Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyoiongoza nchi yetu, lakini kwa namna anavyoifungua kiuchumi na kwa namna ambavyo ameamua kupanua demokrasia ya kweli, katika hatua hizi kwa kweli tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, nampongeza Makamu wa Rais pia, nampongeza pia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, lakini zaidi ya hapo nazipongeza Kamati zote tatu kwa taarifa ambazo wameziwasilisha humu ndani na uchambuzi wa kina ambao wameufanya kwa kweli nazipongeza sana Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kweli hotuba aliyoitoa humu Bungeni ime-set viwango vya juu sana, kwa sababu ime- cover maeneo yote, imechambua kwa undani maeneo yote ambayo yamefanyiwa kazi. Hii ni ishara tu ya mwaka mmoja ya Serikali ya Awamu ya Sita mambo ambayo imeyatekeleza, tukiendelea hivi kwa muda wa miaka minne ijayo nchi yetu itapiga hatua kubwa sana. Kwa hiyo mimi nawapongeza sana, naipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo wameifanya hapa tulipofika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona miradi mingi ya vielelezo, tumeona miradi mbalimbali, huduma za jamii kila mahali, kila eneo limeguswa katika mwaka huu tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo ambayo yamebaki ni mambo makubwa ambayo ni ya muhimu katika maendeleo ya nchi yetu, ambayo naamini kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inabidi itafute namna ambavyo tunaweza kufanya katika kutatua hizi changamoto. Changamoto ya kwanza ninayoiona ni tatizo la ajira kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tuna tatizo kubwa la ajira, vijana wengi wamesoma katika vyuo vikuu, wamesoma katika vyuo vya kati, wengi wana elimu lakini ajira imekuwa ni changamoto. Hali hii tusipoichukulia hatua, tusipoitafakari tukaja na mikakati ya kutosha litakuja kuwa ni bomu kubwa ambalo halitaisaidia nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nafikiri hiki ni kipindi pekee ambacho lazima tuangalie suala la ajira. Hili suala la ajira haliwezi kushughulikiwa na Serikali peke yake linahitaji sekta binafsi ambayo lazima iwe very strong ambayo ndiyo itaweza kuchukua vijana wengi wanaomaliza katika vyuo vyetu, tunahitaji kuwa na viwanda vingi na sekta mbalimbali zifanye vizuri ili ziweze kuajiri hawa vijana wengi ambao wamesoma katika taaluma mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali imeshasema tutatoa ajira zaidi ya 35,000, naipongeza sana Serikali kwa hatua hizo hongereni sana. Lakini hiyo itakuwa ni hatua moja, bado tunahitaji vijana wanaomaliza ni karibu takribani 90,000 mpaka 100,000 kwa mwaka, hiyo haitoshi. Pia sehemu wanayoenda kuajiri zaidi ni kwenye sekta ya Ualimu na Afya, zipo sehemu zingine, zipo taaluma zingine ambazo tunahitaji pia wawe na ajira, wanahitaji kutoa mchango mkubwa katika nchi yetu ambao bado ajira inaendelea kuwa tatizo. Kuna Wahasibu, kuna Wagavi, kuna Wahandisi, kuna Maafisa Utumishi na maeneo mengi kuna tatizo la ajira. Kwa hiyo, ninafikiri bado tunalo hilo tatizo ni lazima tulitafakari.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri Serikali iangalie kwa namna ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameratibu mambo mbalimbali, nashauri hata katika suala la ajira tuwe na mdahalo wa kitaifa wa kuzungumzia namna ya kutatua tatizo la ajira kwa vijana wetu ili kusudi Watanzania wote tushirikiane tuangalie kwa undani, tufanye nini ili kutoa ajira kwa Vijana wetu. Hiyo itatusaidia sana na tutaweza kujenga Taifa ambalo litakuwa linamanufaa na wataweza kufaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo ningependa kuchangia ni mishahara kwa Watumishi wa Umma. Katika kipindi cha takribani cha miaka mitano au Sita Watumishi wa Umma hawakuweza kuongezewa mishahara kwa sababu Serikali ilikuwa haina na uwezo, naamini tumefika mahali ili Watumishi wa Umma hawa waweze kufanya kazi yao vizuri, waweze kutekeleza majukumu mbalimbali, waweze kusimamia mipango mbalimbali ambayo Serikali inatakiwa kutekeleza wanahitaji pia kupewa motisha ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, Serikali sasa hivi iangalie namna itakavyoboresha maslahi ya Watumishi wa Umma. Ninalisema hivyo kwa sababu maslahi ya Watumishi wa Umma yakiboreshwa, wakiwa na mapato ya kutosha hawa pia watatoa ajira, kwa sababu hela wanazozipata wanaenda kuwekeza. Watawekeza kwenye kilimo, watawekeza kwenye miradi mbalimbali na ile miradi itatoa ajira kwa vijana mbalimbali. Kwa hiyo, zile pesa watakazozipata maslahi yakiboreshwa Watumishi wa Umma yataisaidia nchi katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali sasa ifike mahali katika Bajeti hii iwafikirie Watumishi wa Umma wote kuongezewa mishahara yao na nyongeza zile zinazotakiwa na maeneo mbalimbali ili maslahi na mazingira ya kazi yawe mazuri, yakiboreshwa mazingira ya kazi utendaji utakuwa mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni la msingi kwa sababu sasa hivi huko nyuma tulikuwa tunasema mteja ndiyo mfalme, sasa hivi wanasema rasilimali watu ndiyo mfalme katika Taasisi. Kwa hiyo, ukiimarisha hawa Watumishi wa Umma ukawapa motisha vizuri watakafanya kazi vizuri, watatekeleza malengo vizuri na nchi itapiga hatua kubwa. Kwa hiyo, napendekeza tuliangalie kwa makini suala hili la maslahi ya Watumishi wa Umma katika ngazi zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napendekeza tunapoangalia maslahi ya Watumishi wa Umma tuangalie na sekta binafsi, sekta binafsi sasa hivi tuna takribani miaka zaidi ya 13, kile kima cha chini cha mshahara havijawahi kurekebishwa kile cha kisheria. kisheria kima cha chini sekta zote hakijawahi kurekebishwa. Toka kimerekebishwa wakati huo kumetokea mabadiliko mengi, mfumuko wa bei, inflation rate imepanda sana, ukiangalia exchange rate, maisha yamebadilika. Fedha ambazo wanalipwa wafanyakazi wanaofanya sekta binafsi ni kidogo sana haziwawezeshi kuchangia katika Pato la Taifa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri ni vizuri Serikali sasa ikaangalia wafanyakazi wa sekta binafsi, na hasa kima cha chini cha sekta binafsi iwe ni kwenye kilimo, iwe ni kwenye uvuvi, iwe ni kwenye maeneo gani, maeneo yote ya sekta binafsi. Zipo sekta zaidi ya 12 ambazo tulipanga kima cha chini vya mishahara, sasa hivi kima cha chini sehemu nyingine tulisema ni shilingi laki moja toka mwaka 2013, tulisema Laki Moja mpaka leo wanalipa shilingi 100,000, hadi shilingi 150,000 ni nani anayeweza kuishi kwa kiwango hicho cha fedha? Ni wazi kabisa hawawezi katika kiwango hicho cha fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vizuri Serikali sasa ikaliangalia hili ili hawa maslahi yao yakiimarika sekta binafsi ndipo uchumi wetu utaimarika, hawa watakuwa na uwezo wa kununua bidhaa zetu na wakinunua bidhaa zetu uchumi utakua.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kunaweza kukawa na bidhaa, kunaweza kukawa na huduma lakini watu hawawezi ku-access hivyo kwa sababu hawana uwezo wa kumudu namna ya kununua hivyo vitu. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaliangalia hili suala la watumishi wa sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizingumzia ni kule Mkoani Songwe. Sasa hivi tunasema, bandari yetu hii, nchi nyingi zinatamani kuwa na Bandari kama ya Tanzania, lakini hazina hizo bandari. Sisi tunayo bandari na tuna maeneo mengi yenye bandari.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hapo, nchi ya Kongo imeingia kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nchi zote za Afrika Mashariki zinajiandaa sasa kufanya biashara ya DRC. Sehemu pekee ambayo tunaweza tukafanya biashara yetu vizuri ni kuangalia uwezekano wa kufungua Bandari Kavu pale Tunduma. Tukifungua Bandari Kavu pale Tunduma, itasaidia wale wa Congo, Zambia, Zimbabwe na nchi nyingine waweze kusafirishea mizigo yao kupitia TAZARA mpaka pale Tunduma halafu wanakuja kuchukua mizigo pale. Watafanya vizuri sana na uchumi wetu utaimarika vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashauri Serikali, ni vizuri ikaangalia uwezekano wa kufungua Bandari Kavu lakini sambamba na hilo iimarishe TAZARA yetu. Sasa hivi TAZARA inafanya vibaya; na inafanya vibaya kwa sababu hatujaipa uzito unaostahili. Hili shirika toka limeanzishwa ni la nchi mbili; wenzetu upande mwingine inawezekana wasione manufaa ya kuimarisha hii TAZARA, lakini kwa nchi kama ya kwetu ambayo uzalishaji mkubwa upo kwenye Nyanda za Juu Kusiniā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri, ahsante.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, naipongeza Serikali kwa hatua zote hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)