Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kutofuata Maelekezo ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kutofuata Maelekezo ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kama Mjumbe wa Kamati niweze kuchangia. Kwanza naunga mkono taarifa hiyo, na nataka kuchangia ile sehemu ya mwisho.

Mheshimiwa Spika, msingi wa changamoto ambayo tumeijadili hapa leo na siku iliyopita; moja, ni ukweli kwamba Waheshimiwa Wabunge pengine kuna haja ya kubadilisha tafsiri ya suala la anayestahili na asiyestahili. Hili ni tatizo ambalo limeendelea kujitokeza; na tulipoongea na bodi walikuwa wazi sana, kwamba kwa kweli wanafunzi wengi wanaoomba mikopo ya elimu ya juu wanastahili kupata mikopo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto ambayo ipo ni ukweli kwamba bajeti inakuwa haitoshi, ni kama sisi Waheshimiwa Wabunge tunapokwenda kugombea huko, wote wanaogombea wanastahili lakini sasa inabidi warudi watatu. Kwa hiyo, ni lazima utaratibu upatikane wapatikane watatu na hatimaye mmoja, lakini haimaanishi kwamba wale ambao hawakuteuliwa hawastahili.

Kwa hiyo, hata kwenye suala la mikopo tuliona kwa upana wake. Nitawapeni kidogo tathmini, Bodi ya Mikopo inapitia hatua tatu muhimu kabla haijatoa orodha. Kwanza inapokea majina ya watu waliomba, pili wanahakiki. Wakishahakiki wanachukua wale ambao wamepata udahili katika vyuo vikuu.

Mheshimiwa Spika, sasa katika mwaka 2021/2022 waliyoomba mikopo walikuwa 88,688, Bodi ikafanya uhakiki, waliokuwa na sifa zile ambazo bodi inazo wakawa 81,654. Hii ina maanisha kwamba kwa vigezo vya Bodi hawa wote walistahili kupata mikopo. Hata hivyo baadaye waliokuwa wamekidhi vigezo vya udahili katika vyuo vikuu na taasisi ya elimu za juu, kwa sababu unaweza ukawa na kigezo cha kukopa kumbe kule katika taasisi ya chuo kikuu haujapata sifa za udahili. Kwa hiyo, waliokidhi wakawa 74,312. Kati ya hawa Bodi iliwapa mikopo wanafunzi 70,603.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo utaona kwamba waliokosa hapa ni chini ya wanafunzi 3,000. Mwaka huu hali ikoje; mwaka wa fedha 2022/2023. Waliyoomba wanafunzi 97,760 baada ya uhakiki wa Bodi, waliostahili, wenye sifa za Bodi ni wanafunzi 85,876. Baada ya Bodi kufanya uhakiki kwa mujibu wa udahili, wanaostahili mwaka huu ni 80,502; lakini sasa mwaka huu bajeti wanayo kwa wanafunzi wa first year, kwa sababu tukumbuke Waheshimiwa Wabunge bajeti ambayo tulipitisha hapa ni bajeti ya shilingi bilioni 570 kama mwaka jana.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa sababu mwaka jana waliongezeka sana, ina maana wanafunzi wanaoendelea, wale waliokuwa wanaendelea haiwezekani ukawatoa lazima uwapate. Kwa hiyo, kwa sababu bajeti ni ile ile, katika wanafunzi 80,502 wanaostahili kupata mikopo mwaka huu, kwa mujibu wa bajeti sio kwa mujibu wa sifa, ni 42,000. Sijui kama mnanipata hapo? Wanafunzi 80,000 wanaostahili au wenye sifa za kupata mikopo na ambao wamefanyiwa uhakiki, lakini bajeti ambayo tunayo ni ya wanafunzi 42,000 ndio ambayo tunayo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, takriba wanafunzi 40,000 hawatapata mikopo, kwa hiyo ndiyo maana messages zimekuwa nyingi kwetu kuliko mwaka jana. Sasa, huu ndiyo msingi wa changamoto ambayo tunashughulika nayo, na ni muhimu kutibu tatizo badala ya kutibu dalili za tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri kwa taarifa ambayo Mheshimiwa Waziri alitupa; nadhani baadaye Serikali itapata nafasi ya kueleza kwamba wamewasiliana vizuri na Wizara ya Fedha na kuna maendeleo mazuri naamini kwa maelekezo yako Serikali itatoa maendeleo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, hiyo ndiyo changamoto, lakini habari njema ni kwamba…

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Kitila Mkumbo, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante, nilitaka kuongeza mnofu kidogo kwa Mheshimiwa Kitila kwamba lipo tatizo lingine ambalo linafanana na hilo. Kwamba mwanafunzi wa maskini ambaye hana uwezo wa kupeleka karo, amepewa sifa za kupewa mkopo na Bodi ya Mikopo lakini kigezo lazima afanye registration, ajisajili kwanza kwenye shule aliyopata ndipo wampe mkopo. Sasa kama hana hela ya kwenda kujisajili, maana yake chuo hakimtambui kama ana pesa za mkopo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kigezo nacho kitambulike kwamba kama kuna mwanafunzi maskini ana sifa za kupata mkopo na hana uwezo wa kujisajili, chuo kitambue kwamba mkopo wake wa asilimia mia kama amepewa, basi chuo kikubali apokee hiyo hela. Hela zikija ili aweze kujisajili, lakini wanamzuia, hawawezi kumpa mpaka ajisajili na hela hana. (Makofi)

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa muongozo huo mzuri na nitazingatia katika mchango wangu kwa dakika ambazo zimebaki. Tuliona sisi kama Kamati tukitoka hapa bila kugusia msingi wa tatizo, tutakuwa hatujatenda haki, lakini nashukuru kwa maelekezo yako.

Mheshimiwa Spika, sasa nichangie hilo la kwanza la mawasiliano. Mheshimiwa Waziri kwa maelezo yake na maelezo ya Bodi, alienda kwenye Bodi tarehe 12 Julai akatoa maelekezo na akaitambulisha Kamati ile ambayo ilikuwa ifanye kazi na Bodi wakaipokea.

Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida, katika utendaji wa Kiserikali, Waziri alishamaliza kazi yake. Ina maanisha kwamba baada ya hapo vyombo vingine vilivyofuata vilitakiwa vifuatilie. Kwa mfano, Waheshimiwa Mawaziri wanafahamu kwamba Katibu wake wa Mheshimiwa Waziri angemwandikia Katibu Mkuu, kwamba alipokuwa kwenye ziara tarehe hii na Mheshimiwa Waziri ametoa maelekezo, moja, mbili, tatu, naomba kuwasilisha kwa utekelezaji, hilo halikufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Bodi wamekuja kupokea maelekezo rasmi ya Wizara tarehe 31 Agosti. Na kwa kweli kwa ushahidi ya maelezo ya Bodi na nyaraka ambazo waliwasilisha, mara walipopokea maelekezo ya tarehe 31 Agosti walitekeleza lile agizo kwa kasi ambayo hata sisi Wajumbe ilitushangaza. Hata hiyo kazi haijaanza, basi Mwenyekiti wa Kamati ameandika barua Wizarani akieleza kwamba, sasa nimepokea na tupo tayari kuanza kazi tarehe 31 Oktoba, ambayo ni juzi. Bodi baada ya kupata kibali cha Wizara, mara moja walishalipa na hela ya advance ya Kamati kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo katika mazingira hayo, utakuta kwamba Kamati ilipata ugumu from documentary evidence kwamba ni lini uweze kuihukumu Bodi kwamba imekwamisha maelekezo ya Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, kuna changamoto hiyo ya mawasiliano ambayo tumeieleza na tumetoa mapendekezo ambayo tumeyatoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)