda kuchukua mikopo kwa lengo la kwamba mikopo hiyo ilipwe na mkulima ambaye anapolima kahawa yake wala hajui kwamba kuna mtu atakwenda kuchukua mkopo ili kahawa yake ndiyo ilipe ule mkopo. Maelekezo haya yametolewa, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu iendelee kusimama maelekezo haya kuhakikisha kwamba wakulima wetu hawarudi kule walikotoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa maelekezo kwamba Vyama vya Msingi ndivyo viweze kusimamia uuzaji wa kahawa; na vyama vyote vya Ushirika…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba Serikali hii ni ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa nimeipokea na ndiyo maana nimeendelea kumpongeza Mama yetu tokea nianze kuchangia. Nakushukuru sana kwa taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nielekeze mchango wangu kwenye Fungu Na. 65 ambalo linahusu Mfuko wa kuwezesha vijana na hasa kwenye mchakato mzima wa kuwezesha vijana kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii kwa mwaka, vijana wanaohitimu Vyuo Vikuu…

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa tuwe na utulivu kidogo ndani.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Najua ni kengele ya kwanza.

NAIBU SPIKA: Wewe endelea tu.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Vijana wanaohitimu Vyuo Vikuu kwa mwaka wengine wamesema ni 90,000 lakini wale wanaomaliza Degree peke yake ni 48,000 na matokeo yake ni kwamba namba yote hii inapomaliza Vyuo Vikuu inarudi mtaani bila ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona juhudi nzuri za Ofisi ya Waziri Mkuu za kuhakikisha kwamba vijana hawa wanapotoka Vyuo Vikuu wanapatiwa ajira. Nimeomna ushirikiano baina ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Vyuo Vikuu ambapo tumesomewa kwamba wahitimu zaidi ya 2,000 wameweza kupatiwa mafunzo mbalimbali ya ujasiliamali na hivyo kuwawezesha kuanzisha miradi mbalimbali ya kujiajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba jukumu la Ofisi ya Waziri Mkuu ni pamoja na kutambua Makampuni ya Vijana na kushirikiana na PPRA na kusaidia makampuni haya kuyaunganisha na wazabuni wakubwa ili tender zinapokuwa zinatolewa vijana hawa na wenyewe waweze kunufaika na tender za nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Manunuzi ya Mwaka 2011 imeelekeza kwamba makundi maalum wakiwepo vijana, wanufaike na asilimia 30 ya fedha zote za zabuni, lakini katika uhalisia wake ni kwamba vijana wanaojua mambo haya au waliofahamishwa juu ya fursa hizi ni wachache sana na matokeo yake vijana wengi hawana ajira, tender za nchi hii zinaendelea kutolewa kwenye makampuni ya nje na mengine ya ndani makubwa, vijana wengi wameachwa pembeni kwenye utaratibu huu na kwenye mfumo huu wa zabuni za nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mfumo ukiwekwa vizuri na sheria hii ikasimamamiwa, tutawasaidia vijana wengi sana waweze kujiajiri kwenye mfumo wa tender, yaani zabuni na wengine wataweza kufanya shughuli za kandarasi. Sasa hivi tumewaachia vijana wako mtaani, wanashinda club house, wanaikosoa Serikali na kukosoa chama chetu na kusema maneno yanayohusiana na mambo ya kupingapinga, lakini zipo fursa za ku-drain vijana wengi tukawaingiza kwenye zabuni baada ya kuwatoa mitaani na tukawawezesha vijana wetu kujiajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa iliyopo ni utekelezaji wa sheria ya kutoa fursa kwenye makundi maalum nchi hii. Naomba kuishauri Serikali na hususan Ofisi ya Waziri Mkuu, iweke utaratibu mzuri wa kwenda kusimamia sheria zinazolinda maslahi ya makundi maalum ili kila tender inayotolewa nchi hii, kuwe na utaratibu wa tenderer kutoa taarifa ni kikundi gani amekihusisha kwenye zabuni yake na amekilipaje? Hii itahakikisha vijana wetu nchi hii wananufaika na zabuni zote zinatolewa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu iweke utaratibu maalum wa kukusanya taarifa na makampuni yote ya vijana kuhakikisha kwamba kila kampuni ya kijana iliyopo nchini hii inapata fursa hizi. Haya mambo hayafahamiki, vijana wetu hawanufaiki na hizi fursa, wapo kimya utadhani fursa hazipo, lakini zipo hazitangazwi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)